Wazazi watajwa kuwafanyia ukatili watoto 739 Mwanza

Makamu Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net) mkoa wa Mwanza, Aziza Msangi akizungumza wakati wanachama wa mtandao huo walipotembelea na kutoa msaada katika kituo cha kulea watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia cha Foundation Karibu Tanzania kilichopo Kilimahewa wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa asilimia 80 ya watoto wanaofanyiwa ukatili, hufanyiwa na wazazi wao.

Mwanza. Imebainika watoto 739 kati ya 924 waliofanyiwa ukatili wa kijinsia mkoani Mwanza, wamefanyiwa ukatili huo na wazazi wao.

Takwimu hizo zimetolewa leo Alhamisi, Machi 7, 2024, wakati wanachama wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net) Mkoa wa Mwanza walipotembelea kituo cha watoto waliofanyiwa ukatili cha Foundation Karibu Tanzania (FKT) kilichopo Kilimahewa wilayani Ilemela mkoani humo.

Watoto hao ni waliofikishwa katika Dawati la Jinsia mkoani humo, kisha kupelekwa kwa ajili ya uangalizi, matibabu na malezi maalumu katika kituo hicho kuanzia mwaka 2007 hadi 2024.

Mkurugenzi wa kituo hicho, Asunta Ngatunga ametaja ukatili waliofanyiwa kuwa ni pamoja na kubakwa na kulawitiwa (zaidi ya watoto 50) huku wengine wakishushiwa vipigo, kuchomwa moto na mashambulio ya aibu.

“Watoto wengi tunaowapokea hapa tukisema wamebakwa, wanabakwa na wazazi wao wa kuwazaa, tunaposema wamechomwa mtoto na vipigo kwa asilimia 80 ni wazazi wao, asilimia 20 ndiyo watu baki.

“Jamii ifichue ukatili katika maeneo yao kuliko wanavyokaa kimya, ili kuwasaidia wapate haki zao. Unapokaa kimya mwisho wa siku mtoto anapoteza uhai na baadhi ya viungo vya mwili,” amesema Ngatunga.

Mwenyekiti wa TPF Net mkoa wa Mwanza, Virginia Sodoka (aliyeshika sabuni kulia) akimkabidhi sabuni na mahitaji mengine ya kibinadamu, mkurugenzi wa kituo cha kulea watoto waliofanyiwa ukatili wa kijinsia cha Foundation Karibu Tanzania (FKT), Asunta Ngatunga (kushoto). Picha na Mgongo Kaitira

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TPF Net mkoa wa Mwanza, Virginia Sodoka amesema; “Kwenye vituo vyetu hatuna eneo la kuwaweka watoto waliofanyiwa ukatili, kwa hiyo tunashirikiana na wadau ambao wana makazi salama wakiwemo hawa FKT,”

Wakati matukio hayo yakiripotiwa, Makamu Mwenyekiti wa TPF Net mkoa wa Mwanza, Aziza Msangi amewatupia lawama wanawake kwa kutotimiza wajibu wao wa malezi ipasavyo, huku akiwataka kutenga muda wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao.

Amewataka wanawake kutotumia muda mwingi katika shughuli za uzalishaji, badala yake watenge muda wa kuzungumza na kufanya uchunguzi kwa watoto wao mara kwa mara, ili kubaini iwapo kuna viashiria vya kufanyiwa ukatili ikiwemo kuonyesha hofu na kutojiamini.

“Wanawake ndiyo tunaoweza kupunguza ukatili kwa asilimia kubwa sababu ndiyo walezi wa familia. Tunapotoka kwenye majukumu yetu ya uzalishaji tukifika nyumbani tutimize majukumu ya mama ‘mzazi’, tuzungumze na kuwaogesha watoto wetu, ili kujua maendeleo ya watoto wetu,” amesema Msangi.

Naye, Mkuu wa Dawati la Jinsia mkoa wa Mwanza, Faraja Mkinga amesema mbali na kuwafikisha mahakamani wazazi wanaowafanyia watoto wao ukatili, dawati hilo huwafikisha katika vituo vinavyohifadhi watoto waliofanyiwa ukatili kwa ajili ya kujengewa uelewa wa athari za ukatili kwa mtoto.

“Wakati mwingine si lazima tuwawajibishe wazazi kwa kuwafikisha mahakamani, tunawaleta hapa na kuwapatia elimu, kisha tunawakabidhi watoto wao. Baadaye tunafanya ufuatiliaji wa hali ya malezi kwa hao watoto waliowahi kuwafanyia ukatili,” amesema Faraja.

Sababu kuu

Awali, Mkuu wa Kituo cha Polisi Nyakato jijini Mwanza, Prisca Sarabanze ametaja kitendo cha wazazi kuishi chumba kimoja na watoto kuchangia uwepo wa matukio ya ulawiti na ubakaji kwa watoto, huku akiitaka jamii pamoja na changamoto ya umaskini, wazazi wajitahidi kulala chumba tofauti na watoto wao.

Pia ameonya tabia ya baadhi ya wazazi kuwalaza watoto wao chumba kimoja na ndugu na wageni wenye umri mkubwa, huku akidokeza kuwa ni miongoni mwa mambo yanayochangia idadi kubwa ya matukio hayo.

“Unakuta mama ni mfanyabiashara anaamka Saa 11 alfajiri kwenda kutafuta mboga soko la Buhongwa, anakwenda kuuza kishiriki hadi saa 4 usiku, akirudi amechoka na hawezi kujua maendeleo ya mtoto, ukimuuliza anasema anatafuta fedha, itamsaidia kweli?,” amehoji Sarabanze.

TPF Net mbali na kuwajulia hali watoto 25 waliofanyiwa ukatili waliopo katika kituo hicho sasahivi, imewakabidhi mahitaji ya msingi ikiwemo vyakula, sabuni, vinywaji na fedha taslimu kwa ajili ya kusaidia ustawi wao wanapoendelea na matibabu katika kituo hicho.