Wafungwa 95 waachiwa huru Gereza la Ludewa

Muktasari:

Katika maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 1,631 huku wanufaika 95 wa msamaha huo wakitokea Gereza la Wilaya ya Ludewa.


  


Ludewa. Katika maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan ametoa msamaha kwa wafungwa 1,631 huku wanufaika 95 wa msamaha huo wakitokea Gereza la Wilaya ya Ludewa.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Desemba 14, 2022 Mkuu wa Gereza hilo, Johanes Baitange amesema kati ya wafungwa 95 waliopata msamaha 65 ni raia wa kigeni.

“ Hawa 95 waliopata msamaha wa Rais kati yao 63 ni raia wa Ethiopia na wawili ni raia wa Malawi,” amesema Baitange

Amesema wafungwa hao 65 wameachiwa huru kutoka Desemba 11, 2022 ila wataendelea kubaki gerezani kusubiri taratibu za kuwaachia kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani.


“Hao wameachiwa huru tarehe 11/12/2022 kwa kuwa makosa yao ni ya kuingia kwa jinai wataendelea kukaa gerezani wakiwa wamezuiwa mpaka hapo taratibu nyingine za kuwatoa gerezani zitakapokamilika kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,” amesema Baitange.


Ameongeza kuwa wafungwa 30 kati ya 95 waliopata msamaha walikuwa hawajafikisha robo ya adhabu yao hivyo wataendelea kutumikia mpaka itakapokamilika ndipo wataachiwa huru.


 “Kwenye orodha ya wafungwa hao 30 wafungwa 15 ni raia wa Kitanzania ambao walikamatwa kwa makosa tofauti tofauti na 15 ni raia wa kigeni kutoka Ethiopia,” amesema Baitange.


Amesema waliopata msamaha ni wale ambao hawajawahi kunufaika na msamaha wa Rais na kuna vigezo vinavyoangaliwa kwa wanaostahili kupata msamaha huo.



“Sifa zilizotakiwa kwa ajili ya msamaha huo ni wafungwa wasiwe wanarudia makosa mbalimbali ya kurudi gerezani, pia wasiwe wafungwa waliotuhumiwa kwa kumiliki silaha au kujihusisha na ujangili hizi ni baadhi ya sifa,” amesema Baitange.