Walinzi wawili wauawa na watu wasiojulikana

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kata ya Misuna, Shabani Omary akionyesha eneo ambalo ulikutwa mwili wa mlinzi Elvis Muna katika mtaa wa Dk Salmin Amour mkoani Singida Picha na Jamaldini Abuu

Muktasari:

  • Ni matukio ya mlinzi katika kiwanda kidogo cha kuchakata chupa za plastiki aliuawa kisha wauaji hao kuiba simu tano za miamala ya simu katika duka la jirani, pamoja na mlinzi wa nyumba ya kulala wageni na baa

Singida. Walinzi wawili katika maeneo tofauti wameuawa na kukutwa wametupwa katika maeneo yao ya lindo.

Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Singida, alipotafutwa na Mwananchi Digital azungumzie matukio hayo leo Jumanne Aprili 23, 2024, Pipi Kayumba amesema atatoa taarifa kamili kesho.

Mwananchi imeelezwa kuwa matukio yote mawili yametokea usiku wa kuamkia Aprili 19, 2024 katika Mtaa wa Ng'ongo Ajipu, Kata ya Majengo na Mtaa wa Dk Salmin, Kata ya Misuna Manispaa ya Singida mkoani Singida.

Katika tukio la kwanza mlinzi wa kampuni ya Imara Security ambaye hajafahamika jina lake mara moja, imeelezwa alikuwa akilinda baa na nyumba ya kulala wageni mali za Super Kitasa Anex.

Mmoja wa mashuhuda aliyejitambulisha kwa jina la Pendo James, ambaye ni muhudumu wa Baa ya Super Kitasa Anex, amesema usiku wa tukio alikuwa amelala kwenye nyumba hiyo ya wageni lakini hakusikia chochote usiku mzima.

Na anasema ilipofika asubuhi aliamshwa na mtu anayefanya usafi akimwambia kamkuta mlinzi amelazwa kwenye kiti akiwa  amefunikwa shuka la kimasai na anatokwa damu nyingi.

"Sisi tulifunga biashara kama saa sita hivi usiku tukamkabidhi mlinzi silaha zake tukajifungia ndani tukalala, asubuhi aliniita mtu wa usafi, nilipotoka nikamkuta amelazwa kwenye kiti amefunikwa na shuka hapo chini kuna damu nyingi,” amesema Pendo.

Amesema alimpigia simu mmiliki wa eneo hilo ambaye alifika mara moja akaondoka na baadaye akarejea akiwa na Polisi.

Akisimulia mkasa huo, mmiliki wa eneo hilo  Lidas Ngowi amekiri kupigiwa simu na muhudumu wake akimjulisha juu ya mauaji hayo.

Amesema alitoa taarifa polisi ambao walifika na kuuchukua mwili wa mlinzi huyo na kuupeleka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kwa uchunguzi zaidi.


Hata hivyo, amesema mlinzi huyo ni mgeni katika eneo hilo. "Huyu mlinzi alikuwa mpya hata jina simfahamu, ndio alikuja siku ya kwanza, wamevunja kitasa cha mlango lakini hawajaondoka na chochote,” amesema.

Katika tukio lingine siku hiyohiyo lililotokea Mtaa wa Dk Salmin, Kata ya Misuna, mlinzi wa kiwanda kidogo cha kuchakata chupa za plastiki, Elvis Muna naye amekutwa ameuawa na kutupwa pembeni kidogo ya eneo la lindo lake.

Imeelezwa wauaji wameiba simu tano zinazotumika kufanyia miamala katika duka la jirani na kiwanda hicho.

Mmiliki wa Kiwanda hicho, Fidelis Kileo amesema alipigiwa simu na msichana wake wa kazi aliyemtaarifu juu ya mauaji hayo naye akatoa taarifa polisi.

Kileo amesema mzee huyo wameishi naye kwa muda mrefu bila kutokea tukio lolote la wizi na kifo chake kimemuhuzunisha.

Hata hivyo, amesema kiwandani kwake hakujaibiwa kitu; “Lakini dukani kwa jirani yangu ndiyo wameiba simu tano zinazotumika kufanyia miamala ya simu.”

“Ni mtu tuliyekaa naye kwa muda mrefu sana,  hatujawahi kupata madhara yoyote ya wizi, nilipata taarifa asubuhi nikaja nikakuta kweli mzee amelala chini amekatwakatwa mapanga, na duka la jirani lilivunjwa,” amesema mmiliki huyo.

Naye jirani wa eneo hilo, Francis Gondwe amesema waliamshwa asubuhi na kupewa taarifa za mauaji hayo.

“Tuliamshwa asubuhi kabisa tukaambiwa kuna tukio, tukaja ndiyo tukakuta babu yetu ameuawa,  tunaomba Serikali iimarishe ulinzi katika eneo hili, haiwezekani walinzi wawili wakauawa kwa usiku mmoja,” amesema Gondwe.

Aidha kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Misuna, Shabani Omary amesema baada ya kupata taarifa hizo waliwasiliana na uongozi wa wilaya ambao ulitoa maagizo ya kuimarishwa kwa ulinzi katika eneo hilo.

 “leo hii tumekaa na uongozi wa wilaya, tulikuwa na katibu tarafa kwa niaba ya mkuu wa wilaya akatupatia utaratibu wa namna ya kuanzisha ulinzi shirikishi,” amesema kiongozi huyo.