Wenje, Msigwa, Pambalu waliamsha fomu Chadema

Muktasari:

  • Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema, kinaendelea na uchaguzi ngazi ya Kanda kwa wagombea na wafuasi wanaowaunga mkono kuchukua fomu kuanzia Aprili 12-22, 2024.

Iringa. Mtindo wa wapigakura kuwachukulia fomu wagombea ndilo jambo linaloonekana kuchukua nafasi kwenye awamu ya kwanza ya uchaguzi wa kanda za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) unahusisha kanda nne.

Katika mchakato wa kuelekea uchaguzi huo, imeshuhudiwa wafuasi mbalimbali wakiwalipia ada za fomu na kuwachukulia wagombea mbalimbali wanaowaunga mkono.

Hilo limeshuhudiwa jana Jumanne Aprili 16, 2024 kwa nyakati tofauti ambapo wafuasi wa wagombea wawili kati ya wanaowania uenyeviti, kwenda makao makuu ya kanda na kuwachukulia fomu wapendwa wao.

Wagombea waliochukuliwa fomu na wafuasi ni Ezekiah Wenje anayetetea kiti cha uenyekiti wa Kanda ya Victoria na Mchungaji Peter Msigwa anayetetea nafasi hiyo Kanda ya Nyasa.

Mtazamo wa wanazuoni wa sayansi ya siasa kuhusu jambo hilo, ni kuwa halina taswira mbaya lakini linaweza kugeuka kuwa baya iwapo wanaofanya hivyo wana sababu za kidini au kikabila.

Dirisha la uchukuaji na urejeshaji fomu kuwania nafasi za uenyekiti wa kanda, makamu mwenyekiti na mweka hazina lilifunguliwa Aprili 12 na litafungwa Aprili 22, 2024 katika kanda husika.

Jana Jumanne, makada zaidi ya 50 wanaomuunga mkono Wenje wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Geita, Deo Shinyanga walimchukulia fomu mwenyekiti huyo anayemaliza muda wake.

Katika maelekezo yake, Shinyanga amesema waliokwenda kuchukua fomu hiyo ni wanachama kutoka majimbo 25 ya mikoa ya Geita, Kagera na Mwanza.

Mbali na kumsindikiza, Shinyanga alisema walichanga fedha kwa ajili ya kulipia fomu hiyo ambayo gharama yake ni Sh100,000.

Msingi wa kuyafanya yote hayo ni kile walichoeleza, mwanasiasa huyo amekuwa mwaminifu ndani ya chama hicho tangu alipotoka bungeni mwaka 2015 bila kurudi nyuma.

“Tunao watu tuliwaamini kwa viwango vikubwa lakini mwisho wa siku wametufedhehesha, lakini Wenje amesimama. Tulikuwa na wenyeviti wa kanda na wamesaliti chama kwa vipande vya fedha,” amesema Shinyanga.

Kwa mujibu wa Shinyanga, Wenje amesimama na chama hicho katika nyakati zote za furaha na zile ngumu hivyo, wanamuona anastahili wadhifa huo.

“Tumeamua kumfariji kwa kumuunga mkono kwa aliyoyafanya kwa Chadema,” amesema.

Pamoja na Wenje, wanaowania nafasi hiyo katika kanda hiyo ni Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Pambalu.

Hata hivyo, Mwananchi imearifiwa tayari Pambalu ameshachukua fomu katika ofisi za chama hicho mkoani Kagera, akiambatana na wafuasi wake 100, lakini yeye alikwenda kuchukua mwenyewe.

"Nimeamua kuchukua mwenyewe bila kutuma watu, kinachofuata ni kuijaza na kuirejesha kisha nasubiri uteuzi katika ngazi husika," amesema Pambalu.

Msigwa naye anacho kibarua cha kuchuana na Mbunge wa zamani wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ katika Kanda hiyo ya Nyasa.

Akizungumza baada ya kuchukuliwa fomu, Mchungaji Msigwa amesema "Ni heshima kwangu kwa watu wanaoniunga mkono kuchanga fedha na kunichukulia fomu naheshimu uamuzi wao. Nina thamani mchango wao wamenipa nguvu zaidi ya kuongeza kasi ta kutekeleza majukumu yangu nitakapoibuka kidedea."

Mbali na hao, mgombea mwingine wa nafasi hiyo ni Emmanuel Ntobi aliyesema atakwenda kuchukua fomu mwenyewe na wakati wa kuirudisha ndipo ataambatana na wapambe.

"Kesho nitakwenda kuchukua fomu, nimedhamiria kuleta mageuzi katika Kanda ya Serengeti," amesema Ntobi ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema mkoani Shinyanga.

Mwanazuoni wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema hilo si jambo baya iwapo msingi wake ni mapenzi ya wafuasi kwa mgombea husika.

Lakini, amesema itakuwa mbaya iwapo wanaoamua kumchukulia fomu mgombea huyo wanashinikizwa na sababu za kikabila au udini.

“Kama msingi wa wafuasi wanaomchukulia fomu mgombea ni kwa sababu wanapenda misimamo na uongozi wake, ni dhahiri baada ya uchaguzi hakutakuwa na mpasuko.

“Lakini itakuwa mbaya iwapo watu wanamchukulia mtu kwa vigezo vya kidini na kikabila, kwa maana nchi yetu inaweza kutengeneza tatizo kubwa kwenye siasa,” amesema.

Kadhalika, mwanazuoni huyo amesema kwa mtazamo wa siasa za Tanzania, jambo hilo linachagiza uchaguzi na kuonyesha nani anapendwa zaidi.


Ratiba ya uchaguzi

Uchaguzi huo wa Chadema, utahusisha Kanda nne za awali Victoria – Serengeti, Magharibi na Nyasa na unatarajiwa kufanyika Mei 2024.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho bara, Benson Kigaila, nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo ni mwenyekiti wak, makamu mwenyekiti na mweka hazina wa kanda.

Kwa upande wa mabaraza ya chama Bazecha, Bawacha na Bavicha nafasi zinazoshindaniwa ni mwenyekiti wa Kanda, makamu wake, katibu wa mweka mazina.


Uchaguzi wa awamu

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema amesema “uchaguzi wetu unafanyika kwa awamu mbalimbali, hivyo kanda hizo ndio awamu ya kwanza ya uchaguzi wa kanda.”

“Baadaye itafuata awamu ya pili ambayo itahusisha kanda nyingine zilizobakia, kisha uchaguzi wa ngazi ya Taifa utafuata baada ya kanda zote kukamilisha uchaguzi.