Rais kuteua ma-DED ngoma nzito

Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi

Muktasari:

  • Wadau wataka nafasi ziombwe kulingana na sifa zitakazoainishwa.

Dar es Salaam. Kauli ya Mbunge wa Mlimba (CCM), Godwin Kunambi ya kuhoji sababu za wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kuteuliwa na Rais, imewaibua wadau wakisema nafasi hizo ziombwe kulingana na sifa zitakazowekwa.

Suala la uteuzi wa wakurugenzi wa halmashauri, limekuwa likilalamikiwa na wadau na hasa baadhi ya vyama vya upinzani, vikidai kuwa nafasi hizo zinatumika kuweka upendeleo kwa CCM, hasa unapofika uchaguzi.

Mbali na vyama vya siasa, wadau mbalimbali wamekuwa wakikosoa uteuzi wa viongozi hao kwa kuzingatia zaidi vigezo vya kisiasa kuliko uwezo kitaaluma na uzoefu.

Suala hilo liliibua mijadala zaidi katika Serikali ya awamu ya tano ya hayati John Magufuli, aliyeteua watu mbalimbali, wakiwamo walioshindwa kwenye kura za maoni za CCM katika uchaguzi wa mwaka 2020, kuwa wakurugenzi wa halmashauri, makatibu tawala, wakuu wa mikoa na wilaya.

Uteuzi huo ulichukuliwa kuwa ni upendeleo wa kisiasa bila kujali vigezo vya utumishi wa umma, ukiwemo uzoefu wa kazi husika.

Hata hivyo, baadhi ya wateule hao walishaondolewa katika nafasi zao na kuhamishiwa katika nafasi nyingine serikalini.

Alichosema Kunambi

Akizungumza juzi wakati akichangia maoni yake kwenye hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji kwa mwaka 2024/2025 bungeni jijini Dodoma, Kunambi alishauri nafasi za wakurugenzi wa halmashauri zipatikane kwa watu kufanya usaili ili mamlaka ya uteuzi ipelekewe majina ya watu watatu ambao wanatokana na utumishi ili mmoja wao awe mkurugenzi.

“Nchi iliyobaki duniani, nchi inayoteua wakurugenzi wa halmashauri ni Tanzania peke yake kwenye sayari ya dunia. Ukienda South Africa (Afrika Kusini) wanaitwa managers (mameneja).

“Ili mkurugenzi wa halmashauri apatikane, anapitia mchakato wa ajira, lazima awe professional (mtaalamu). Yaani katika sehemu ambayo hatakiwi ateuliwe mwanasiasa, basi ni mkurugenzi wa halmashauri,” alisema.

Alishauri kuwa Rais apelekewe majina yaliyopitishwa kwenye usaili.

“Mpelekeeni majina matatu ya watu competent (watu mahiri) tutaona mambo mazuri. Sasa kwa sababu aligombea ubunge mweke pale, no no we can’t move like that (hapana, hapana hatuwezi kwenda kwa namna hiyo).

“As a nation we need to transform our mindset (Kama Taifa tunahitaji kubadilisha mtazamo).”

Kunambi, aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kabla ya kugombea ubunge mwaka 2020, alisema katika halmashauri hizo, kunatakiwa kuwe na kitengo cha mipango na uwekezaji na kwamba katika utumishi wake alikianzisha jijini humo.

Hata hivyo, wakati Kunambi akitoa maelezo hayo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi), Dk Adolf Ndunguru, alisema hayo ni mamlaka ya Rais.

“Uteuzi wa mkurugenzi ni mamlaka ya Rais, si mamlaka ya mbunge. Kama mbunge amehoji si mamlaka yake, kama amehoji ongea naye yeye; mwambie aendelee na maoni yake,” alisema.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 36(1) inampa Rais mamlaka ya kuanzisha na kufuta nafasi za madaraka ya namna mbalimbali katika utumishi wa Serikali.

Kifungu cha (2) kinasema, “Rais atakuwa na madaraka ya kuteua watu wa kushika nafasi za madaraka ya viongozi wanaowajibika kuweka sera za idara na taasisi za Serikali, na watendaji wakuu wanaowajibika kusimamia utekelezaji wa sera za idara na taasisi hizo katika utumishi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Aprili 23,2024, Ruth Mollel, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma), aliunga mkono kauli ya Kunambi, akisema nafasi hizo zinahitaji wenye sifa kitaaluma.

“Ingekuwa ni vizuri sana hizi kazi zitangazwe vigezo vijulikane, watu washindanishwe, wale watakaoshinda, basi apelekewe Rais afanye uteuzi, wale waliofanyiwa usaili na kuchunguzwa ili achague. Kwa hiyo mimi naungana na Mbunge wa Mlimba, Kunambi,” amesema.

Amesema kwa utaratibu uliopo sasa, uchunguzi kwa watumishi hao haufanyiki.

“Wewe hujaona mtu anatolewa hapa anapelekwa kule, hiyo vetting inafanywa saa ngapi? Haiwezekani mtu anateuliwa tu leo, lazima afanyiwe vetting kwanza, hata miezi mitatu au miwili,” amesema.

Amesema kabla ya utaratibu wa sasa wa Rais kuteua wanasiasa, awali wakurugenzi walikuwa wanachukuliwa kutoka miongoni mwa viongozi wa idara za halmashauri.

“Tulianzisha reforms (mabadiliko) kwenye utumishi wa umma zilizoweka vigezo vya kushindanisha, lakini kwa sababu nyingine zimeachwa,” amesema.

Ametaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na elimu na tabia za mtu. “Kwa hiyo unapotangaza mtu atajipima kama anavyo,” alieleza.

Naye Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe, aliyewahi kufungua kesi kupinga wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi, amesema nafasi hizo hazipaswi kuwa za kisiasa.

“Wakurugenzi wa halmashauri ni watumishi wa umma, sio wanasiasa. Kauli za Mbunge Kunambi zinaonyesha kuwa kuna watu wanateuliwa kisiasa, lakini hawana sifa, hawana uzoefu wala weledi,” amesema.


Kazi za halmashauri

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano, ibara ya 146 (2) Serikali za Mitaa inahusika na kuhakikisha utekelezaji wa sheria na ulinzi wa wananchi na kuimarisha demokrasia katika eneo husika na kuitumia demokrasia kuharakisha maendeleo ya wananchi.

Halmashauri za manispaa zimeanzishwa chini ya sheria za Mamlaka za Miji mwaka 1982, majukumu makuu ya Serikali za Mitaa ni pamoja na kusimamia na kudumisha amani, ulinzi na usalama katika maeneo ya mipaka yake, kuhamasisha/kuendeleza na kuwapatia huduma bora za kijamii na kiuchumi wananchi walio katika eneo la mipaka ya halmashauri.

Majukumu mengine ni kusimamia sera za maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo yao, kuchukua hatua madhubuti za kuhifadhi na kuendeleza mazingira, kusimamia utawala, fedha, mambo yote ya uendeshaji katika ngazi mbalimbali zilizo ndani ya mamlaka yake.

Mengine ni kusimamia na kuhakikisha demokrasia inadumishwa katika jamii, kukusanya mapato yatakayowezesha mamlaka ya serikali ya mtaa kuendesha shughuli zake pamoja na kutoa taarifa za matumizi kupitia kamati mbalimbali.