TPA yafungua milango watumishi wake kwenda DP World

Muktasari:

  • Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imesema watumishi wanaotakata kwenda kuajiriwa na Kampuni ya DP World watalipwa stahiki zao baada ya kuacha kazi.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), imewataka watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam wanaotaka kuajiriwa na Kampuni ya DP World kujitokeza kuorodhesha majina kabla ya Machi 29, 2024.

TPA imesema katika mchakato wa uwekezaji bandarini hapo, “hakuna mtu yeyote atakayepoteza kazi.”

Machi 20, 2024, TPA ilitoa tangazo kwa watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam ikielezea mkataba walioingia na DP World ya Dubai unaohusu uendeshaji wa gati namba 0-3 na gati 4-7 kwa kipindi cha miaka 30.

Oktoba 22, 2023, TPA na DP World zilisaini mikataba mitatu mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Dodoma inayohusu uwekezaji na uendeshaji Bandari ya Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza ufanisi.

Kabla ya kutia saini mikataba hiyo, Serikali iliingia makubaliano na Serikali ya Dubai kuhusu uwekezaji huo (IGA). Mikataba hiyo ni wa nchi mwenyeji (HGA), wa ukodishaji na uendeshaji wa gati 4 – 7, na uendeshaji wa pamoja wa gati 0 – 3 kati ya TPA na DP World kwa shughuli za kibiashara na za kiserikali.

Katika tangazo lililotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Plasduce Mbossa kwenda kwa watumishi wa bandari, amesema kutokana na makubaliano yanayohusisha usimamizi na uendeshaji wa maeneo tajwa, watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam wanapaswa kuchagua kati ya kubaki TPA au kusitisha mkataba wa ajira wa TPA na papo hapo kuajiriwa upya na kampuni ya DP World.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, menejimenti imekamilisha shughuli ya utoaji elimu kwa watumiahi wote wa TPA walio kwenye maeneo husika, kazi iliyoanza Machi 4 hadi 19, 2024.

"Lengo la kutoa elimu ni kuwapa watumishi wote uelewa sahihi wa mabadiliko ya uendeshaji yanayoendelea Bandari ya Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine, elimu hiyo inahusisha mabadiliko ya uendeshaji wa bandari, utaratibu wa makabidhiano, mtumishi kusitisha mkataba na TPA na papo hapo kuajiriwa upya na kampuni ya DP World,” linaeleza tangazo hilo.

Imeelezwa elimu pia imejumuisha stahiki ambazo zitatolewa na TPA na kuajiriwa upya na Kampuni ya DP World.

Katika msisitizo imesema mtumishi anatakiwa kufanya hivyo kwa hiyari bila kushurutishwa.

"Kwa msingi huo nawajulisha watumishi wa Bandari ya Dar es Salaam makabidhiano kati ya TPA na Kampuni ya DP World yameanza kutekelezwa. Kwa kuwa zoezi la utoaji elimu kwa watumishi limekamilika," limeeleza tangazo hilo.

Mwananchi Digital limemtafuta Mbossa kupata ufafanuzi wa baadhi ya maswali, ikiwemo kama itatokea hakuna mtumishi hata mmoja atakayejitokeza itakuwaje? na je, kuna hakikisho la kwamba lazima wataajiriwa DP World?

Katika majibu yake, Mbossa ameanza kwa kusema: “Hakuna mtumishi yeyote wa TPA ambaye atapoteza ajira yake. Lakini niseme tu mpaka sasa zaidi ya watumishi 70 wamekwishajitokeza.”
Amesema iwapo wasingejitokeza bado wangeendelea kuwa wafanyakazi wa TPA kwa kufanyakazi eneo la DP World na DP World atawalipa TPA mishahara yao ambayo wao (TPA) watawalipa wafanyakazi.

Mbossa amesema wao wana bandari nyingi, wanaweza kuwahamishia zingine.

“Ninachoweza kusisitiza na kuwatoa hofu watumishi, suala hili tunaenda nalo kwa umakini na kama nilivyosema, hakuna mtumishi yeyote wa TPA atakayepoteza ajira yake,” amesema na kuongeza:

“Na iwapo ikitokea watumishi wote wa Bandari ya Dar es Salaam wakajitokeza kutaka kwenda kuajiriwa na DP World watalipwa stahiki zote, basi tutachukua jukumu la kuajiri watumishi wengine.”