Watatu mbaroni wakituhumiwa kumtoa mimba mtoto

Njombe. Jeshi la Polisi mkoa wa Njombe linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na utoaji wa mimba ya mtoto mwenye umri wa miaka 16, mkazi wa kitongoji cha Singida kilichopo Tandala wilayani Makete Mkoa wa Njombe.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe, Mahamoud  Hassan Banga Hayo, amesema hayo leo Machi 15, 2024  alipozungumza na waandishi wa  habari.

Amesema awali mtoto huyo ambaye anafanya kazi katika mgahawa  huko wilayani Makete,  alidaiwa kuwa na uhusiano na kimapenzi wa bosi wake.

Banga amesema baada ya msichana huyo kupata mimba kukawa na mkakati wa kuitoa na alishirikishwa dada wa binti huyo.

Amesema kwa maelezo ya awali dada wa binti huyo alipatiwa Sh500,000 na kumshirikisha nesi wa hospitali ya Ikonda na  baada ya kupata taarifa hizo wote walikamatwa.

Kwa mujibu wa Banga, tukio hilo limetokea Novemba 10, 2023 na kuripotiwa Novemba 13, 2023 baada ya kuona hali ya binti hiyo inazidi kuwa mbaya baada ya kutoa mimba hiyo.

"Kuna binti aliyeonekana kutolewa ujauzito katika mazingira ambayo si mazuri na baada ya hapo ndugu zake walifika kituo cha polisi wakiwa na huyo binti likafunguliwa jarida na kuna watu watatu wamekamatwa kuhusika na tukio hilo" amesema Banga.

Amesema upelelezi wa shauri hilo umekamilika na wakati wowote watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.