Rais Samia atekeleza asilimia 95 hoja za Tucta

Rais Samia Suluhu Hassan akiingia katika uwanja wa Jamuhuri mjini Dodoma ambapo alikuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi)

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imetekeleza kwa asilimia 95 maombi yaliwasilishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), ikiwemo nyongeza za mishahara na kupandisha madaraja kwa watumishi.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amesema maombi mbalimbali yaliyowasilishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), ikiwemo nyongeza za mishahara na kupandisha madaraja kwa watumishi yametekelezwa kwa asilimia 95.

Maombi mengi ambayo yaliyowasilishwa Mei Mosi mwaka 2022 katika maadhimisho hayo ni kulipwa kwa mafao kwa wakati kwa watumishi wanaostaafu, pia kulipwa mafao kwa watumishi waliondolewa kazini kutokana na dosari ya vyeti feki. Kuondolewa kwa tozo katika miamala ya benki.

Mengine ni mikataba na hali bora ya wafanyakazi kwa taasisi za umma, uidhinishwaji wa miundombinu ya taasisi na ushirikishwaji wa mapitio ya sheria na miongozo mbalimbali katika sehemu ya kazi.

“Wafanyakazi ninyi ni mashahidi, sehemu ndogo sana imebaki na Serikali inaendelea na utekelezaji,” amesema Rais Samia katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi iliyofanyika kitaifa leo Jumatatu Mei Mosi 2023 mkoani Morogoro.


Maadhimisho ya mwaka huu, yalikuwa na kauli mbiu ya ‘mishahara bora na ajira za staha ni nguzo kwa maendeleo ya wafanyakazi na wakati ni sasa’ ambapo Rais Samia amesema kauli mbiu hiyo ina lengo la kuboresha maisha ya wafanyakazi kwa upana wake.

Hata hivyo, Rais Samia aliongeza kaulimbiu nyingine katika maadhimisho hayo akisema ‘Uadilifu na weledi kazini ndiyo chimbuko la maisha bora kwa wafanyakazi’.

Rais Samia amewahakikisha Tucta na vyama vya wafanyakazi kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kazi serikalini na sekta binafsi ili kupatikana ajira zenye usalama na staha kwa wote.