Wataalamu watoa siri iliyopo kwenye vyakula vya asili

Muktasari:

  • Ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza wananchi wameshauriwa kutumia vyakula vya asili ili kulinda afya zao badala ya matumizi ya vyakula vya kisasa ikiwamo chipsi.

Mbeya. Ulaji wa vyakula vya asili imetajwa kuwa suluhisho la magonjwa yasiyoambukizwa na uzito uliopitiliza, huku elimu ikitakiwa kwa wananchi ili kulinda afya yao.

 Kutokana na hali hiyo, Shirika la Agrithamani limeandaa Tamasha la Misosi Asili ikilenga kuhamasisha matumizi ya vyakula vya asili ili kulinda afya na lishe kwa wananchi.

Program ya msosi asilia inasimamiwa na mradi wa Agri-Connect, ambao unatekelezwa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Kimataifa na kufadhiriwa na Umoja wa Ulaya.

Amesema lazima wananchi waache mazoea ya ulaji vyakula vya kisasa badala yake watumie vyakula asili ili kuondokana na magonjwa yasiyoambukizwa kama figo, shinikizo la damu, kisukali, presha na moyo.

“Hili zoezi litakuwa endelevu, kwa kipindi cha nyuma tulilenga zaidi watoto juu ya utapiamlo lakini kwa sasa tumeona kuwafikia wananchi wote ili kuhamasisha afya iliyo imara,” amesema.

“Kumekuwapo mfumuko wa magonjwa mengi ndio maana tumeamua kuja na program hii na mamalishe wanapaswa kubadili mapishi yao kuja kiasili,” amesema Joyce.

Mratibu wa wadau Agrithamani Foundation, Famba Godwin amesema lengo la tamasha hilo ni kuhamasisha matumizi ya vyakula vya asili ili kulinda afya kuepukana na udumavu na magonjwa.

“Kumekuwapo na ulaji usiozingatia muongozo wa kitaalamu, hivyo tunaamini kupitia tamasha hili wananchi watapata elimu ya lishe hivyo mama na baba lishe watabadilika katika mapishi,” amesema Godwin.

Mama lishe, Janeth Mwafwaga amesema licha ya wananchi wengi kuzoea vyakula vya kisasa, lakini lazima wataendelea kuwashauri kutumia vyakula asili.

“Vyakula vya asili vina faida kubwa kwa sababu mapishi yake hayana kemikali wala mafuta kama ilivyo vyakula vya kisasa, tutawahamasisha wateja wetu ili wabadili mfumo wao,” amesema Janeth.

Mkazi wa Airport jijini humo, Victor Mbwaga amesema kizazi cha sasa kimeharibika na matumizi ya vyakula vya kisasa akiomba kuwapo elimu nchi nzima kuepukana na vyakula visivyo na faida mwilini.

“Kwanza tunashukuru kwa elimu hii lakini kutokana na ukubwa wa tatizo la ulaji vyakula kisasa kuwapo mwendelezo na isambae nchi nzima ili kunusuru afya za Watanzania,” amesema Mbwaga.