Tanesco, mamlaka za maji zakwamisha ujenzi wa barabara

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kishere akikabidhi ripoti ya ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka 2022/2023 kwa Rais Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Kutosomana kwa mifumo ya Tehama miongoni mwa taasisi za Serikali kumesababisha uharibifu na uchelewesha wa ujenzi wa barabara, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imesema.

Dar es Salaam. Kukosekana kwa mawasiliano miongoni mwa taasisi za Serikali kumetajwa kuwa sababu ya ucheleweshaji na upotevu wa fedha za ujenzi wa barabara nchini, kulikosababisha hasara ya zaidi ya Sh1 bilioni za miradi ya maendeleo nchini.

Hayo yamebainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kicheere alipokuwa akiwasilisha taarifa ya ripoti yake ya mwaka 2022/23 kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Chamwino Dodoma leo Machi 28, 2024.

Kichere amesema Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limekuwa halitekelezi maombi ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) ya kuhamisha nguzo za umeme kwenye maeneo ya barabara.

“Tanesco haizingatii maombi ya Tarura ya kuhamisha nguzo za umeme katika maeneo ya barabara. Hii inazuia moja kwa moja maendeleo ya miradi kadhaa yenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni. Wakati mwingine unakuta barabara imejengwa, lakini katikati kuna nguzo ya umeme au kwenye mabega ya barabara kuna nguzo ya umeme. 

Pia, CAG amezitaja mamlaka za maji, akisema zinachangia kuharibu barabara zilizotengenezwa na Tarura.

“Huko Arusha Serikali ilitumia Sh194.53 milioni katika mradi wa barabara, lakini ukaharibiwa na kazi za mamlaka za maji ambazo zilianza tu mara baada ya barabara kukamilika. Mamlaka ya maji sasa inatakiwa kuingia gharama nyingine ili kurekebisha barabara waliyoiharibu wakati wanaweka miundombinu yao,” amesema. 

Ametoa pia mfano wa ujenzi wa barabara ya Ngerengere – Kidunda yenye urefu wa kilometa 75 kwa gharama ya Sh1.91 bilioni.

“Februari 19, 2023, Dawasa iliwajulisha Tarura kuhusu mkataba iliosainiwa Oktoba 31, 2022 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la Kidunda, uliojumuisha ujenzi wa barabara Ngerengere – Kidunda yenye urefu wa kilometa 75 barabara hiyo hiyo hadi kiwango cha changarawe.

“Wakati Tarura inaarifiwa kuhusu ujenzi huo, ilikuwa imeshalipa Sh1.45 bilioni za ukarabati wa barabara hiyo. Wakandarasi wawili walikuwa wamekamilisha kazi yao, huku kazi ya wakandarasi wawili ikiwa inaendelea. Tarura ilitoa amri ya wakandarasi kusitisha kazi yao ili kuruhusu kazi ya Dawasa kuchukua mradi kwa uboreshaji uliokusudiwa,” amesema.

Amesema tatizo hilo linasabishwa na mifumo ya Tehama ya taasisi za Serikali kutokusomana na kukosekana kwa mawasiliano miongoni mwa taasisi hizo.