Ubovu wa miundombinu chanzo katikakatika ya umeme

Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga akizungumza wakati akijibu maswali ya wabunge leo Jumanne Aprili 23, 2024 bungeni jijini Dodoma.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Baada ya Serikali kutangaza kuisha kwa mgawo wa umeme nchini, Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli amehoji ni lini changamoto ya kukatikakatika umeme itaisha.

Dodoma. Serikali imesema changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara inatokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza huduma hiyo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 23, 2024 na Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea,  Bonnah Kamoli.

Mbunge huyo alitaka kujua ni lini hasa changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini itaisha.

Akijibu swali hilo Kapinga amesema changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara inatokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza huduma hiyo.

‘Miundombinu hiyo inahitaji uwekezaji mkubwa sana ambapo Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu hiyo,” amesema.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2023/24, Serikali kupitia Tanesco imetumia jumla ya Sh109.89 bilioni kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya umeme na pia imetumia Sh105.51 bilioni katika miradi ya kuimarisha nguvu ya umeme Tanzania (Voltage Improvement projects).

Aidha, amesema kwa sasa, Tanesco imeanza kutumia nguzo za zege ambazo zinadumu muda mrefu zaidi.

Amesema Serikali kupitia Tanesco, itaendelea kuongeza bajeti kila mwaka ya matengenezo ya miundombinu ya umeme hadi tatizo hilo litakapokwisha kabisa.

Katika maswali ya nyongeza, Bonnah amehoji kwa kuwa Serikali inafanya uwekezaji mkubwa kwenye uzalishaji wa umeme, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha miundombinu iliyopo inaweza kuhimili umeme unaozalishwa sasa.

Amehoji pia kwa nini Serikali isifungue milango ili kukawa na ushindani kwenye huduma hiyo.

Akijibu swali hilo, Kapinga amesema kwa kuwa wameimarisha uzalishaji wa umeme sasa ni kuboresha miundombinu ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inakuwa ya uhakika zaidi.

“Miundombinu tunayoiweka itakuwa ni stahimilivu ili wateja wetu ambao ni Watanzania kupata umeme wa uhakika kwa wakati wote,” amesema.