Wafanyabiashara waliokwama Somanga wasimulia adha kukatika kwa barabara

Muktasari:

  •  Kauli ya Mwenyekiti wa wafanyabiashara Taifa aliyoitoa kwa njia ya sauti kupitia mitandao mbalimbali imewaibua wafanyabiashara waliokwama Somanga baada ya daraja kusombwa na maji.

Lindi/Mtwara.Wafanyabiashara wa Kusini wanaotumia barabara kuu inayokwenda mikoa ya Pwani na Dar es Salaam wamezungumzia adha wanayoipata kutokana na kukatika kwa barabara hiyo muhimu kwa uchumi wa watu wa kusini na Taifa kwa ujumla.

Maoni ya wafanyabiashara hao yanafuata baada ya Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Taifa, Hamis Livembe kutoa tahadhari kwa wafanyabiashara kutokana na miundombinu ya barabara kusombwa na maji, baadhi ya wafanyabiashara waliokwama njiani wameeleza hali ilivyo.

Katika taarifa yake, mwenyekiti huyo amesema hali ni mbaya, mvua zinazoendelea kunyesha katika wilaya za Rufiji na Kilwa, hivyo amewataka wafanyabiashara kusitisha safari zao katika kipindi hiki.

“Madaraja yamesombwa na maji, wafanyabiashara wamekwama na wengine wako kisiwani kutokana na madaraja kukatika na maeneo mengine kujaa maji, sio jambo jema kusafiri kwa kuwa kuna kipande kirefu kimefunikwa maji ambapo hatujui kama chini kuko salama, hata gari zenyewe hazikutani zaidi ya kilomita 150 maji yamejaa,” amesema.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu kutokea Somanga, leo Mei 5, 2024, mfanyabiashara Salehe Sunday aliyekuwa akirejea Lindi kabla ya kukwama kutokana na miundombinu ya barabara kusombwa na maji kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika mkoa wa Lindi.

Amesema kuharibika kwa barabara hiyo kuna athari kubwa kwao kwa sababu zipo bidhaa ambazo zinaharibika haraka, lakini pia usalama wao huko barabarani ni wa mashaka  kwa kuwa baadhi ya vitu vinaibiwa.

“Mimi nipo Somanga, tunaathirika hasa kwa mizigo ambayo tulitarajia leo kufika kwa mfano mzigo kama wa maji yakipasuka yanaweza kulowesha maboksi, kuna bidhaa nyingine kama nyanya zinaharibika.

“Usalama wetu sio mzuri, magari yenyewe tumekodi, hata wateja ambao walitarajia leo kupata mzigo haiwezekani kutokana na hali ya barabara, usalama wa mali unakuwa mdogo kwa sababu magari ni mengi, kwa hiyo ni tatizo kubwa kwetu wafanyabiashara,” amesema Salehe.

Zahoro Mkandenje, mfanyabiashara wa vifaa vya kielektroniki mkoani Lindi, amesema kukatika kwa barabara hiyo ni mtihani kutokana na mizigo ya wateja walioagiza kutoka Dar es Salaam kukwama njiani.

“Barabara ikijifunga hata kwa siku moja ni shida kubwa, sasa kwa hili sijui lini itafunguka. Mfano, nilikuwa na oda ya mizigo ambayo nilitakiwa niwakabidhi leo wateja wangu na hawajanilipa, nilikuwa nasubiria ifike ndiyo wanilipe na kesho walikuwa wanatakiwa waitumie. Kwa hiyo, kujifunga kwa barabara kumeathiri biashara zangu,” amesema Mkandaje.

Amesema, “Wapo wateja hawaelewi, wanasubiri lakini mwingine hawezi kusubiri, wapo walioniagiza nyaya kwa ajili ya spika ambazo wanatakiwa wazitumie kesho na nimeshazinunua lakini haziwezi kufika kwa wakati na mimi nitakuwa nimeshapata hasara,” amesema.

Kwa upande wake, Shabani Kikotekeki, mfanyabiashara na fundi simu mjini Lindi ameiomba Serikali  ilishughulikie tatizo hilo haraka ili barabara iweze kupitika.

“Biashara nyingi za mikoa ya Lindi na Mtwara zinategemea barabara hivyo kujifunga ni tatizo kubwa na litazorotesha uchumi wa watu wa kusini” amesema Kikotekeki