Hiki ndicho kipindi kigumu kwa mwanamke kuliko wakati mwingine wowote

Muktasari:

Kipindi hicho huwa na umuhimu mkubwa kwa mama mwenyewe na mtoto aliyembeba tumboni. Tukumbuke kuwa utunzaji wa ujauzito si jukumu la mama peke yake, bali pia baba wa mtoto, ndugu na jamaa wote wa karibu wanaoishi na mjamzito huyo.

Katika maisha ya mwanamke hapa duniani kipindi muhimu ambacho anahitaji uangalizi wa hali ya juu kuliko wakati mwingine wowote ni kile cha ujauzito.

Kipindi hicho huwa na umuhimu mkubwa kwa mama mwenyewe na mtoto aliyembeba tumboni. Tukumbuke kuwa utunzaji wa ujauzito si jukumu la mama peke yake, bali pia baba wa mtoto, ndugu na jamaa wote wa karibu wanaoishi na mjamzito huyo.

Tunaambiwa kuwa kila mwaka takribani wanawake milioni 21 walio na miaka kati ya 15 hadi 19, na milioni mbili walio na umri chini ya miaka 15 hubeba mimba katika nchi zinazoendelea. Inakadiriwa pia wasichana milioni 16 walio na umri kati ya miaka 15 na 19 pamoja na milioni 2.5 walio na umri wa chini ya miaka 16 hujifungua kila mwaka katika nchi zinazoendelea.

Pia inkadiriwa kuwa wasichana milioni 3.9 walio na umri kati ya 15 hadi 19 hutoa mimba bila sababu maalumu za kiafya.

Kuna mambo mbalimbali ambayo mjamzito pamoja na ndugu wanaoishi karibu yake wanapaswa kuyazingatia na kuyatilia mkazo katika kipindi hicho.

Moja ni kuhudhuria katika kituo cha afya kilicho karibu yake kwa ajili ya kupata huduma za kliniki kutokana na maagizo atakayokuwa amepewa na wauguzi wa afya. Huduma za kliniki huhusisha mambo muhimu kama ya upimaji wa maaambukizi ya virusi vya Ukimwi, maradhi ya zinaa kama kaswende na kisonono ambayo ni hatari kwa mama pamoja na mtoto wakati wa ujauzito. Wataalamu wa afya wanasema maradhi hayo huweza kusababisha mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya kimaumbile na hata chini ya uzito wa kawaida.

Lakini ili kukabilia na changamoto hizo, mjamzito anatakiwa kupata chanjo za muhimu kama za tetenasi, homa ya ini na dawa za kuongeza damu.

Ni lazima mjamzito ahimizwe kupata chanjo hizo ambazo pia huzuia kupata tatizo la anemia yaani upungufu wa damu mwilini. Pili kipindi mama akiwa mjamzito, anatakiwa apate lishe bora. Ni jambo la muhimu kufahamu kwamba mahitaji ya mwili huongezeka mara abebapo ujauzito.

Yeye huhitaji virutubisho na mtoto aliyeko tumboni naye huvipata virutubisho hivyo kupitia kwa mama. Hivyo akivikosa, hata mtoto naye anavikosa.

Hivyo mjamzito anatikiwa apatiwe virutubisho vya kutosha kukidhi mahitaji yake na ya mtoto aliyeko tumboni.

Madhara gani yanaweza kutokea kama mjamzito atavikosa vitu hivyo?

Wataalamu wa afya ya mama na mtoto wanasema kama mama hatapata virutubisho na chanjo zote kwa ukamilifu, kuna hatari ya kujifungua mtoto aliye na uzito mdogo. Pia, mama hataweza kutoa maziwa ya kutosha kumnyonyesha mtoto wake baada ya kujifungua.

Moja ya tatatizo kubwa linalowakabili wanawake wengi katika kipindi cha ujauzito linalohusisha lishe ni upungufu wa damu. Hali hii hujitokeza pale lishe ya madini ya chuma na protini kuwa pungufu kwenye mwili wa mama.

Vitu hivyo viwili ni muhimu sana katika utengenezaji wa chembe chembe nyekundu za damu. Hivyo, inashauliwa mjamzito ale mbogamboga kwa wingi, vitoweo kama nyama na maini kwa wingi ili kiwango chake cha damu kisishuke.

Inashauriwa pia ale matunda kwa wingi ili kulinda damu yake isipungu hata baada ya kujifungua.

Wapo wajawazito wengine hupoteza damu nyingi kipindi cha kujifungua na kujikuta akikumbwa na shida ya upungufu mkubwa wa damu na kuhatarisha uhai wake.

Je kwa wale wenye tabia ya utumiaji wa vilevi na uvutaji wa sigara wanatakiwa kufanya nini?

Mjamzito anashuriwa aachane na matumizi ya bidhaa za tumbaku, dawa za kulevya pamoja na ulevi. Mambo hayo yanaweza kumsababishia akajifungua mtoto njiti au mwenye mtindio wa ubongo. Pia mzunguko wa damu kwenye mwili wa mtoto unaweza ukaathiriwa hasa upande wa kulia unaopeleka damu kwenye mapafu. Lakini madhara ya sigara huchangia mama kuchelewa kujifungua au mtoto anaweza kupata matatizo kwenye mfumo wake wa chakula.

Pia matumizi ya vitu hivyo husababisha kondo la nyuma kujitenga na mfuko wa uzazi wakati wa kujifungua na kumsababishia mama kuvuja damu ndani kwa ndani.

Lakini sigara huathiri figo za mtoto na ni moja ya chanzo kinachosababisha mtoto kupoteza maisha ghafla baada ya kuzaliwa au kufia tumboni.

Umuhimu wa mazoezi kipindi cha ujauzito Suala la mazoezi wakati wa ujauzito huwa na umuhimu wake. Kwasababu humsaidia mjamzito kwa wale wenye hali ya msongo wa mawazo kupunguza kama si kumaliza kabisa hali hiyo. Kutembea kipindi cha ujauzito ni moja ya mazoezi badala ya kushinda kitandani au kukaa sehemu moja. Mazoezi hupunguza hatari ya kupatwa na matatizo wakati wa kujifungua mfano halisi ni kwa wale wanawake walio na kisukari huwapunguzia hatari ya kujifungua watoto wakubwa kwa njia ya upasuaji.

Matumizi ya vyandarua

Mjamzito anahimizwa kutumia chandarua ili ajikinde na malaria.

Ugonjwa huo ni miongoni mwa maradhi hatari yanayosababisha vifo vingi vya mama na mtoto.