Uzalishaji umeme wapaa, wabunge walia uuzaji dizeli

New Content Item (2)
New Content Item (2)

Muktasari:

  • Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Bitekom amesema katika mwaka wa fedha 2024/25, utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Nishati utaongozwa na vipaumbele vinavyojikita katika kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.

Dodoma. Wakati Wizara ya Nishati ikiliomba Bunge kuidhinisha Sh1.883 trilioni, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetaka udhibiti wa uuzaji holela wa mafuta ya dizeli na petroli pamoja na bei tofauti za gesi asilia.

Pia, kamati imeitaka Serikali kuhakikisha Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) inashughulikia tofauti ya bei ya gesi asilia kama inavyotoa kwa bidhaa ya mafuta.

Akizungumza bungeni jana Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk David Mathayo alisema ongezeko la uuzaji holela wa mafuta ya dizeli na petroli maeneo ya vijijini linahatarisha usalama wa raia na mali zao.

“Serikali ihakikishe Ewura inaimarisha usimamizi wa biashara ya mafuta katika maeneo hayo ili kuepusha uwezekano wa kutokea majanga ya moto,” alisema Dk Mathayo wakati Wizara ya Nishati ilipowasilisha bungeni taarifa ya mapato na matumizi ya wizara hiyo na taasisi zake, ikiomba Bunge kuidhinisha Sh1.883 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akisoma taarifa ya mapato na matumizi ya wizara hiyo alitaja mafanikio waliyoyapata ni kuongezeka umeme uliounganishwa katika mfumo wa gridi ya Taifa hadi kufikia megawati 2,138 kufikia Machi mwaka huu, kutoka megawati 1,872.1 zilizozalishwa mwaka 2022/23, ikiwa ni ongezeko la asimia 14.2.

Dk Biteko alisema mafanikio mengine ni kukamilisha ujenzi wa mitambo ya kufua umeme ya Kinyerezi I Extension unaozalisha megawati 185, kwa sasa mitambo yote minne inafua umeme kiasi cha megawati 40 kila mmoja, hivyo kuwezesha uzalishaji wa umeme kuingizwa katika gridi ya Taifa. Pia, Dk Biteko alitaja ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa jua mkoani Shinyanga wa megawati 150 unaoendelea na matarajio ni umeme huo kuanza kuzalishwa ifikapo Januari, 2025.


Vipaumbele 2024/25

Naibu Waziri Mkuu huyo alisema katika mwaka wa fedha 2024/25, utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Nishati utaongozwa na vipaumbele vinavyojikita katika kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.

Dk Biteko amesema miongoni mwa yatakayofanyika ni kufikisha gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia, kupeleka nishati vijijini, ikiwamo katika vitongoji; kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia, ikiwamo wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG).

Pia, ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania.

“Wizara itaendelea kutekeleza na kusimamia shughuli za utafutaji na uendelezaji katika vitalu vya kimkakati na wawekezaji; usambazaji wa gesi asilia viwandani, katika taasisi na majumbani na kuimarisha matumizi ya CNG katika magari,” amesema.

Vipaumbele vingine alisema ni kuendelea na kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini na upatikanaji wa nishati ya mafuta vijijini kupitia uanzishwaji wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo.

Dk Biteko amesema pia kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli na ufanisi katika kushughulikia upatikanaji wa bidhaa hizo.

Dk Biteko alitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuimarisha uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, uzalishaji na usambazaji wa umeme.

Pia kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma, tija na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi na mashirika yaliyo chini ya wizara hiyo. Mashirika hayo ni Tanesco, TPDC, Ewura, Pura, PBPA pamoja na kampuni tanzu.

“Wizara itaendelea kuimarisha ushiriki wa wazawa katika shughuli za mafuta na gesi asilia na rasilimali watu ya wizara na taasisi zake na upatikanaji wa vitendea kazi muhimu,” alisema.

Kuhusu Mradi wa Kuzalisha Umeme kwa Kutumia Maji wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha MW 2,115, Dk Biteko alisema tayari uzalishaji umeanza kwa MW 235 kupitia mtambo Namba 9.

“Aidha, matarajio ni mradi huu kukamilika Desemba, 2024 kwa mitambo yote nane yenye uwezo wa kuzalisha MW 235 kila moja kuwa inazalisha umeme.”


Usambazaji gesi

Katika hotuba yake, Dk Biteko alisema Serikali itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani.

Alisema kazi zitakazotekelezwa ni kufanya tathmini ya athari kwa mazingira na jamii, usanifu wa kihandisi na ujenzi wa miundombinu ya kusambaza gesi asilia kwenye viwanda vya Mkuranga na Kongani ya Viwanda ya Kwala mkoani Pwani.

Nyingine ni kukamilisha ujenzi wa vituo vya CNG ambacho ni kituo mama katika eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na vituo vidogo vya Kairuki na Muhimbili, mkoani Dar es Salaam.

Dk Biteko alisema Serikali imejipanga kununua vituo vitano vya CNG vinavyohamishika vitakavyotoa huduma katika Jiji la Dar es Salaam.

“Sekta binafsi itaendelea kushiriki katika ujenzi wa vituo vya CNG na karakana za kubadilisha mifumo ya matumizi ya nishati ya gesi asilia kwenye magari,” alisema Dk Biteko.

Alisema Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) litakamilisha awamu ya kwanza ya mradi wa usambazaji wa gesi asilia chini ya ufadhili wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea).

Alisema nyumba 980 zitaunganishwa katika mikoa ya Lindi na Pwani; na kuanza awamu ya pili ya mradi huo kwa kuendelea kusambaza gesi asilia maeneo ya Mkuranga, mkoani Pwani.

“Katika mwaka 2023/24 Serikali iliendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuendeleza sekta ndogo ya mafuta na gesi asilia nchini katika maeneo ya utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji, usafirishaji na usambazaji wa bidhaa za mafuta na gesi,” alisema.

Katika utekelezaji, Dk Biteko alisema: “Ujenzi wa vituo vya kujaza gesi asilia (CNG) katika magari uliendelea kwa kushirikisha pia sekta binafsi.”

Alisema TPDC na Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA) ziliendelea na taratibu za kumpata mshauri mwelekezi wa kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa michoro ya kihandisi na tathmini ya athari ya mazingira na jamii ili kuwezesha GPSA kujenga vituo vya CNG katika bohari za Dar es Salaam na Dodoma.

Alisema hiyo ni hatua ya kuwezesha vyombo vya moto vinavyomilikiwa na Serikali kutumia CNG.

Dk Biteko alisema sekta binafsi iliendelea kutumia fursa ya matumizi ya CNG katika vyombo vya moto kwa kujenga vituo Dar es Salaam na Pwani, pamoja na karakana nane za kubadilisha mifumo ya matumizi ya CNG kwenye magari, ambayo ni nyenzo muhimu ya kuchochea matumizi ya gesi katika magari.

“Hatua hizi zimeendelea kuimarisha matumizi ya gesi asilia katika magari,” alisema.


Maoni ya kamati

Hata hivyo, katika maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wameitaka Ewura kushughulikia tofauti ya bei ya gesi asilia kama inavyotoa bei elekezi kwa bidhaa ya mafuta.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Mathayo alisema uwepo wa bei tofauti za gesi asilia miongoni mwa viwanda vinavyotumia gesi katika uzalishaji umesababisha malalamiko miongoni mwa watumiaji hao.

“Kwa kuwa jukumu mojawapo la Ewura ni kupanga bei ya gesi ili kuweka usawa miongoni mwa watumiaji, Serikali ihakikishe taasisi hiyo inatekeleza jukumu lake kama ilivyo kwenye mafuta, maji na umeme,” alisema.