Uchaguzi Serikali za mitaa bado mikononi mwa Tamisemi

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge asema Serikali imeeleza sababu, wao waitaka kuharakisha mchakato wa chombo kimoja kusimamia chaguzi zote.

Dar es Salaam. Wakati wananchi, wadau wa siasa na wanaharakati wakipinga uchaguzi wa Serikali za mitaa kusimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Serikali imesema ni ngumu kufanya mabadiliko kwa sasa.

 Imesema uchaguzi huo utakaofanyika baadaye mwaka huu, tayari maandalizi yake yamefanyika, hivyo ni ngumu kufanya mabadiliko.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumanne, Januari 30, 2024 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Dk Joseph Mhagama alipowasilisha maoni na ushauri wa kamati hiyo kuhusu Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa mwaka 2023.

“Kuhusu ibara ya 11 ya muswada huu, Serikali ilieleza kuwa uchaguzi wa Serikali za Vijiji, Mitaa na Vitongoji unafanyika mwaka huu (2024) na tayari maandalizi yameshafanyika, kwa hiyo itakuwa vigumu kwa sasa kubadili majukumu ya usimamizi wa uchaguzi huu.

”Hivyo, inaendelea kufanya utafiti juu ya namna bora ya kusimamia uchaguzi huo kwa siku za usoni,” amesema mwenyekiti huyo.

Amesema kamati inaishauri Serikali kuharakisha mchakato utakaowezesha kuwa na chombo kimoja pekee cha kusimamia chaguzi zote nchini, ikiwemo uchaguzi wa Serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.

Mkurugenzi wa uchaguzi

Dk Mhagama amesema katika ibara ya 9(3) ya muswada huo imemtaja mkurugenzi wa uchaguzi kuwa ndiye atakuwa Katibu wa Kamati ya Usaili wa wajumbe wa Tume.

Amesema ibara ya 18(1) ya muswada inaeleza mkurugenzi wa uchaguzi atateuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume.

Kuhusu ibara hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama amesema Serikali inapendekeza ibara ya 9 inayohusu kamati ya usaili ifanyiwe marekebisho.

Lengo la kuweka utaratibu wa kupendekeza kwa Rais majina kwa ajili ya uteuzi wa mwenyekiti na makamu mwenyekiti na kufanya usaili wa wajumbe watano wa Tume kama ilivyo sasa.

“Ibara hiyo inapendekezwa kufanyiwa marekebisho ili kumuondoa mkurugenzi wa uchaguzi kuwa katibu wa kamati hiyo na badala yake kumwezesha Rais kuteua ofisa mwandamizi katika utumishi wa umma kuwa katibu wa Kamati ya Usaili,” amesema Jenista.

Zikitumika rejea za uchaguzi uliofanyika mwaka 2019 ambao ulibainika kuwa na dosari, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Januari 24, 2024 kiliratibu maandamano ya amani kupinga muswada huo na mingine ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023 na Muswada wa Marekebisho yaSheria ya  Vyama vya Siasa wa mwaka 2023 kupelekwa bungeni, kikieleza inakiuka haki za wananchi.

Chadema imeahidi kuendelea kuratibu maandamano hayo hadi pale haki na sauti ya wananchi itakaposikilizwa.