Wajitosa kufanya utafiti wa mikopo ya halmashauri

Mkuu wa shule ya Biashara na Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT), Profesa Agnes Mwakaje akifungua warsha juu ya Utafiti unaofanywa na chuo hicho ili kubaini namna bora ya kuwawezesha kiuchumi, Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kinafanya utafiti ili kuja na mapendekezo ya namna bora mikopo ya asilimia 10 itakavyokuwa na matokeo chanya juu ya changamoto za ajira na  uchumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Musoma. Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Sua) pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kinafanya utafiti kubaini sababu za kuendelea kuwepo kwa changamoto za kiuchumi na ajira kwa makundi maalum licha ya kuwepo kwa fursa ya mikopo ya asilimia 10.

Utafiti huo unaofanywa kwa miaka mitatu ulianza Septemba 2021,mbali na kubaini changamoto lakini pia utakuja na mapendekezo ya namna bora ya kuwezesha makundi hayo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Akizungumza kwenye warsha ya maofisa maendeleo ya jamii kutoka mikoa ya Mara na Arusha mjini Musoma Oktoba 11, 2023; Mratibu wa utafiti huo, Dk Joel Joshua amesema wameamua kufanya utafiti huo ili kuja na suluhisho la kudumu mapema juu ya changamoto hizo zinazokabili makundi hayo.

"Tunataka kujua kama shida ipo kwenye sera, sheria au mitaala kwasababu tumebaini kuwa pamoja na Serikali kuweka mazingira ya uwezeshaji wa makundi haya ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu bado hakuna matokeo chanya na badala yake makundi haya yanakabiliwa na changanoyo za ajira na uchumi kwa ujumla,"amesema

Amesema tayari wamekusanya taarifa za awali ikiwemo takwimu baada ya kuyafikia makundi hayo katika mikoa ya Mara na Arusha na kwamba hivi sasa wanaendelea na ukusanyaji  wa taarifa kutoka kwa watendaji wa Serikali kabla ya kuanza kufanya uchambuzi wa takwimu na kuziweka kwa pamoja.

Akifungua warsha hiyo, Mkuu wa Shule ya Biashara na Uchumi MJNUAT, Profesa Agnes Mwakaje amesema utafiti huo unalenga kupatikana kwa njia bora zaidi ili kuwezesha makundi hayo kujitegemea kiuchumi tofauti na ilivyo sasa.

"Serikali inatambua umuhimu wa makundi haya ndio maana ikaja na huu utaratibu wa mikopo isiyokuwa na riba kupitia halmashauri  lakini kwasababu tunaona hakuna matokeo chanya tumeamua tuingilie kati ili tushauri nini kifanyike ili kuwa na mafanikio,"

"Utafiti huu ni wa muhimu ili kubadilisha mfumo wa asilimia 10 uweze kuwa na tija na kuyafikia malengo ya Serikali kutokanana na umuhimu wa makundi haya katika jamii naamini baada ya utafiti mwanga utaonekana," amesema Profesa

Amesema makundi hayo ni miongoni mwa makundi yanayokabiliwa na athari ya ukosefu wa ajira hivyo utafiti huo utakuwa suluhisho la kudumu juu ya changanoto hiyo hali ambayo pia itakuwa na matokeo chanya kwenye uchumi wa jamii na nchi kwa ujumla.

Ofisa Maendeleo ya Jamii kutoka jiji la Arusha, Manyama Shaban amesema miongoni mwa changamoto zinazokabili mikopo hiyo ni pamoja na urejeshaji duni hasa kwa kundi la vijana.

"Kwa asilimia kubwa vijana hawarejeshi mikopo angalau akinamama wanajaribu kidogo lakini hii inasababishwa na mambo mengi hivyo utafiti huu ukikamilika na mapendekezo yakafanyiwa kazi naamini huu mpango utakuwa na tija kubwa sana katika jamii,"amesema