Tanroad yataja vyanzo uharibifu wa barabara Geita

Watumishi wa Wakala wa Barabara Mkoani Geita wakifanya usafi katika eneo la soko Nyankumbu mjini Geita ikiwa ni maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma

Muktasari:

Watumishi wa Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Geita wameadhimisha wiki ya Utumishi wa Umma kwa kufanya Usafi katika Soko la Nyankumbu mjini Geita ikiwa na lengo la kuhamasisha na kutoa elimu juu ya kuhifadhi na kutunza barabara.

Geita. Shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo na biashara ndogondogo zinazofanywa kwenye hifadhi za barabara mkoani Geita zimetajwa kuwa chanzo cha wafugaji kuswaga mifugo katikati ya barabara na kuharibu miundombinu pamoja na kusababisha kizuizi kwa watumiaji wa barabara hizo.

Akizungumza na wananchi wa Mji wa Geita juu ya sheria, kanuni na adhabu mbalimbali kwa yeyote atakayebainika kuharibu miundombinu ya barabara, Kaimu Meneja wa Tanroad mkoani Geita, Fredrick Mande amesema mkoa huo unachangamoto kubwa ya mifugo kupita barabarani na kuharibu miundombinu.

Mande aliyeambatana watumishi wengine wa Tanroads wakiadhimisha wiki ya watumishi wa Umma kwa kufanya usafi katika Soko la Nyankumbu amesema pamoja na Tanroads kutoa elimu mara kwa mara na kupiga marufuku wafugaji kufanya shuguli za ufugaji mjini pamoja na kuzuia shughuli za kilimo na biashara kwenye hifadhi za barabara bado wameendelea kukaidi na kusababisha uharibifu wa miundombinu.

“Changamoto kubwa ya utunzaji wa barabara ni mifugo kupita barabarani maeneo mengi ya hifadhi yamevamiwa hivyo mifugo inakosa sehemu ya kupita na hivyo wafugaji kuswaga mifugo, tumeweka alama za kuonyesha kingo za barabara lakini bado wanakaidi”amesema Mande

Amesema mbali na uvamizi wa maeneo ya hifadhi ya barabara wizi wa alama za barabarani yakiwemo mabango na nguzo za vibao vya kupunguza mwendo kasi umeshamiri akidai ili kukabiliana na wizi wa alama za barabarani wamelenga kufanya misako kubaini zinakopelekwa ili hatua zichukuliwe kwa mujibu wa sheria.

“Kumekuwa na wimbi la wizi wa alama za barabarani kama nguzo na yale mabango ya kupunguza mwendo kasi hatujajua hivi vifaa wanavitumia kwenye shughuli gani lakini tumeanza misako na tukiwabaini watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria,”amesema Mande

Mwenyekiti wa Mtaa wa Uwanja, Enos Cherehani amesema madereva hususani wa pikipiki na bajaji wamekuwa wakitumia vibaya kivuko cha watembea kwa miguu na kusababisha ajali za mara kwa mara eneo la soko.

“Hawa madereva ni wagumu tuendelee kutoa elimu kwenye kivuko, unaona taa imemruhusu mtembea kwa miguu kuvuka lakini madereva bajaji au pikipiki nao wanapita hii imekuwa changamoto sana kwa watembea kwa miguu tunaomba askari awe anasimama hapa na kuwachukulia sheria,”amesema

Mkazi wa Nyankumbu, Mkanda Emoto amesema ili kukabiliana na uvamizi wa hifadhi za barabara pamoja na upitishaji wa mifugo barabarani Serikali inapaswa kutekeleza sheria kwa kutaifisha mifugo au kuwafikisha Mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine.