Wazee Lindi wachoka kukaa nyumba isiyo na umeme

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Natalis Linuma amesema Serikali inatambua changamoto hiyo na kwamba wataifanyia kazi haraka.

Lindi. Wazee wanaolelewa kwenye Kambi ya Rasbula Manispaa ya Lindi mkoani hapa, wameiomba Serikali ikarabati nyumba wanayoishi na iwekewe umeme wakidai wamechoka kuishi kwenye nyumba chakavu isiyo na nishati hiyo.

Hayo wamesema  leo Jumatano Aprili 24,2024, baada ya kukabidhiwa msaada wa vyakula, magodoro na nguo  kutoka serikalini na kwa wadau.

Selemani Hamisi, mlezi wa kituo hicho amesema: "Leo mmekuja hakuna mvua, lakini mngekuja wakati mvua inanyesha mngeona jinsi nyumba inavyovuja na hakuna hata umeme, tunatumia umeme wa jua, mvua ikinyesha tu hakuna mwanga, tunaomba Serikali ya mkoa itusaidie,” amesema Hamisi.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Lindi, Natalis Linuma amesema Serikali inatambua changamoto hiyo wataifanyia kazi haraka.

Hata hivyo, ametoa rai kwa wazee hao na wananchi kwa jumla kuendelea kuuenzi Muungano kwa kudumisha amani na utulivu nchini.

"Serikali inawatambua wazee na kuwathamini ndiyo maana tumekuja kuwaletea misaada mbalimbali kusudi tusherehekee Muungano wetu, niwaombe wazee wangu tuendelee kuudumisha,” amesema Linuma.

Katibu Tawala Wilaya ya Lindi, Hudhaifa Rashidi amesema changamoto za wazee hao wamezichukua na watakwenda kuzifanyia kazi.

"Tutahakikisha kituo hiki tunakiboresha vizuri, pia  kiwe kwenye mandhari nzuri, tunataka kuwaenzi hawa wazee, lazima sisi kama wilaya tuhakikishe mazingira wanamoishi ni salama ili tukisema tunaenzi miaka 60 ya Muungano tuwe tunaakisi jambo hilo kwa uzito wake,” amesema Rashidi.

Fatuma Boli, mzee anayelelewa kambini hapo ameishukuru Serikali na wadau kwa kujitolea kuwaletea misaada ya chakula.

"Tunaishukuru Serikali pamoja na wadau kwa kutukumbuka sisi wazee ili tusherehekee pamoja miaka sitini ya Muungano,” amesema Fatuma.

Wakati huohuo, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Lindi, Dominic Bymungu amewashukuru wadau kwa kujitoa kuwaletea vyakula kwenye magereza yao.

Pia,  amewaomba wasiishie kwenye sherehe za kitaifa bali wawe wanatoa hata nyakati za kawaida.

“Tunawashukuru sana wadau pamoja na Serikali kwa kutukumbuka kutuletea vyakula, muendelezo huu uendelee hata kwa nyakati zingine,” amesema Bymungu.