Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima kwa mara ya nne

Muktasari:

  • Ni kwa kutambua uongozi wake wa kipekee katika kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, ambayo yameboresha ustawi wa Watanzania, kukuza sifa ya Tanzania duniani kote na kuendeleza mahusiano ya kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kutunukiwa shahada ya udaktari wa heshima katika uchumi na Chuo Kikuu cha Ankara nchini Uturuki Alhamisi, Aprili 18, 2024.

Hayo yameelezwa leo Jumatano Aprili 17, 2024 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba katika ukurasa wake wa mtandao wa X.

“Seneti ya Chuo Kikuu cha Ankara, chuo kikuu cha pili kwa ukubwa nchini Uturuki, imeamua kwa kauli moja kutoa udaktari wa heshima wa uchumi kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

“Kwa kutambua uongozi wake wa kipekee katika kuendeleza mageuzi ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, ambayo yameboresha ustawi wa Watanzania, kukuza sifa ya Tanzania duniani kote na kuendeleza mahusiano ya kibiashara, kiuchumi na kisiasa kati ya Tanzania na nchi nyingine, ikiwemo Uturuki,” ameandika Makamba.

Makamba ameongeza kuwa hafla hiyo itaongozwa na uongozi wa chuo hicho na kuhudhuriwa na mawaziri, wanadiplomasia, kitivo na wanafunzi.

Shahada hiyo ya udaktari wa heshima itakuwa ya nne kwa Rais Samia kutunukiwa baada ya awali kutunukiwa nyingine na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru nchini India na Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza).

Rais Samia anaanza ziara ya kitaifa ya siku tano nchini Uturuki kuanzia leo Aprili 17 hadi 21, 2024 kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdoğan.

Samia anakwenda ziara hiyo ikiwa ni miaka 14 imepita tangu Rais wa Tanzania alipotembelea nchi hiyo ikiwa ni miaka saba tangu Rais wa nchi hiyo, Recep Tayyip Erdogan alipotembelea Tanzania, Januari 2017.

Akitangaza ziara hiyo juzi, Makamba alisema lengo la ziara hiyo ni kuimarisha mahusiano ya kibiashara na kiuchumi kwani Tanzania inahitaji mitaji, teknolojia na wawekezaji.

Mbali na Rais Samia kufanya mazungumzo ya kiserikali na mwenyeji wake, atakwenda mjini Instanbul ambao ndiyo mji wa kibiashara ambako limeandaliwa kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Uturuki, ambalo litakutanisha wafanyabiashara wa pande zote.

Baada ya kongamano hilo, Rais atakutana na kampuni kubwa 15 nchini humo kwa ajili ya kuwashawishi kuja kuchangamkia fursa zilizopo Tanzania.

“Kuna maeneo ambayo tunashirikiana nao yalitarajiwa kuwa maeneo zaidi ya 10 lakini hadi sasa tuna maeneo kama sita,  ambayo yamethibitishwa kuwa tutasainiana mikataba na hati za makubaliano,” amesema Makamba.

Miongoni mwa maeneo ambayo wanatarajia kuingia makubaliano Tanzania na Uturuki ni ufadhili wa masomo ya elimu ya juu.