Soko la Kariakoo sasa ni mwendo wa kidijitali

Kaimu Meneja wa Shirika la Masoko Kariakoo, Sigsibert Valentine akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

  •  Soko hilo lilianza kukarabatiwa Januari 2022 baada ya kuungua usiku wa Julai 10, 2021

Dar es Salaam. Shirika la Masoko Kariakoo limesema ukarabati wa soko umekamilika kwa asilimia 93, likitarajiwa kufunguliwa ndani ya mwezi mmoja kutoka sasa.

Kwa watakaohitaji maeneo ya kufanyia biashara wanatakiwa kuomba kwa kutumia mfumo wa kidijitali (Tausi).

Soko la Kariakoo lilikuwa katika ukarabati tangu Januari 2022 baada ya kuungua usiku wa Julai 10, 2021.

Moto ulisababisha hasara kwa wafanyabiashara kwa mali zao kuteketea. Kutokana na hilo, Serikali ilitenga Sh28 bilioni kwa ajili ya kulikarabati.

Ukarabati ulienda sambamba na ujenzi mpya wa soko dogo litakalokuwa na ghorofa sita kwenda juu na ghorofa mbili kwenda chini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Aprili 21, 2024 kuhusu maendeleo ya mradi huo, Kaimu Meneja wa Shirika hilo, Sigsibert Valentine, amesema kukamilika kwa soko hilo kunafika ukingoni, na kwamba mwezi mmoja kuanzia sasa litaanza kufanya kazi.

"Kumekuwa na maswali mengi tunayapata ikiwamo kwenu waandishi, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida wakitaka kujua soko litaanza kazi lini. Niwaambie tu tumefika mahali pazuri, malengo yetu ni kabla ya mwaka mpya wa fedha soko liwe tayari limeanza kazi," amesema Valentine.

Wafanyabiashara watakavyorudi

Akieleza utaratibu wa wafanyabiashara watakavyorudi sokoni hapo, Valentine amesema kwa waliokuwapo kabla ya soko kuungua, wamewekewa utaratibu wao kwani ahadi ya Serikali ni kuwarudisha wote waliokuwapo.

Kwa wapya, amesema watapaswa kuomba kupitia mfumo wa kidijitali wa kukusanya mapato na kutunza takwimu za biashara (Tausi).

Amesema uhakiki wa wafanyabiashara waliokuwepo unaendelea, japo hakuwa tayari kutaja idadi ya waliohakikiwa.

"Kutokana maboresho yanayofanyika katika uendeshaji wafanyabiashara katika soko jipya la Kariakoo na maagizo ya Serikali kutumia mifumo ya kielektroniki ili kuleta tija, shirika litatumia mfumo wa Tausi kutangaza maeneo ya biashara na kukusanya mapato," amesema.

Amesema wafanyabiashara walikuwapo wenye malimbikizo ya madeni hawataruhusiwa kurudi sokoni mpaka watakapokamilisha malipo.

Ameeleza hao mfumo wa Tausi hautawatambua kwa kuwa hauna taarifa zao.

"Takwimu zilizopo zinaonyesha Shirika linadai zaidi ya Sh497 milioni jitihada za kufuatilia madeni zinaendelea na mpaka sasa Sh15.8 milioni sawa na asilimia tatu zimekusanywa hadi kufika Aprili, 2024," amesema.

Meneja huyo ametoa wito kwa wafanyabiashara katika kipindi kilichobaki wakamilishe malipo ya madeni.

Ili mfanyabiashara kujisajili amesema atatakiwa kuwa na namba ya kitambulisho cha Taifa, namba ya simu iliyosajiliwa, namba ya utambulisho wa mlipakodi.

Kwa kampuni watapaswa kuwa na utambulisho wa mlipakodi wa kampuni kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na vielelezo vyote vya uanzishaji kampuni ikiwemo kutoka Brela.


Yanayotarajiwa

Valentine amesema wanatarajia baada ya wafanyabiashara kurejea kutakuwa na ongezeko lao kutoka 1,600 waliokuwapo awali hadi kufika 3,500.

Pia, kuwapo ajira za moja kwa moja zisizopungua 4,000, na kuboreshwa mandhari ya Jiji la Dar es Salaam ambalo ni kitovu cha biashara nchini.

Faida nyingine ni kuongezeka kwa mapato kupitia tozo, ada na ushuru kutoka Sh4 bilioni zilizokuwa zikikusanywa awali hadi Sh11 bilioni.

Pia, kuendeleza historia ya soko hilo kama kivutio cha utalii.

Amesema wanaendelea kushirikiana na ofisi ya mkuu wa mkoa katika maandalizi hayo ya soko hilo kufanya kazi saa 24.

Amesema wameshatuma maombi kwa ajili ya umeme ambao utawezesha uwepo wa taa zinazowaka saa 24 eneo hilo.

Pia, kutafungwa kamera za kisasa ili kulifanya eneo hilo kuwa katika hali ya usalama wakati wote.

Kutakuwa na huduma za kibenki na maduka ya kubadilishia fedha.


Wafanyabiashara, wananchi wafunguka

Akizungumzia hatua hiyo, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko dogo, Minja Msuya, amesema ni hatua nzuri kwa kuwa wengi walikuwa wamejishikiza maeneo ambayo si rafiki tangu ujenzi ulipoanza.

Ameiomba Serikali kuwafikiria wafanyabiashara  waliokuwa wapangaji, ambao idadi yao ni kubwa ukilinganisha na wamiliki.

Msuya amesema wanafika takribani 600 ukilinganisha na wamiliki wasiozidi 300.

"Nakumbuka kilio cha wafanyabiashara wapangaji tulikifikisha ofisi ya mkoa na jambo hilo likaanza kufanyiwa kazi kwa wafanyabiashara kujaza fomu maalumu, lakini hadi sasa tunaelekea soko kuanza kufanya kazi ukimya umetawala na wao kubaki njiapanda,” amesema.

"Kwa upande wa wamiliki sina shida nalo kwa kuwa tumeshirikishwa hatua zote  na uhakiki ila hawa wapangaji ndio naomba waangaliwe kwa kuwa nia ya kufanya biashara wanayo isipokuwa kwa miaka yote waliyokuwepo sokoni hapo  hawakupata bahati ya kumiliki maeneo kutokana  na ugumu wa upatikanaji wake," amesema.

Grace Godfrey, mkazi wa Kariakoo amesema kuanza kazi kwa soko hilo ni habari njema kwa kuwa kwa muda wote lilipokuwa likikarabatiwa walikuwa wanafanya manunuzi kwa wafanyabiashara waliopanga bidhaa chini ambao hawakuwapo kihalali.

Musa Makau, mfanyabiashara wa vifaa vya shule pembezoni mwa soko hilo amesema kuanza kazi kwa soko hilo kutachangamsha biashara zao kutokana na kipindi chote ambacho wafanyabiashara walikuwa hawapo zilidorora.

Ameomba ahadi ya  kulifungua mwaka huu itimizwe.