Takukuru yaanza kuchunguza safari ya China ya Mkurugenzi Geita

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Zahara Michuzi

Muktasari:

  • Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita imeanza kuchunguza safari ya China aliyokwenda Mkurugenzi wa Mji wa Geita (TD) Zahara Michuzi.

Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita imeanza kuchunguza safari ya China aliyokwenda Mkurugenzi wa Mji wa Geita (TD), Zahara Michuzi.

Uchunguzi huo umetokana na agizo la Mkuu wa Wilaya ya Geita, Corneli Magembe aliyeiagiza kuchunguza safari ya Zahara aliyokwenda nchini China kama ilikuwa kwa maslahi ya halmashauri au ni maslahi binafsi.

Pia aliitaka taasisi hiyo kubaini kama matumizi ya safari hiyo yalitokana na fedha za halmashauri au binafsi na endapo watabaini alitumia fedha za halmashauri fedha hizo zirejeshwe na zielekezwe kutekeleza miradi ya maendeleo.

Akizungumza na Mwananchi digtal ofisini kwake leo Novemba Mosi, 2023 Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Azza Mtaita amesema tayari uchunguzi w ajambo hilo umeanza na wanachoangalia ni kama kunataratibu zilizokiukwa.

Amesema kwa kuanza wanaangalia sheria inasema nini,kuwahoji mashahidi, kukusanya vielelezo na watakapojiridhisha ndipo watamhoji Mkurugenzi huyo.

“Uchunguzi una mambo mawili ‘negative na positive’ tutakapojiridhisha ndipo tutamhoji Mkurugenzi lengo la uchunguzi huu ni kupata ukweli na tutakapokamilisha tutatoa taarifa ya tulichobaini,”amesema Mtaita

Akizungumza jana na waandishi wa habari Zahara hakuwa tayari kuzungumzia safari hiyo ya China lakini akasema jambo hilo liendelee kama lilivyoelekezwa.

Akizungumzia tuhuma za kutokukaa ofisini, amesema wananchi wanapaswa kufuatwa walipo na kuonyeshwa fursa za uwekezaji huku akisema hakuajiriwa kukaa ofisini na kwamba ameajiriwa kutatua changamoto za Watanzania.

“Nimeajiriwa kutatua matatizo ya watanzania popote walipo ndio maana nimepewa gari nzuri, mafuta na dereva mzuri sioni sababu ya kukaa ofisini wakati vitendea kazi nimepewa nifike ‘site’ kutimiza wajibu wangu wa msingi masuala haya mengine naomba yaendelee kama yalivyoelekezwa,”amesema Zahara