Simbachawene aeleza machungu ya kutumbuliwa, atoa maelekezo

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene akizungumza na watumishi wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza. Picha na Saada Amir

Muktasari:

Simbachawene aliyekuwa nje ya Baraza la Mawaziri tangu mwaka 2017 alipoamua kujiuzulu kwa hiari nafasi yake ya Waziri wa Tamisemi baada ya Hayati Dk John Magufuli kuwataka wote walioguswa na kashfa ya mikataba mibovu na uendeshaji wa biashara ya madini kukaa pembeni kupisha uchunguzi.

Mwanza. ‘Uchungu wa mwana aujuaye mzazi’ ni msemo ambao unaweza kutumika kuonesha jinsi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene alivyoonesha machungu wanayopitia watumishi kufukuzwa kazi akijitolea mfano wa kutumbuliwa.

Simbachawene aliyekuwa nje ya Baraza la Mawaziri tangu mwaka 2017 alipoamua kujiuzulu kwa hiari nafasi yake ya Waziri wa Tamisemi baada ya Hayati Dk John Magufuli kuwataka wote walioguswa na kashfa ya mikataba mibovu na uendeshaji wa biashara ya madini kukaa pembeni kupisha uchunguzi baada ya ripoti ya biashara ya madini ya Tanzanite na almasi kuonyesha namna Serikali ilivyopoteza trilioni za fedha kutokana na mikataba mibovu.

Julai 21, 2019 alirejeshwa kwenye baraza hilo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) na baada ya miezi sita tangu aingie wizara hiyo, Simbachawene alihamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi leo Ijumaa, Agosti 4, 2023, Waziri huyo amewataka viongozi kuwasikiliza wanaowaongoza badala ya kutumia vibaya madaraka yao ikiwemo kuwafukuzisha kazi kwa sababu ya mamlaka yao.

“Unajua kuna kesi unachanganyikiwa, sisi wengine tuliowahi kutumbuliwa tunajua kutumbuliwa kunakuwaje. Kwahiyo jamani unapogusa kwenye kitu ambacho mtu anakitegemea akili yake haiwezi kuwa sawa,

“Akienda kwa wakubwa huko yeye ni mdogo, akifika anahisi yeye anaonewa kwahiyo hawezi kujieleza vizuri, anaingia na kilio akitoka huko anakuwa na kilio kikubwa zaidi, ndomana mimi katika sala zangu mtu akija ofisini kwangu ana majonzi nataka atoke akiwa hana majonzi hata kama sina uwezo,”amesema Simbachawene

Amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa (Ras) na wa Wilaya (Das) kusoma sheria zilizowapa majukumu ya nafasi zao na kuangalia muunganiko wa mamlaka zao, za kinidhamu na kiutawala ili wapunguze malalamiko ya watumishi yanayokwenda ngazi za juu ikiwemo Tume ya Utumishi wa Umma na kuyashugulikia wenyewe.

“Na mjiulize ninyi ambao ni viongozi mnasimamia wapi mtu anapokuja ofisini kwako ana majonzi na machozi yanamdondoka… kwanini asitoke hana machozi anafrahi mbona ni rahisi tu? Hata kama tatizo ni gumu si unaendelea kupambana nalo taratibu,”

“Unakuta binti ameanza kazi, amechukuliwa na mwanaume mtaani akazalishwa mtoto, mwanaume huyo kampeleka wakakope kwa kutumia kitambulisho chake wafungue biashara… jamaa anaondoka na hela anakimbilia Dar es Salaam yule binti ana mtoto mgongoni, mwanaume amemkimbia, mshahara hana amekopa pesa kesi hizo ni nyingi nyingi; Nyinyi huku (Maofisa utumishi) mnasema huyu mwalimu mtoro au huyu nesi mtoro afukuzwe kazi bila kujua ana changamoto gani,”amesema

Amewataka Ma Ras, Das na Wakuu wa wilaya kutokubali watumishi wahukumiwe na mamlaka za ndani kwa kufukuzwa kazi bila kujua matatizo yanayowasibu ili kutowaongezea matatizo zaidi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha amesema wilaya hiyo imewapa watumishi uhuru wa kujiamini kwenye nafasi zao na kuhudumia wananchi kwa kujituma na kwa weledi.

Mtumishi wa idara ya Afya, Jasmini Kajura amewaomba maofisa utumishi kuzingatia maelezo ya Waziri Simbachawene akidai si kila mtumishi mtoro kazini anapenda kufanya hivyo badala yake viongozi wafuatilie kabla ya kuchukua maamuzi ya kuwafukuzisha kazi kwakuwa wengine wanamatatizo yanayowachanganya ikiwemo mikopo umiza.