Serikali mbioni kurudisha shule za ufundi

Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda

Muktasari:

  •  Serikali imeanza mchakato wa mapitio ya sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na kuboresha mitaala ya elimu ili iweze kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa na stadi za ujuzi katika shule 123 zilizokuwa zikitoa elimu hiyo.


Dodoma. Serikali imeanza mchakato wa mapitio ya sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na kuboresha mitaala ya elimu ili iweze kuwajengea uwezo wanafunzi kuwa na stadi za ujuzi katika shule 123 zilizokuwa zikitoa elimu hiyo.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Jumatano na Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda wakati akijibu swali la Mbunge wa Hai, Saashisha Mafuwe.

Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itafufua shule za msingi za ufundi zilizopo Wilaya ya Hai na kuweka utaratibu kwa wanafunzi wa shule hizo kufanya mitihani na kupata vyeti.

Waziri amesema mara baada ya mitaala tajwa kukamilika pamoja na manunuzi ya vifaa na mashine mbalimbali za ufundi, Elimu ya Ufundi itatolewa katika shule za msingi na sekondari.

Amesema utaratibu wa kufanya mitihani ya Elimu ya Ufundi na kupata vyeti utaandaliwa kwa kushirikiana na mamlaka husika ikiwemo Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET).

“Mheshimiwa Spika, pamoja na mapitio ya Sera na Mitaala, Serikali inaendelea kufanya maboresho makubwa katika Chuo cha Ualimu Kleruu na Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Morogoro (MVTCC) kwa kufanya ukarabati wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa mabweni ya Wanafunzi kwa lengo la kuongeza fursa ya mafunzo kwa Walimu wa masomo ya Ufundi,” amesema Profesa Mkenda.

Kwa mujibu wa Waziri, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya kimeanza maandalizi ya utoaji wa mafunzo hayo katika ngazi ya Stashahada katika Elimu ya Ufundi (Diploma in Technical Education) na Postgraduate Diploma in Technical Education ambapo kwa sasa mitaala ya masomo inafanyiwa kazi na Tume ya Vyuo Vikuu ili kuidhinishwa na kuanza kutumika katika chuo hicho.