Hatari ya ‘wallet’ kwa afya ya mwanaume

Dar es Salaam. Wanaume wengi hupendelea kutumia wallet (pochi) kuhifadhia fedha, kadi za mawasiliano na vitu vidogo muhimu. Wengi wana utaratibu wa kuweka mfuko wa nyuma wa suruali.

Kwa wale wanaojaza fedha katika wallet zao, wataalamu wa mifupa na mishipa ya fahamu wamebainisha hatari ya kupata maumivu ya mgongo na kiuno yasiyoisha, yanayochangiwa na mkao mbaya au kukaa upande.

Licha ya changamoto ya mgongo, wataalamu wa afya wameonya pia tabia za wengi wao kutozitakasa, hivyo kuwa rahisi kubeba bakteria wa magonjwa mbalimbali.

Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) imesema zaidi ya asilimia 60 ya wanaume wanaotibiwa migongo katika taasisi hiyo, tatizo lao halikusababishwa na ajali bali ni changamoto mbalimbali na kazi wanazozifanya.

Akizungumza na Mwananchi, Daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa Taasisi ya Mifupa MOI, Dk Kennedy Nchimbi anasema wallets kubwa kwenye mifuko ya suruali za wanaume huharibu uwiano wa mwili kwa kuigeuza mifupa ya nyonga.

Anasema utaratibu huo huweka mgandamizo mkubwa kwenye uti wa mgongo hivyo kuzifanya pingili zake zijisogeze kutoka kwenye mpangilio wake wa kawaida.

“Wallet ni kihifadhio cha vitu lakini kinachohusiana na mgongo, ni wapi unaiweka ndiyo tatizo lilipo. Wanaume wengi huziweka mfuko wa nyuma na kutengeneza mwinuko, kiuno kinakaa upande na kiuno ndiyo mgongo huohuo,” anasisitiza.

Dk Nchimbi anasema akikaa upande athari inakuja kwenye mgongo, husababisha matatizo makubwa ya uti wa mgongo pamoja na maumivu ya nyonga na mgongo kwa wanaume wengi pasipo kuelewa nini chanzo cha tatizo hili.

“Unaweza usiyaone moja kwa moja ndani ya muda mfupi, lakini yakatokea muda mrefu baadaye,” anasema na kueleza kuwa mara nyingi waathirika hupatiwa tiba ya dawa za vidonge, sindano na mazoezi tiba.

“Nashauri wanaume waache kuweka pochi nyuma ya mfuko wa suruali, waweza kuiweka popote hatushauri uweke mfuko wa nyuma. MOI tunaona wanaume wanakuja wamepata matatizo ya mgongo zaidi ya asilimia 60, haijasababishwa na ajali wengi ni changanmoto na kazi wanazozifanya,” anasema.

Daktari wa Ubongo na Uti wa Mgongo MOI, Nicephorus Rutabasibwa anasema kuna mshipa wa fahamu ujulikanao kitaalamu kama Sciatic Nerve unaotoka kwenye uti wa mgongo kuelekea mguuni, kupitia kwenye mfupa wa kiuno.

“Sasa kama umeweka wallet iliyotuna sana katika mfuko wa nyuma wa suruali uliyovaa na ukakaa nayo, basi ule uzito unaweza kukandamiza mshipa wa Sciatic Nerve na kusababisha ganzi na maumivu kwenye mguu, pia unaleta maumivu katika mgongo kwa sababu mshipa huo unakua umeshatoka kuelekea kwenye mguu,” anasema Dk Rutabasibwa.

Anataja madhara mengine anayoweza kupata mtu kama atakalia pochi iliyojaa ni kupata maumivu yanayoambatana na ganzi.


Baadhi waacha kuzitumia

Hata hivyo baadhi yao wamesema wameacha matumizi ya wallet kutokana na sababu mbalimbali huku wengine wakizitaja za kiafya.

“Nina vitu vingi sana vya kubeba, hivyo niliamua kuachana na wallet kwa sasa natumia mifuko kuweka fedha, vitambulisho na kadi mbalimbali nahifadhi kwenye gari na zingine nacha ofisini,” anasema Mohammed Omary mkazi wa Tanga.

Mkazi wa Dar es Salaam, Japhet John anasema, “Situmii wallet kwa sababu huwa zinanipotezea pesa zangu, niliwahi kutumia mara moja ambayo niliweka hela lakini baada ya hapo nikasahau nilipoiweka.”


Saikolojia

Mtaalamu wa saikolojia Saldin Kimangale anasema wanaume hupenda wepesi kiasi inachowezekana, hivyo hufanya juhudi kubwa kupunguza chochote kitakachowaletea uzito na ndiyo hulka yao.

“Begi kwa mwanaume ni mzigo, kwa hivyo kuwa na pochi (wallet) ambayo inaweza kuhifadhi kadi na pesa maana yake ni kuwa hilo ni jambo linalopendeza zaidi kwa mwanaume,” anasema.

Kimangale anasema kuhusu kuumia mgongo, mbali na kutoamini jambo hilo na kuliona kuwa hutokea kwa nadra tena kwa watu wengine, bado unahitajika utayari kujifunza namna ya kujisaidia ili kuondokana na madhara ya pochi lake lakini sio kuacha pochi.

“Kuna suala pia la usalama wa pochi na pahala anapoiweka na wepesi wa kuitumia ni msukumo mwingine wa kumfanya mwanaume apendelee zaidi matumizi ya pochi na kuiweka mfuko wa nyuma. Lakini begi au pochi la kiunoni ni salama zaidi kwa mwanaume,” anasema Kimangale.