Rais Samia mgeni rasmi ‘The Citizen Rising Woman’

Rais Samia Suluhu Hassan.

Muktasari:

  • Mpaka sasa gazeti la The Citizen limeshachapisha makala za wanawake viongozi kutoka sekta mbalimbali 217 na msimu huu unaoisha una jumla ya makala za wanawake 240.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tuzo za msimu wa nne wa kampeni ya   ‘The Citizen Rising Woman’ zinazofanyika Ijumaa Machi 8, 2024 katika ukumbi wa The Super Dome uliopo eneo la Masaki, jijini Dar es Salaam.

 Rais Samia pia anatarajiwa kushiriki mahojiano ya ana kwa ana kuhusu mchango wa Serikali katika kuwezesha wanawake nchini kwenye uongozi wa nyanja mbalimbali.

Mhariri Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Limited (MCL), Victor Mushi, amesema utoaji wa tuzo hizo, utaambatana na matukio mbalimbali yatakayohanikiza maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani ambayo huadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka.

Itakumbukwa tuzo hizi zilianza kuratibiwa na Kampuni ya MCL mwaka 2021.

Mushi amesema tuzo hizo hutolewa kwa kuzingatia vipengele viwili. Cha kwanza ni kwa waajiri wenye sera imara au programu maalumu zinazolenga kuwainua wanawake kufikia malengo yao kwenye kampuni husika.

Kipengele cha pili ni kwa waajiri walioajiri wanawake wengi kwenye nafasi za juu za uongozi.

Ikiwa ni miaka minne imetimia tangu kuanza kwa mradi wa The Citizen Rising Woman,  mpaka sasa gazeti la The Citizen limeshachapisha makala za wanawake viongozi kutoka sekta mbalimbali 217 na msimu huu unaoisha una jumla ya makala za wanawake 240.

Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Bakari Machumu, amesema: “Wakati kampeni ya Rising Woman inaanza mwaka 2021, kampuni ya Mwananchi Communications Ltd haikuwa na mwanamke hata mmoja katika uongozi wa juu wa kampuni. Miaka minne baadaye wanawake wako asilimia 30 kwenye ngazi hiyo na tunaonyesha namna tunavyoishi kwa vitendo kile tunachokiamini na kukitangaza kwa jamii. Hii ni hatua kubwa kwetu kuelekea 50 kwa 50,” amesema Machumu.

Mada mbalimbali zitatolewa sambamba na sherehe hiyo kutoka kwa  Mkurugenzi Mtendaji wa Global Compact Network Tanzania, Marsha Macatta, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Serengeti, Dk Obinna Anyalebechi, Mwanzilishi mwenza wa Empower, Miranda Naiman na Kamishna Mkuu wa Jeshi la Uhamiaji, Dk Anna Makakala.

Mchokoza mada atakuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi.