Warombo wataka kuanzisha benki yao

Wananchi wa Rombo wanaoishi Dar es Salaam wakiwa katika mkutano wa kujadili masuala mbalimbali ya wilaya yao, kwenye Viwanja vya Msimbazi Center jijini humo. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Kwa ufupi: Wananchi wa Rombo wanaoishi Dar es Salaam wametakiwa kuungana kuanzisha benki yao ambayo itawasaidia kuongeza nguvu ya kukuza uchumi.

Dar es Salaam. Wenyeji wa Rombo wanaoishi Mkoa wa Dar es Salaam wamehamasishana kushirikiana kuanzisha benki yao itakayowasaidia kukuza uchumi wa pamoja.

Wamesema endapo wazo hilo litafanikiwa, benki hiyo itawapa fursa ya kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo nchini, hivyo kukuza uchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na kuleta maendeleo mapana kwa Taifa.


Wananchi wa Rombo wanaoishi Dar es Salaam wakiwa katika mkutano wa kujadili masuala mbalimbali ya wilaya yao, kwenye Viwanja vya Msimbazi Center jijini humo. Picha na Janeth Joseph


Waliweka nia hiyo walipokutana wakiwa na madiwani wa kata zote 28,  mbunge na viongozi wengine katika Ukumbi wa Msimbazi Center, uliopo jijini hapa kujadili maendeleo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Wamsema yote yanawezekana kwa kuwa wananchi wanaotoka katika wilaya hiyo ni wachakarikaji na ni watu ambao wanajua kutumia fursa vizuri.

Akizungumzia suala la uanzishwaji wa benki hiyo, mmoja wa wananchi hao, Felician Mtenga amesema Warombo wengi wamekuwa wakijishughulisha na shughuli mbalimbali za kibiashara na kwamba benki hiyo itatoa fursa ya kuanzishwa kwa viwanda ambavyo vitasaidia kukuza uchumi na kuleta maendeleo makubwa ya kiuchumi.

"Tunamshukuru Mungu tumekutana hapa leo, hili ni jambo la kipekee sana ambalo linatupa fursa sisi Warombo, tujadili uchumi wetu wa pamoja na fursa zilizopo, leo tungekuwa na benki tungekuwa na msemaji wetu mkuu wa benki, ambaye angesimama hapa na kutuambia tumechukua mkopo wa bilioni kadhaa benki kuu,  kwa ajili ya kuendeshea shughuli zetu," amesema.

"Hii itasaidia wale wenye mitaji mikubwa waweze kuanzisha viwanda kwa kuchukua mikopo benki. Sisi Warombo tunao uwezo mkubwa na wakufanya mambo makubwa, hivyo tukianzisha benki yetu tutapiga hatua kubwa zaidi ya kimaendeleo," amesema.

Adelaide John, mmoja wa wananchi hao, amesema wanapokuwa na benki yao wenyewe, inakuwa njia rahisi ya kupata mikopo kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao za kibiashara.

"Tunapokuwa na benki yetu wenyewe inakuwa ni njia rahisi kupata ya fedha. Kote duniani unapotakiwa kufanikiwa ni lazima muwe na benki yenu ndio mnaweza kupata mitaji mikubwa na hii itatoa fursa kwa watu kujiingiza kwenye shughuli za kujenga viwanda, pamoja mambo mengine,"

"Sisi tuna watu wengi ambao wanaweza kufanya hivyo na kuchakarika, uwezo huo tunao wa kuanzisha benki ya Warombo, Warombo wanazo fedha, ni namna tu ya kuungana pamoja ili fedha ziweze kutumika kwa kukopesha na kutoa mitaji kwa ajili ya uzalishaji," amesema.

Kwa upande wake Pantaleo Shirima amewataka Worombo kuendelea kutunza umoja wao ili wanapoamua kufanya jambo liweze kufanyika kwa ukubwa na kwa ubora na liweze kuleta tija kwa manufaa ya wengi.

"Tutunze tamaduni zetu, tumshukuru sana Mbunge kwa kutukutanisha, hili jambo tulilitafuta kwa muda mrefu sana, kwa haya anayoyafanya ya kutuweka pamoja kama leo, hakika hili ni jambo kubwa, namwona Mramba yupo hai kwa kupitia Mkenda kwa kufuata nyayo zake,"

Akizungumza na wananchi hao, Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imeendelea kufanya mambo makubwa katika wilaya hiyo na kwamba watapambana kupanua fursa za kiuchumi zilizopo wilayani humo  ili wananchi waweze kunufaika na rasilimali zilizopo.

"Tunataka tupate mageti ya kupandia mlima Kilimanjaro zaidi ya Nalemoru ambalo tunalo, tupate jingine moja lipite pale Mkuu au Mashati ili kufungua fursa za kiuchumi, tukianza hivi tutachochea maendeleo ya kiuchumi katika wilaya yetu.

"Rombo tunayo mambo mazuri ambayo yanaweza kututambulisha katika shughuli zetu, kwa kuwa Warombo ni wachapakazi na tunatazamia hivi karibuni tufungue jukwaa la ndizi kwa maendeleo mapana ya wilaya yetu," amesema profesa Mkenda ambaye ni Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia.

Mkuu wa Wilaya hiyo, Raymond Mwangwala yeye amewataka wafanyabiashara waliopo Dar es Salaam kuchangamkia fursa zilizopo wilayani humo na kwamba Serikali imetoa zaidi ya Sh15 bilioni kwa ajili ya maboresho mbalimbali ya miundombinu.

"Wilaya ya Rombo wananchi wake wanashughulika na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha biashara, chakula na matunda, hivyo tunawakaribisha wawekezaji kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya juisi ili kuongeza thamani ya mazao haya na mengine," alisema.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Saashisha Mafuwe, mbunge wa Hai, ambaye amempongeza Profesa Mkenda kwa kuwakutanisha Warombo wanaoishi Mkoa wa Dar es Salaam akisema ni hatua kubwa ya maendeleo inayopaswa kuigwa na wengine.

"Mshikeni aendeleze ahitimishe kazi hii, siasa ni maendeleo, leo mmeweza kukutana hapa na kujadili mambo mbalimbali yanayohusu Rombo, ni kwa sababu mmepata mbunge mzuri, tumshike mkono twende naye ili aweze kufanya kazi hiyo nzuri," amesema.