Wahamiaji haramu wengine 16 wakamatwa Mufindi, gari yenye namba za Serikali yatumika

Wahamiaji haramu 16, raia wa Ethiopia waliokamatwa wakiwa wametelekezwa kwenye mashamba la mahindi baada ya  kushushwa katika gari walilokuwa wamepakiwa. Picha na Mary Sanyiwa, Mufindi

Muktasari:

  • Dereva atelekeza gari baada ya kuona askari anawafuatilia, awashusha wahamiaji hao msituni.

Iringa. Jeshi la Polisi mkoani Iringa  limewakamata  wahamiaji haramu 16, raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila  kibali.

 Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Mafinga leo Aprili 8,2024 Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Allan Bukumbi amesema Jeshi hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Uhamiaji  mkoani humo, wamefanikiwa kuwakamata wahamiaji hao katika eneo la msitu wa Luganga, kata ya Sao Hill Tarafa ya Ifwagi wilayani Mufindi.

Amesema wahamiaji hao waliwakamata wakiwa  wametelekezwa katika  shamba la mahindi  baada ya kushushwa kwenye gari ambalo awali lilikuwa likisomeka namba za usajili STL 3999 Landcruiser V8 yenye rangi nyeupe.

“Baada ya amelitelekeza gari hilo baada ya kuna anafuatiliwa na askari, akaona hataweza kupitia barabara kuu, hivyo alipita njia nyingine na kufika sehemu ambapo alikutana na tikiti ( swap), alisindwa kuendelea na safari hiyo, ndipo alifikia hatua ya kuwashusha  wahamiaji hao  na kutokomea kusikijulikana," amesema RPC Bukumbi

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa , Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa  Polisi (SACP), Allan Bukumbi akizungumza na waandishi wa habari Mjini Mafinga, baada ya kuwamata wahamiaji hao haramu. Picha na Mary Sanyiwa, Mufindi

Amesema uchunguzi  wa awali umebaini gari hiyo imesajiliwa kwa namba T803 CVW inayomilikiwa na Saidi Hassan, mkazi wa Tabata, Dar es Salaam huku akieleza  jitihada zinaendelea kumtafuta dereva huyo na mmiliki wa gari hilo.


 Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji (ACI), Peter Kimario na Ofisa Uhamiaji Mkoa wa Iringa, amesema biashara  hiyo haramu ya binadamu ni mbaya, kwani inahatarisha  usalama wa Taifa.

"Kupitia vyombo vya habari, nitoe wito  kwa wananachi watusaidie katika kampeni yetu ambayo imeanzishwa  nchini mzima inayoitwa ‘Mjue jirani yako’ kwa sababu hawa tumewakamtwa kwenye magari ya aina hiyo.

“Hivyo tunaamini wanaweza kutumia mbinu za kuvaa vizuri kama wa Tanzania na kusafiri katika vyombo vya usafiri vya kawaida bila kuwajua," amesema ACI Kimario

Kimario  amefafanua kuwa  kampeni hiyo  imeanzishwa ili kujua vitu vinavyoendelea katika maisha ya wananchi kwa sababu usalama wa nchi kila mtu anahusika.

Hata hivyo, amesema jeshi hilo la uhamiaji litaendelea kushirikiana na vyombo vingine, ili kuhakikisha wahamiaji hao wanafikishwa kwenye vyombo husika na kuchukuliwa hatua.