Siku ya kukumbukwa Muungano

Komandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), akiwa ameruka kwa miguu yote hewani na kuvunja mbao zilizokuwa zimeshikwa na wenzake wakati wa maonyesho ya kijeshi ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Muungano kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam jana. Picha na Emmanuel Herman

Muktasari:

Ni maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Dar es Salaam. Makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) jana walizipamba sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano, baada ya kuonyesha umahiri wa mapigano ya kujihami dhidi ya maadui kwa kutumia viungo vyao, huku baadhi ya askari wengine wakirusha ndege za kivita na kuruka na miamvuli (Parachute).

Unaweza kusema maelfu ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Uwanja wa Uhuru jana walikuwa wakiwasubiri wanajeshi hao, kwani baada ya kutambulishwa na Meja Evans Mtambi, wananchi hao walianza kuwashangilia kwa nguvu.

Makomando wenye miili ya ukakamavu waliingia katika uwanja huo saa 4:43 asubuhi wakiwa katika makundi matatu katika siku hiyo ambayo ni ya kukumbukwa.

Yalianza kuingia makundi mawili kwa mwendo wa kurukaruka kwa ukakamavu, huku wakitoa salamu ya utii kwa Rais Jakaya Kikwete, kitendo kilichozidisha shangwe uwanjani hapo.

Mara baada ya kupita kwa makundi hayo, liliingia kundi la tatu likiwa na makomandoo 18, ambapo 17 kati yao walikuwa wamevalia fulana nyeusi na suruali za kijeshi, huku kiunoni wakiwa wamening’iniza ala ya kuhifadhia kisu.

Walianza kwa kuonyesha mitindo mbalimbali ya kujihami na adui kwa kutumia viungo vyao, fimbo na visu huku wakijirusha hewani na kutua chini kwa mtindo wa aina yake.

Katika hali isiyotarajiwa, wanajeshi hao walianza kuvunja matofali kwa kutumia ngumi na kichwa, kitendo kilichowafanya wananchi na wageni mbalimbali waliohudhuria maadhimisho kuwashangaa kwa uhodari huo.

Wakiwa hawaamini wanachokiona, ghafla mmoja wa wanajeshi hao alilala chali na kupangiwa matofali mawili makubwa tumboni, ambayo yalivunjwa na mwenzake aliyetumia nyundo kubwa.

Huku baadhi yao wakiwa wamevua fulana na kubaki vifua wazi, walianza kuchapana kwa kutumia mbao ngumu katika miili yao.

Kila mbao hizo zilipokuwa zikitua katika miili ya wanajeshi hao, zilikuwa zikipasuka vipandevipande mithili ya ubao uliokanyagwa na lori la mizigo.

Kuruka kwa miamvuli

Kivutio kingine kilikuwa ni wanajeshi watano walioruka kwa miamvuli (Parachute) kutoka umbali wa futi 4,500 kutoka usawa wa bahari huku wakielekezwa jinsi ya kutua na moshi wa kijani ambao husambaa hewani kwa kufuata uelekeo wa upepo.

Wanajeshi hao waliokuwa wamejifunga bendera za Tanzania kiunoni, waliruka kutoka katika ndege ndogo mbili zilizopita juu ya uwanja huo na kuanza kutua chini taratibu huku wakiwa wanazunguka angani kwa mtindo wa kubinuka sarakasi.

Mara baada ya kutua salama wanajeshi hao waliitwa na Rais Kikwete katika jukwaa kuu na kuwapa pongezi kwa kushikana nao mikono.

Ndege za kivita

Tukio lingine lililowachanganya mamia ya wananchi waliofurika katika uwanja huo, ni jinsi ambavyo ndege za kivita zilivyopita angani.

Zilianza kupita ndege tatu za mafunzo ambazo zilitoa moshi wenye rangi ya bendera ya taifa, baada ya dakika tatu zikapita ndege nyingine tatu za mafunzo ya awali na kufuatiwa na ndege ndogo mbili na kubwa moja za usafirishaji.

Baadaye ilipita ndege inayotumiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano ikiwa imezungukwa na ndege nyingine mbili za kuilinda na maadui, na kufuatiwa na ndege nyingine tatu za kivita ambazo zilijizungusha hewani na kufuatiwa na nyingine moja iliyopita kwa kasi na kupaa juu zaidi.

Ndege moja ya mwisho kupita uwanjani hapo ilijizungusha angani kama ishara ya kutoa heshima kwa Rais Kikwete.

Magereza

Jeshi la Magereza nalo halikuwa nyuma katika maadhimisho hayo, kwani lilionyesha mfano wa kupambana na kuwakamata wafungwa na mahabusu wanaoleta vurugu katika magereza.

Polisi

Pia Jeshi la Polisi, kikosi cha mbwa nalo lilionyesha umahiri wake wa kukamata wahalifu kwa kutumia mbwa waliopewa mafunzo maalumu, ambao mbali na kukamata wahalifu pia wana uwezo mkubwa wa kusikia na kubaini harufu ya dawa za kulevya.

Halaiki

Vijana wa halaiki 3,475 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar nao walipamba maadhimisho hayo baada ya kuonyesha umahiri wa kuruka sarakasi, kuchora maumbo yenye ujumbe wa miaka 50 ya Muungano pamoja na kuimba nyimbo mbalimbali za kusifu Muungano.

Wanamuziki

Wanamuziki wa miondoko mbalimbali nchini nao walikuwa miongoni mwa watu waliozipamba sherehe hizo baada ya kuimba nyimbo mbili za kusifu Muungano.

Vijembe

Wakati JWTZ wakionyesha silaha za kivita kama vifaru vyenye uwezo wa kutembea nchi kavu, magari ya kubebea madaraja na kutungulia ndege, Meja Mtambi alikuwa akitumia lugha za vijembe zilizotafsiriwa kama onyo kwa wanaoichokoza Tanzania.

“Hakuna adui kutoka sehemu yoyote anayeweza kuchezea anga la Tanzania, atakayejaribu atakiona cha mtema kuni,” alisema na kuongeza;

“Ndege hizi hutoa mlio mkali. Unaposikia mlio huo ujue upo salama lakini ujikague kwanza huenda masikio yanasikia lakini sehemu nyingine za mwili hazipo.”

Kauli za JK

Alianza kwa kusema hakusudii kutoa hotuba kwa kuwa angeharibu utamu wa sherehe hiyo, huku akisema wananchi wengi wamefurahishwa na matukio waliyoyaona.

Rais Kikwete aliwatambulisha viongozi mbalimbali wa kimataifa waliohudhuria sherehe hizo.

“Wa tatu ni mwenyeji kwetu, ndugu yetu, mwenzetu, amesoma hapahapa, amejifunzia uanamapinduzi hapahapa, naye siyo mwingine bali ni Yoweri Kaguta Museveni,” alisema huku akishangiliwa na wananchi.

Aliongeza kuwa: “Wanasema watu wengi waliokwenda kufanya ukorofi kwenye nchi zao walipita hapahapa sina uhakika na hilo.”

Aliwataja marais John Galang (marehemu), Museveni na Laurent Kabila (marehemu), kwamba walianzia harakati za ukombozi wa nchi zao Tanzania.

Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Godluck Eliona na Ibrahim Yamola.