Wavuvi Mto Kilombero walia athari za mafuriko

Mvuvi katika Mto Kilombero Mzee Kipili akisafisha samaki kando ya mto huo Kwa ajili ya kuwauzia wateja wake. Picha Hamida Shariff

Muktasari:

  • Wavuvi wameiomba Serikali iwawezeshe mitaji kwa ajili ya kununua nyavu na mitumbwi kwa sababu waliyokuwa nayo imesombwa na maji

Morogoro. Wavuvi katika Mto Kilombero wameeleza athari walizozipata kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Akizungumza na Mwananchi Digital jana Ijumaa Mei 3, 2024, mwenyekiti wa kambi ya wavuvi katika Mto Kilombero, Amani Timoth ametaja athari hizo kuwa ni kupungua kwa  samaki wakubwa na wale adimu waliokuwa wakiwauza kwa bei ya faida kubwa.

"Mto huu ni maarufu kwa kutoa samaki aina ya kitoga na njege ambao hupendwa na watu wengi wakiwamo wageni wanaokuja Ifakara na wilayani Kilombero, lakini hivi sasa wamepungua kwa sababu ya mto kufurika maji," amesema Timoth.

Amesema mbali ya kupungua kwa samaki, hivi sasa mto huo una wanyama wakali kama mamba wanaotishia usalama wa wavuvi.

“Hivi tunavyozungumza hapa, ndani ya miezi miwili, vijana wawili wameliwa na mamba walipokuwa wakivua samaki,” amesema Timoth.

Mvuvi mwingine, Mzee Kipili amesema kutokana na kufurika kwa maji katika mto huo wanahofu kuendelea na kazi ya uvuvi.

"Uvuvi ndio kazi yetu inayotufanya tuendeshe maisha yetu ya kila siku, lakini sasa hivi maisha yetu magumu sana hatuna njia nyingine ya kuingiza kipato na mtoni hatuwezi kwenda mbali na mitumbwi tunaogopa kuliwa na mamba au isije kuzama kwa sababu maji ni mengi sana,” amesema Kipili.

Mvuvi Gerlad Mpapai ameiomba Serikali kuwawezesha mitaji kwa ajili ya kununua nyavu na mitumbwi kwa sababu waliyokuwa nayo imesombwa na maji wakati wa mafuriko.

"Mitumbwi na nyavu zetu za kuvulia samaki zote zimesombwa na mafuriko sasa hivi tunavua kwa shida na bado tunahofu kubwa kwa sababu bado mto umefurika,” amesema Mpapai.

Amesema tangu ameanza kazi ya kuvua samaki hajawahi kuona mafuriko makubwa kama yaliyotokea mwaka huu.