Wahandisi nchi watakiwa kuungana, kupewa miradi mikubwa

Muktasari:

  • Kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa mwaka ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandishi (ERB) unaofanyika kwa siku tatu na kuhudhuriwa na zaidi ya wahandisi 3500 nchi nzima

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa amewataka wahandisi nchini kuungana ili wapewe miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali.

Akizungumza leo  Ijumaa Septemba 7, 2018 jijini Dar es Salaam wakati akifunga mkutano wa mwaka wa wahandisi, Kwandikwa pia amewataka wahandisi hao kufanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi ili kutekeleza miradi kwa ubora unaotakiwa.

Katika mkutano huo ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) naibu waziri huyo amesema uhandisi ni taaluma muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

“Shughuli ya uhandisi ni skeleton ya nchi, ni muhimu kwa uchumi wa nchi. Bodi inajitahidi kusimamia maadili ya wahandisi, wapo wahandisi ambao wamesimamishwa kazi kwa kukiuka maadili ya kazi yao,” amesema Kwandikwa.

Kuhusu kuwawezesha wazawa, Kwandikwa amesema wameanza mchakato wa kuwawekea utaratibu wa kisheria wahandisi kutoka nje ya nchi.

Amesema katika utaratibu huo, wahandisi hao watatakiwa kushirikiana na wahandisi wazawa katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Kaimu msajili wa ERB, mhandisi Patrick Barozi amesema kifungu cha 13 na 14 cha sheria ya bodi hiyo kitafanyiwa marekebisho ili kuwalazimisha wahandisi wa nje kushirikiana na wazawa kwenye miradi ya Serikali.

Amebainisha kuwa pia wanafanya utaratibu wa kuanzisha mfuko wa maendeleo ya ERB utakaotambuliwa kisheria na fedha zitakazopatikana zitatumika kwenye ujenzi wa jengo la makao makuu ya bodi hiyo mjini Dodoma kwa gharama ya Sh13 bilioni.

“Baada ya mkutano huu tutaandika mapendekezo yetu na kuyawasilisha serikalini kupitia Wizara ya Ujenzi ili yafanyiwe kazi. Baadhi ya mambo yaliyopendekezwa na wahandisi ni pamoja na kutengenezewa mazingira ya kushiriki kwenye miradi mikubwa,” amesema Kwandikwa.