Wachimbaji wadogo Geita kunufaika na tafiti za kijiolojia

Mtambo wa kuchoronga miamba ya madini ukiendelea na kazi ya uchorongaji kwenye mgodi wa Kadeo uliopo kata ya Rwamgasa Wilaya ya Geita.Mtambo huo ni miongoni mwa mitambo 5 iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 2023 jijini Dodoma ikiwa na lengo la kumuwezesha mchimbaji mdogo kuchimba kwa uhakika na kupata taarifa sahihi zitakazomuwezesha kuaminiwa na taasisi za kifedha. Picha na Rehema Matowo

Muktasari:

  • Taarifa za GST zinaeleza kuwa tafiti za awali za uchunguzi wa miamba na madini zimefanyika kwa asilimia 16 pekee hapa nchini  na Oktoba 5,2023 Waziri  wa Madini, Antony Mavunde alikaririwa akisema  Serikali imelenga kuongeza akiba ya taarifa hizo kutoka asilimia 16 iliyopo sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Geita. Serikali imesema kuwa uchimbaji madini nchini hautakuwa na tija kama wachimbaji wadogo hawatakuwa na taarifa za tafiti za awali za kijiolojia kwenye maeneo yao.

Kutokana na hilo, Shirika la Madini imeunda kamati  itakayokutana na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), kuboresha mkataba uliopo baina yao ili waweze kufanya tafiti za awali zitakazowezesha mitambo hiyo kufanya kazi kwenye maeneo yenye uhakika na kuleta tija zaidi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mtambo wa kuchoronga madini kwa Mkoa wa Geita ulioanza kufanya kazi kwenye mgodi wa Kadeo, Mkurugenzi Mtendaji wa Stamico, Venance Mwasse amesema bado zipo changamoto za tafiti za awali,  “hili ni suala la kitaalamu tukilikwepa, aidha mashine hazitafanya kazi au zikifanya zitaleta hasara zaidi kwa sababu hazitafanya sehemu ya uhakika.

“Tayari tumeanza kuyafanyia kazi makubaliano  tulionayo na GST ambayo ndio wenye jukumu, kamati ilituelekeza twende tukaiboreshe na tayari imeundwa timu ya kufanya hivyo,  kwa kuwa wakati tunasaini makubaliano, mitambo haikuwepo. Sasa mitambo ipo, imekuja kutufumbua macho na tunawahakikishia wachimbaji hatutawaacha nyuma,” amesema Mwasse.

Akizungumzia umuhimu wa mitambo ya kuchoronga miamba, Dk Mwasse amesema awali wachimbaji wadogo walikua wakichimba kwa kubahatisha kutokana na kukosa taarifa sahihi, hivyo baadhi walipoteza mitaji lakini pia kutoaminiwa na taasisi za kifedha na kutokopesheka.

Amesema Serikali kupitia Stamico wamelenga kufanya mageuzi kwenye sekta ya uchimbaji mdogo nchini kwa kuwawezesha kuchimba kwa uhakika na kuacha kuamini imani potofu za ushirikina.

Wakizungumza kwenye uzinduzi huo, baadhi ya wachimbaji wadogo wamesema ujio wa mitambo wa kuchoronga madini unaongeza tija na watakua na uhakika wa madini wanayoyatafuta.

Fortunatus Luhemeja amesema mara nyingi wachimbaji wadogo wamekuwa wakitaka kujua kama madini wanayoyatafuta yapo, kwa ukubwa gani, kina gani na yatachimbwa kwa muda gani na kuwa kupatikana kwa mtambo huo ni suluhisho la changamoto zao.

 “Tukishakuwa na taarifa za miamba na wingi wa madini tuliyonayo, tunaweza kufanya shughuli zetu kwa tija na kupata kipato cha uhakika.”

Christopher Kadeo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Mkoa wa Geita (Gerema), ameishukuru Serikali kwa kusikiliza kilio chao na kusema mitambo hiyo itawaondoa kwenye uchimbaji wa kubahatisha ambao umekuwa ukiwapa hasara kila mara, na kuanza kuchimba kisasa na kwa tija zaidi.

Mtambo huo ni miongoni mwa mitambo mitano iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 2023 na mitambo mingine 10 inatarajiwa kuingia nchini Aprili na Juni, mwaka huu.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo Mjumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Idd Kassim amesema ili kubadili madini kuwa utajiri ni vema GST wakafanya tafiti kwa wachimbaji wadogo kwa gharama nafuu.

“Nasisitiza ni vema ikawekwa bei elekezi itakayomuwezesha mchimbaji mdogo kumudu, kwa sasa wachimbaji nikiwemo mimi sina taarifa za awali za miamba.”

“Wachimbaji wanatamani kutumia mtambo huu lakini hawana taarifa za utafiti wa awali,” amesema Idd.

Akizindua mtambo huo kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Cornel Magembe amesema kupatikana kwa mitambo ya kuchoronga miamba kutamaliza matukio ya ajabu yaliyokuwa yakitokana na shughuli za uchimbaji unaotegemea imani za kishirikina.

“Mashine hizi zitakuhakikishia kwenye eneo unalochimba kuna kiasi gani cha madini, umbali na mwelekeo yanakopatikana  badala ya kuchimba kwa kubuni  na kuamini kwenye mti fulani kuna madini mengi kama wengi wetu wanavyoamini.”

“Hii pia itatupunguzia matukio ya ajabu kwenye vyombo vya habari kila siku kuna taarifa za ajabu zinatoka Geita, hii inatokana na imani za kishirikina, kuna watu hadi sasa wanaamini darubini za kishirikina. Kuwa ukichinja kuku mweupe au mweusi anabaini madini yaliko lakini pia wapo wanaotafuta walemavu ili watumike kuonyesha madini yalipo”amesema Magembe.

Taarifa za GST zinaeleza tafiti za awali za uchunguzi wa miamba na madini zimefanyika kwa asilimia 16 pekee hapa nchini.

Oktoba 5, 2023 Waziri wa Madini, Antony Mavunde alisema Serikali imelenga kuongeza akiba ya taarifa za miamba ya madini kutoka asilimia 16 iliyopo sasa hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.

Sekta ya wachimbaji wadogo wa dhahabu imetoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya watu 1.2 milioni na ajira zisizo za moja kwa moja kwa watu zaidi ya milioni 7.2. Sekta hiyo  kwa ujumla huchangia asilimia 56 ya fedha za kigeni ambazo zinachangia asilimia 9.1 kwenye Pato la Taifa (GDP).