VIDEO: Hatua kwa hatua saa 2:20 SGR Dar-Moro

Muktasari:

  • TRC yafanya majaribio ya treni ya mwendo kasi inayotarajiwa kuanza rasmi kabla ya Julai kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma

Dar/Moro. Wakati safari rasmi za treni zikitarajiwa kuanza Julai mwaka huu, jaribio la kwanza la treni ya umeme ikiwa na mabehewa manne limefanyika jana kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ikitumia saa 2:20 kufika.

Muda huo ni upungufu wa saa 1:40 ya muda wa basi ambao kwa mwendo wa kawaida hutumia saa nne kutoka Dar hadi Morogoro.  Treni hiyo ilianza kurudi saa 7:48 na kufika Dar es Salaam saa 10:07,  ikitumia saa 2:19.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema majaribio yana taratibu zake, hivyo treni hiyo ilitembea kilomita 100 hadi 120 kwa saa kwa ajili ya usalama.

“Ingawa makadirio ni spidi 160, vichwa vyetu vinaweza kwenda hadi spidi 200, japo kwenye kona huwezi kwenda kwa spidi hiyo, ni kinyume na masharti tuliyopewa," alisema.

Hata hivyo, kutoka Stesheni ya SGR Posta hadi Pugu, kwa mujibu wa Kadogosa, treni hiyo ilitembea spidi 50 kutokana na ujenzi unaoendelea.

Amesema safari rasmi zitaanza mwishoni mwa Julai mwaka huu, kutokana na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, baada ya kuunganisha kipande cha Dodoma.

Kuhusu nauli, Kadogosa amesema wameshawasilisha mapendekezo Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), lakini kutokana na ubora wa huduma itaongezeka kidogo kulinganisha ile ya basi.

Umeme kukatika

Swali la wengi ilikuwa umeme utakapokatika katikati ya safari nini kitatokea? Kadogosa amesema kwa sasa hawatumii umeme mwingi.

“Kama tutaanza ile ya Mwanza na Kigoma hapo ndipo tutahitaji umeme mwingi, ingawa tuna ‘transimition line’ ambayo inajitegemea inahusu reli tu sio kitu chochote," amesema.

Alisema hata itatokea nchi nzima hakuna umeme, treni itaendelea kufanya kazi.

“Kuna vichwa vinatumia umeme na dizeli, ikitokea umeme umekatika abiria hawezi kujua tuna switch tu, hiyo ni kwa ajili ya tahadhari kama itatokea nchi nzima haina umeme, kwa sasa Dar es salaam ukikatika sehemu nyingine utakuwepo,” amesema.

Ikiwa na mabehewa manne, mawili ya business (daraja la juu) na mengine economy (daraja la kati), treni hiyo ilianza safari saa 4:30 asubuhi kwenye stesheni ya SGR Dar es Salaam na kuwasili Morogoro saa 6:50mchana.

Njiani, ikiwa imetembea kwa dakika 30, umeme wa ndani ya treni ulikatika kwa baadhi ya taa, soketi za kuchaji simu na viyoyozi kuzima, lakini treni iliendelea na safari bila abiria kuhisi chochote.

Muda mfupi badaye ulirejea na kukatika tena saa 5:18 na saa 5:59 lakini mara zote ulirejea baada ya mfupi, huku mara zote treni ikiendelea na safari, japo kila umeme ulipokatika kuna nyakati lilipunguza mwendo.

Masha Yassin, Ofisa Usafirisha Mwandamizi wa TRC amesema kuna vituo ilikuwa ikifika inabidi kuingiza umeme wa phase nyingine.

“Hiyo inaitwa nutro zone, maana kuna phase one, two na kuendelea, hivyo ili umeme wa phase nyingine uingie lazima wa phase nyingine ukate, ndicho kilikuwa kinatokea umeme unakata na kurudi ndani ya muda mfupi," alisema.

Akizungumzia safari ya jana ya majaribio, Kadogosa amesema ni ya tofauti, kwani imekuwa na mabehewa.

Muonekano wa treni ya umeme ikianza majaribio leo Dar-Morogoro

"Mwanzo tulikuwa tunafanya majaribio ya kichwa cha treni hii tu, leo (jana) tumefunga mabehewa manne, ingawa inaweza fungwa mabehewa 12 hadi 15," amesema.

Kutoka Stesheni Dar es Salaam jana, treni hiyo ilianza safari kwa mwendo wa kawaida, huku baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaan liiliokuwa ikipita wakiacha shughuli zao na kuifurahia, wengine wakiipungia mikono na wengine kuchukua video na picha mnato kwa simu

Ndani ya mabehewa, kwenye daraja la 'Economy' mabehewa yake yana vitu vya 3 by3 (siti za watu watatu watatu) na nyingine za 2 by 2 (wawili wawili), yakiwa na meza ndogo ya chakula kwenye kila kiti na kabati ndogo ya ukutani ya kutundika suti au nguo za aina hiyo.

Unaweza kuhama kutoka behewa moja kwenda jingine, ingawa pia huwezi kufanya hivyo kama mlango wa behewa lako umefungwa, hadi ufunguliwe na mhudumu.

Pia huruhusiwi kuweka mizigo chini ya kiti, kuna eneo maalumu la kuweka mizigo. Mradi wa treni ya umeme nchini ulianza mwaka 2017 na kuzinduliwa na Rais wa awamu ya tano, hayati John  Magufuli na kuendelezwa na mrithi wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Awamu ya kwanza kati ya Dar es salaam mpaka Morogoro ulielezwa ungekamilika ndani ya miezi 30 mpaka kufikia Novemba 2019, jambo ambalo halikuwezekana.

Iliongezwa miezi 18 mpaka Aprili, 2021, ikashindikana pia.

Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wakati huo, Leonard Chamuriho akaeleza reli hiyo ingeanza kufanya kazi ndani ya miezi minne, yaani Agosti 2021, ikashindikana tena.

Januari 17, 2022 aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali wakati huo, Gerson Msigwa alieleza kuwa awamu ya kwanza ya kipande cha Dar es Salaam mpaka Morogoro ungekamilika na majaribio yangeanza Aprili 2022, haikuwezekana hadi jana majaribio ya kwanza yalipoanza.

Alichokisema Matinyi

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi aliyekuwa sehemu ya safari hiyo amesema majaribio hayo ni uthibitisho wa Serikali kutimiza ahadi zake ikiwemo ile iliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan mwishoni mwaka jana na kwamba mpaka Julai mwaka huu treni hiyo itaanza safari zake.

“Tuna miezi michache kufika Julai na tayari tumefanya majaribio ya kwanza na tunatarajia kufanya majaribio mengine kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma na kurudi na hatimaye zitakuja kuanza shughuli rasmi za kibiashara treni zikibeba abiria na mizigo," alisema Matinyi.

Awali, ahadi ya kuanza kwa safari hiyo ilitolewa na Kadogosa akisema zitaanza Desemba 2022.