Simbachawene: Wabunge kuweni wapole

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene

Muktasari:

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene alisema mpango wa kupeleka fedha kwa halmashauri mbalimbali kwa ajili ya ujenzi unakwenda taratibu kulingana na upatikanaji wa fedha, hivyo wabunge wawe wapole.

Dodoma. Serikali imepeleka Sh100 milioni kati ya 500 zilizotakiwa kwa ajili a ujenzi wa nyumba za watumishi Wilaya ya Itilima, Bunge limeelezwa jana.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tamisemi, George Simbachawene alisema mpango wa kupeleka fedha kwa halmashauri mbalimbali kwa ajili ya ujenzi unakwenda taratibu kulingana na upatikanaji wa fedha, hivyo wabunge wawe wapole.

Simbachawene alitoa kauli hiyo kufuatia wabunge wengi kusimama na kutaka kuhoji juu ya ofisi za wilaya mpya zitajengwa lini, ikiwamo swali la Ritha Kabati kuhusu Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Midimu (CCM) alitaka kujua mpango wa Serikali kuwezesha kujenga ofisi na nyumba za watumishi Wilaya ya Itilima.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Suleiman Jafo alisema Sh100 milioni zilizopelekwa zilisaidia ujenzi wa nguzo za jengo. Alisema fedha hizo zilitengwa katika bajeti ya mwaka 2014/15 na katika mwaka wa huu 2016/17 zimetengwa Sh500 milioni ili kuendeleza ujenzi huo na nyumba ya mkuu wa wilaya.