Ujenzi laini kubwa ya kupokea umeme kutoka Bwawa la Nyerere waanza

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Gisima Nyamo-hanga akizungumza na waandishi wa habari walipotembelea miundombinu ya kituo cha kupooza umeme kutoka Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere (JNHPP) cha Chalinze mkoani Pwani leo Aprili 17, 2024. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Tanesco yakabidhi kazi kwa kampuni kutoka China, ujenzi kukamilika ndani ya miezi 22

Pwani.  Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limemkabidhi mkandarasi kutoka China ujenzi wa laini kubwa yenye urefu wa kilomita 345 ya kusafirisha umeme kutoka Kituo cha Chalinze mkoani Pwani kuelekea Dodoma.

Kazi ya ujenzi inatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi 22, mradi ukihusisha umeme wa msongo wa kilovoti 400.

Kampuni ya TBEA ya China inatekeleza ujenzi huo kutokana na udogo wa laini ya kupokea umeme kutoka Bwawa la Kuzalisha Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) linalotarajiwa kuzalisha megawati 2,115 baada ya kuwashwa mitambo yote tisa.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 17, 2024, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Gisima Nyamo-hanga amesema laini zilizopo zina uwezo wa kubeba megawati 850, hivyo zinazobaki zitabebwa na laini mpya inayoanza kujengwa kuwezesha kufikisha umeme sehemu mbalimbali nchini.

“Umeme unaoenda katika kituo cha Chalinze ni megawati 235 hiyo ni kutokana na udogo wa laini, itakapofunguliwa mitambo yote utapokea megawati 2,115,” amesema Nyamo-hanga.

Amesema kwa sasa wamekamilisha mradi wa umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka JNHPP.

“Miundombinu ya kuutoa umeme JNHPP tayari imekamilika umeme umefika hapa Chalinze, kama tulivyosikia mashine namba tisa imefunguliwa na umeme wake unaletwa hapa na kusambazwa katika gridi ya Taifa kwa ajili ya matumizi yetu,” amesema Nyamo-hanga.

Mbali na ujenzi huo, amesema ukaguzi wa miundombinu ya usafirishaji wa umeme unafanyika ili kurekebisha kwenye kasoro kwa kipindi hiki cha mvua.

Amesema wamekuwa wakipata hasara kwa nguzo kusombwa na maji.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Tanesco, Dk Rhimo Nyansaho amesema wamefika katika kituo hicho kumsisitiza mkandarasi kukamilisha kazi ndani ya miezi 22.

“Tumefika ili kumkabidhi mkandarasi na tunaamini kama kila kitu kipo, zikiwemo fedha tunataka afanye kazi kwa kipindi kisichozidi miezi hiyo na menejimenti mtusaidie kufanya tathimini na ufuatiliaji, ubora uzingatiwe,” amesema.

Dk Nyansaho amewataka menejimenti kusema mapema endapo mkandarasi hafanyi kazi ipasavyo ili waweze kuchukua hatua za tahadhari mapema.

Amesema licha ya kuwapo umeme wa kutosha lakini kusipokuwa na njia salama zenye uimara katika usafirishaji changamoto zitaendelea kwa baadhi ya maeneo.