Tanzania inaweza kuuza umeme nje

Dar es Salaam. Ingawa ndoto ya Tanzania kuuza umeme nje ya nchi hutafsiriwa kama kauli ya kisiasa, upo uwezekano wa kutimia iwapo mambo kadhaa yatazingatiwa kuelekea utekelezwaji wake.

Kiu ya biashara hiyo ya nishati nchini kwenda nchi za jirani, ilianza tangu mwaka 2013, Tanzania ikiwa mikononi mwa uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Julai 17, mwaka huo, aliyekuwa Waziri wa Nishati, Profesa Sospeter Muhongo alitangaza tarajio hilo la Tanzania kuingiza nishati yake ya umeme katika soko la nje ya nchi.

Kauli hiyo ilitokana na kile kilichoelezwa na Profesa Muhongo, kulikuwa na matarajio ya mapinduzi katika uzalishaji wa umeme, baada ya kusainiwa mkataba wa ujenzi wa mradi wa Kinyerezi.

Kukamilika kwa mradi huo, kulitarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme na hivyo, Tanzania kuwa na ziada ya Megawati 500 kufikia mwaka 2014.

Lakini, kukamilika na kuanza kufanya kazi kwa mradi huo, hakukuifanya ndoto hiyo itimie, bado umeme uliozalishwa wakati huo, ulikidhi sehemu ya mahitaji ya nchi na haukutosheleza kuuzwa nje.

Nchi za Kenya, Uganda na Malawi ndizo zilizotajwa kuwa soko la awali la umeme kutoka Tanzania na kwa mujibu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) tayari ujenzi wa njia za kusambaza nishati hiyo katika mataifa hayo ulishaanza.

Tumaini la uhai wa ndoto hiyo linatokana na ukweli kwamba, tayari Tanesco imefikia uwezo wa uzalishaji umeme zaidi ya mahitaji ya ndani ya nchi.

Kulingana na shirika hilo, Tanzania inazalisha megawati 1,872.05 za umeme, huku mahitaji ya nchi yakiwa ni megawati 1,363.94, hivyo kuna ziada ya megawati 508.11.

Si hivyo tu, matumaini mengine ya Tanzania kuuza umeme nje ya nchi yanatokana na utekelezwaji wa mradi wa uzalishaji umeme wa Julius Nyerere (JHPP) unaotarajiwa kuzalisha megawati 2,115.

Mei 30, mwaka huu, Waziri wa Nishati, January Makamba alisema ndoto ya Tanzania kuuza umeme nje ya nchi bado ipo, lakini Serikali inahitaji kujiridhisha na mambo kadhaa kabla ya kutimia.

Katika mazungumzo yake na kituo kimoja cha redio nchini, Makamba alisema, “ili kutimiza ndoto ya kuuza umeme nje, kwanza ni lazima umeme wetu uwe umejitosheleza kwa watu wetu wa ndani, pili kujenga ‘inter connector’ ambapo kwa sasa vitu vyote hivyo viwili bado havijakamilika.”


Itawezekanaje

Uzalishaji wa umeme wa kutosha ni moja ya nyenzo muhimu ya kufanikisha Tanzania kuwa na uwezo wa kuuza nishati hiyo nje ya nchi, kulingana na Profesa Emrod Elisante, mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Uwezekano wa hilo, anasema unatokana na kutumika ipasavyo kwa vyanzo mbalimbali vya uzalishaji wa nishati hiyo.

“Kuna chanzo cha jua, gesi ingawa tunatumia lakini bado chanzo hiki hakijatumika vya kutosha, tunahitaji kuongeza namna ili kituzalishie zaidi,” anasema.

Kwa mujibu wa Profesa Elisante, kwenye eneo la gesi asilia pekee inawezekana kupatikana Megawati 850 kutoka zinazozalishwa sasa.

Lakini, anaeleza ni muhimu katika uzalishaji na lengo hilo, kuzingatia ongezeko la mahitaji ya ndani, kwa kuwa kadiri siku zinavyokwenda ndivyo wanaohitaji wanaongezeka.

Profesa Elisante anaeleza vipo vyanzo vya umeme ambavyo hadi sasa havijaanza kutumika na vikitumika vitakuwa na tija na kuwezesha nchi kuwa na uwezo wa nishati na hata kuuza nje ya nchi.

Anavitaja vyanzo hivyo ni umeme wa mabaki ya mazao na mabaki ya viwandani.

“Ili kufikia azma hii na kwa uhakika hatupaswi kuacha chanzo chochote, tuhakikishe viwanda vinazalisha umeme na mabaki ya mazao,” anasema.

Mtaalamu wa uchumi kutoka chuo hicho, Dk Samwel Wangwe anasema uwekezaji katika miradi wezeshi kwa usambazaji umeme nje ya nchi ndiyo msingi wa kutimia kwa ndoto hiyo.

Ingawa kuna mashaka ya uwezo wa kiuchumi katika kutekeleza hilo, anasema sekta binafsi na wadau wengine washirikishwe kushirikiana na Serikali kwa kuwa gharama za uwekezaji huo ni kubwa.

“Uwekezaji ndiyo kila kitu, hapa kunahitajika ufanyike uwekezaji wa usambazaji wa umeme, lakini pamoja na miradi tuliyonayo tuwekeze katika miradi mingine ili wakati tunauza nje, tusipunguze kile kinachotumika ndani ukizingatia mahitaji huongezeka,” anasema.

Kuuza umeme nje ya nchi si sifa pekee, zipo faida lukuki ndani yake, kama anavyofafanua Dk Wangwe.

Anasema kwa kuuza umeme nje ya nchi, Tanzania itapata fedha za kigeni, itaongeza wawekezaji kwa kuwa na uhakika wa upatikanaji wa umeme.

Anaeleza mambo hayo yote matokeo yake ni kuimarika kwa uchumi wa nchi.

Anatoa angalizo kuwa, utekelezaji wa hilo usiathiri upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

“Unaweza ukauza huku ndani wanao wanaumia, tuhakikishe miradi itakayotumika kuuza nje inaongezwa ili ufike wakati tuwe tunauza nje, huku tunao wa kutumia ndani bila wasiwasi,” anasema.

Mtafiti na Mshauri wa masuala ya uchumi, Thobias Shija anasema biashara hiyo inawezekana kwa Tanzania, lakini ni muhimu kwanza ufanyike uwekezaji wa kutosha.

Kama alivyoeleza Makamba, anasema ni muhimu Serikali iwe na uhakika wa kutosheleza mahitaji ya ndani na ziada ndiyo ifanyiwe utaratibu wa kuuzwa.

Kuimarika kwa mahusiano baina ya Tanzania na nchi nyingine ni moja ya faida aliyoitaja, huku kuongezeka kwa mapato ikiwa ni faida nyingine.

“Faida kubwa ni mapato, tutazalisha umeme mwingi na kuweza kusambaza nje na hapo tutaingiza fedha kutokana na biashara hiyo na hata hivyo hatutauza bei sawa na tunayowauzia watu wetu wa ndani,” anasema.

Lakini, anasema mapato hayo hayatatumika kwenye uzalishaji umeme pekee, bali uwekezaji kwenye maeneo mengine utafanyika na hivyo Tanzania kufaidika.

Ongezeko la ajira ni faida nyingine itakayopatikana, akisema kwa kuwa kutakuwa na miradi mingi ya uzalishaji na usambazaji umeme, ni muhimu kuwepo vijana wa kuisimamia.

Kwa mujibu wa Shija, ingawa kuna matumaini ya kufikiwa kwa hilo, bado kuna safari ndefu, kwani inahitajika nchi ijitosheleze kwa mahitaji yake na ziada ndiyo iuzwe nje.

Mshauri wa masuala ya Mabadiliko ya Nishati Afrika, Silas Olan’g alieleza uwezekano wa kuuza umeme nje ya nchi utatokana na nchi kuzalisha umeme wa ziada na kuwa na uhakika wa vyanzo vyake. Anaeleza iwapo nchi itaingia mkataba inapaswa kuwa na uhakika wa usambazaji bila kukoma, ili kuepuka usumbufu kwa wateja.

Baada ya kujitosheleza, anashauri umeme huo unapaswa kuingizwa kwenye gridi ya kikanda ili nchi inayonunua ichukue kutoka humo.

“Ili kuuza lazima tuingize kwenye gridi ya kikanda ambayo nchi yenye umeme inaingiza humo unatumika na unalipwa na hata ukipungukiwa unatoa kwenye gridi hiyo na unatumia kisha utailipa nchi yenye ziada hiyo,” anasema.