Wanawake, vijana hatarini kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza

Muktasari:

  • Profesa Mohamed Janabi asisitiza umuhimu wa kufunga ili kuupa mwili nafasi ya kufanya kazi na kuimarisha afya.

Dar es Salaam. Watu saba kati ya 100 wanafuata ulaji unaofaa, jambo linaloonyesha wengi hawazingatii hilo, hivyo kujiweka katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza (NCD).

Hayo yamebainishwa leo Aprili 17, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa kampuni mbalimbali ulioandaliwa na UN Global Compact kwa lengo la kuhamasisha afya bora sehemu za kazi, hasa kwa kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu amesema mkutano huo unatoa matumaini kwamba angalau kuna kundi jingine linaunga mkono juhudi za kuimarisha afya za wananchi.

Amesema katika suala la kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, kuna maeneo ambayo Watanzania wanafanya vizuri na mengine hawafanyi, huku vijana wakiwa hatarini zaidi kuathirika na magonjwa hayo.

"Kwenye suala la kufanya mazoezi tunafanya vizuri, ndiyo maana utasikia kuna mbio za marathoni kila sehemu. Kwenye suala la ulaji bado hatufanyi vizuri, takwimu zinaonyesha watu saba kati ya 100 ndiyo wanafuata ulaji unaofaa, maana yake hatuzingatii ulaji unaofaa.”

"Suala la uzito kupita kiasi linazidi, zamani ilikuwa ni mtu mmoja kati ya wanne ndio ana uzito uliopitiliza, sasa ni mtu mmoja kati ya watu watatu ana uzito uliokithiri," amesema.

Amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri zaidi wasomaji, wafanyakazi na watu walio katika umri mdogo.

Ameeleza Serikali ina mzigo mkubwa katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo na wanashirikiana na wadau kutoa elimu kuhusu mitindo bora ya maisha.

"Kama jamii tunapaswa kuhakikisha tunafanya vizuri. Kwa bahati mbaya vijana wanaathirika zaidi kuliko rika jingine lolote, na wanawake wanaathirika kuliko wanaume katika sehemu nyingi tu kama hizi," amesema Dk Ubuguyu.

Mkurugenzi Mtendaji, UN Global Compact, Marsha Marcatta-Yambi amesema wanazisaidia kampuni binafsi, asasi za kiraia na Serikali katika uendelevu ili kuendana na nguzo nne za Global Compact ambazo ni haki za binadamu, mazingira, kazi na vita dhidi ya rushwa.

Kwa kufanya hivyo amesema wanatekeleza Agenda ya 2030 ambayo kwa Afrika ni chapta itakayofanya mwendelezo wa ajenda hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzzane Ndomba-Doran amesema kongamano hilo ni muhimu kwa kuwa wafanyakazi wengi katika kampuni wako hatarini kupata magonjwa yasiyoambukiza, hivyo wanahitaji kupewa hamasa na mbinu za afya bora.

"Magonjwa haya yanatokana na mitindo ya maisha, mbali na yale ya mgongo kuuma, kuna haya mengine yasiyoambukiza, mfanyakazi hafanyi mazoezi, kwa hiyo ni muhimu kuwa na makongamano kama haya ili kujenga afya za waajiriwa sehemu za kazi," amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi amesisitiza umuhimu wa kufunga akisema unaupa mwili nafasi ya kufanya kazi na kuimarisha afya.

"Nashauri muwe mnaacha kula baadhi ya milo hasa mlo wa asubuhi, hii itasaidia viungo vya mwili kama insulini kufanya kazi yake kwa ufanisi zaidi. Huwezi kupata madhara kwa kufanya hivyo," amesema Profesa Janabi.