Serikali kuanzisha gridi ya Taifa ya maji 

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza wakati akijibu maswali ya wabunge leo Jumanne Aprili 23, 2024 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Baada ya wabunge kutoa ushauri wao bungeni, Serikali imesikia kilio chao na sasa imeanza safari ya kuelekea kwenye mpango huo.

Dodoma. Wizara ya Maji imeanza safari kwa ajili ya kuwa na gridi ya Taifa ya maji na katika mwaka 2024/25 itaajiri mtaalamu mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu wa mpango huo.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 23, 2024  na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Buhigwe Kavejuru Felix.

Mbunge huyo amehoji Serikali ina mpango gani wa kuanzisha mradi wa gridi ya maji ya Taifa kwa kutoa maji Ziwa Victoria na Tanganyika.

Akijibu swali hilo, Aweso amesema Serikali inaendelea na maandalizi ya utekelezaji wa gridi ya Taifa ya maji inayolenga kutumia vyanzo vya uhakika yakiwamo  maziwa na mito.

“Kwa sasa hatua iliyofikiwa ni ya kuajiri mtaalamu mshauri atakayefanya upembuzi yakinifu wa mpango huo anayetarajiwa kuajiriwa katika mwaka wa fedha 2024/25,”amesema.

Amefafanua kuwa  Serikali imeanza kutumia vyanzo vikubwa vya maji vya uhakika yakiwemo maziwa, mito mikubwa na mabwawa kwa ajili ya kusambaza huduma ya maji kwenye maeneo ambayo hayana vyanzo vya uhakika vya huduma hiyo.

Ametoa mfano ni mradi wa kutoa maji ziwa Victoria ambao umenufaisha miji ya Kahama, Shinyanga, Tinde, Nzega, Tabora, Igunga na Shelui.

Katika swali la nyongeza Felix amehoji Serikali ina mkakati gani wa kutumia Bwawa la Mwalimu Nyerere kama chanzo kipya cha maji kitakachosaidia katika ujenzi wa gridi ya Maji ya Taifa.

Pia amehoji mkakati wa Serikali katika kutafuta vyanzo vya pesa vitakavyosaidia ukamilishaji wa ujenzi wa mabwawa ya Farkwa na Kidunda, yatakayoweza kuingia kwenye mpango wa maji ya gridi ya Taifa.

Akijibu maswali hayo, Aweso amesema mkakati wa Wizara ya Maji na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa wanatumia rasilimali zote toshelevu.

Amesema bwawa la Mwalimu Nyerere wameliainisha, na kuwa mkakati wao sasa hivi ni kumpata mtaalamu mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi na kuhakikisha kuwa maji hayo yanakwenda Dar es Salaam na Mkoa wa Lindi.

Kuhusu kuwa na vyanzo vipya vya fedha, Aweso amesema wizara yake imejipanga kuvitafuta.