Sera ya elimu bure alama isiyofutika kwa serikali ya awamu ya tano

Sera ya elimu bure alama isiyofutika kwa serikali ya awamu ya tano

Muktasari:

  • Elimu ni miongoni mwa sekta ambazo marehemu Rais John Magufuli alizivalia njuga katika utawala wake. Licha ya mafanikio yaliyopatikana, changamoto nazo hazikukosekana pamoja na kuwapo kwa jitihada za kuzitafutia mwarobaini.


Elimu ni miongoni mwa sekta ambazo marehemu Rais John Magufuli alizivalia njuga katika utawala wake. Licha ya mafanikio yaliyopatikana, changamoto nazo hazikukosekana pamoja na kuwapo kwa jitihada za kuzitafutia mwarobaini.

Alipoingia madarakani Novemba 2015 alianza kutekeleza:

Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyotamka kuwa Serikali itahakikisha Elimumsingi (elimu ya awali hadi kidato cha nne), inakuwa ya lazima na ya bure kwenye shule za umma.

Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Ufundi ilitoa Waraka wa Elimu na 5 wa Mwaka 2015 ambao ulifuta ada kwa elimu ya sekondari, kidato cha kwanza mpaka cha nne, kwa shule za umma na michango yote katika elimumsingi.

Waraka huu pia ulifuta Waraka namba 8 wa mwaka 2011 kuhusu michango shuleni.

Waraka huo ulielezea kuwa, Serikali itaanza kutoa elimu pasipo malipo kwa elimumsingi kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne, kuanzia mwaka wa masomo wa 2016 ambapo kiasi cha Sh 131.4 bilioni kilitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa sera hiyo kwa kipindi cha miezi sita.

Kabla ya utekelezaji wa sera hiyo, gharama za elimu msingi zilichangiwa na Serikali na wazazi.

Hata hivyo, wazazi walionekana kubebeshwa mzigo mzito wa kuchangia gharama, hali iliyowafanya baadhi ya wazazi kushindwa kupeleka watoto shule.

Kutokana na utoaji huo wa elimu bila malipo, ongezeko la wanaoandikishwa kuanza darasa la kwanza na wanaoingia kidato cha kwanza na cha tano limekuwa kubwa kwa sababu ya mwamko wa wazazi.

Hali hiyo ikasababisha kuwapo kwa changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa vyumba vya madarasa ili kuhimili ongezeko kubwa la wanafunzi hao, uchache wa walimu na uhaba wa zana za kujifunzia na kufundishia.

Matokeo ya kuvutia katika takwimu

Kwa mujibu wa kitabu cha hali ya uchumi cha mwaka 2016, mwaka huo ambao ndiyo ulikuwa mwanzo wa utekelezaji wa elimu bila malipo, idadi ya wanafunzi wa elimu ya msingi iliongezeka hadi kufikia wanafunzi zaidi ya 8.63 milioni kutoka zaidi ya wanafunzi 8.29 milioni.

Aidha, katika kipindi hicho, idadi ya wanafunzi katika shule za msingi za Serikali ilikuwa zaidi ya 8.34 milioni ikilinganishwa na zaidi ya wanafunzi 8.01 milioni mwaka 2015 ambapo wasichana walikuwa zaidi ya 4.22 milioni na wavulana zaidi ya 4.11 milioni.

Kwa upande wa shule za sekondari, mwaka 2016, idadi ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita katika shule za sekondari ilikuwa wanafunzi zaidi ya 1.8 milioni ikilinganishwa na wanafunzi zaidi ya1.77 milioni mwaka 2015, sawa na ongezeko la asilimia 1.8.

Pia wanafunzi waliojiunga na elimu ya sekondari kwa kidato cha kwanza mwaka 2016 walikuwa 538,826 ikilinganishwa na wanafunzi 448,826 mwaka 2015, sawa ongezeko la asilimia 20.1.

Mwaka 2018 kitabu hicho kikaeleza kuwa, idadi ya wanafunzi katika elimu ya msingi ilikuwa zaidi ya 10.11 milioni ikilinganishwa na wanafunzi zaidi ya 9.31 milioni mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 8.5.

Kwa upande wa elimu ya sekondari, idadi ya wanafunzi iliongezeka kutoka wanafunzi zaidi ya 8.96 milioni mwaka 2017 hadi wanafunzi zaidi ya 9.71 milioni mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 8.3.

Vilevile, kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wa rika lengwa (miaka 7-13) kiliongezeka hadi asilimia 91.1 kutoka asilimia 84.0 mwaka 2017.

Changamoto

Pamoja na mafanikio hayo, changamoto hazijakosekana. Kwa mfano, utafiti uliofanywa na shirika la HakiElimu hivi karibuni umeonyesha kuwepo kwa ongezeko la wanafunzi kila mwaka na ongezeko hilo linatabiriwa kupitiliza kuanzia mwaka 2022.

Kutokana na hilo, HakiElimu ikashauri Serikali kuwekeza Sh1.2 trilioni katika miundombinu ya elimu ili kumaliza tatizo la uhaba uliopo.

“Kunatakiwa kuwa na mpango wa miaka mitano ambao kila mwaka zitengwe Sh250 bilioni,” inasema sehemu ya ripoti ya utafiti huo.

Aidha, utafiti huo unaonyesha mwaka 2016 kulikuwa na wanafunzi 12,847 walioshindwa kujiunga na kidato cha kwanza katika mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma na Mtwara kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Mwaka 2018 kulikuwa na wanafunzi 133,747 walioshindwa kujiunga na kidato cha kwanza kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa. Hali ikawa hivyo hivyo mwaka 2019 (wanafunzi 59,765).

Kwa mujibu wa takwimu za Elimu Msingi (Best) za mwaka 2019, uwiano kati ya walimu na wanafunzi ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 70, badala ya mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45.

Aidha, wakati kukiwa na jumla ya madarasa 133,748 ya shule za msingi, yanahitajika madarasa 82,200 ili kuziba pengo la uhaba wa madarasa.

Wasemavyo wadau

Akizungumzia hali ya elimu katika utawala wa Rais Magufuli, Meneja wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Nicodemus Shauri anasema kitendo cha Rais Magufuli kutekeleza Sera ya Elimu ya 2014 kilikuwa cha ujasiri.

“Kwa sababu hiyo sera ilikuwepo tangu mwaka 2014 baada ya kupitishwa na Rais Jakaya Kikwete. Yeye ndiye aliyeanza kuitekeleza. Hata hivyo kumekuwa na changamoto nyingi,” anasema Shauri.

Anataja changamoto hizo kuwa ni pamoja na ongezeko la wanafunzi wakati miundombinu, walimu na vifaa vya kufundishia vikiwa havitoshi.

“Wanafunzi wengi wameandikishwa na wengine wanaingia kidato cha kwanza, lakini miundombinu haitoshi. Walimu ni kweli waliajiriwa, lakini bado hawatoshi,” anaeleza

Anaongeza kuwa dhana ya elimu bila ada haikutafsirwa vizuri, matokeo yake hata ile michango ya wazazi iliyokuwa ikisaidia iliondolewa na kusababisha matatizo zaidi.

“Elimu bila ada ni sawa, lakini michango ya wazazi ilisaidia kuajiri walimu waliokosekana, kulipa walinzi, kuendeleza ujenzi na chakula cha wanafunzi. Kusema ukweli elimu bure imerudisha mno nyuma juhudi za kutoa elimu kwa wanafunzi. Hizo Sh23 bilioni zinazotolewa kila mwezi na Serikali hazitoshi kitu,” anasema Shauri na kupendekeza Serikali kurejesha michango iliyokuwa ikitolewa na wazazi kwa lengo la kuboresha elimu.