Profesa Kitila amkaribisha Boniface Jacob Ubungo

Dar es Salaam. Mbunge wa Ubungo (CCM), Profesa Kitila Mkumbo amemkaribisha mpinzani wake Boniface Jacob (Chadema) kufanya mikutano ya hadhara, akisema watashindana kwa hoja katika majukwaa.

Profesa Kitila aliyewahi kuwa mwanachama wa vyama vya Chadema na ACT-Wazalendo kwa nyakati tofauti alishindana kwa ukaribu na Jacob  katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ambao alimshinda meya huyo wa zamani wa Ubungo na Kinondoni.

Katika uchaguzi huo, Profesa Kitila aliibuka kidedea baada ya kupata kura 63,221 kati ya kura 89,656 na Jacob ambaye alikuwa diwani wa Ubungo alipata kura 20,620.

Profesa Kitila ameeleza hayo leo Jumatano Januari 4, 2023 katika mjadala wa ‘Twitter Space’ uliokuwa na mada ya ‘kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara na kuukwamua mchakato wa Katiba je ni mwelekeo mpya wa siasa nchini?

“Mimi kama mbunge wa Ubungo namkaribisha rafiki yangu Boniface Jacob aje kufanya mikutano aje na chama chake tupambane kwa hoja, tutamjibu kwa hoja,” amesema Profesa Kitila.

Kuhusu kuondolewa kwa zuio la mikutano ya hadhara, Profesa Kitila aliyewahi kuwa katibu mkuu wa wizara ya maji, amesema ni hatua kubwa na inakisia utuhubu na mwelekeo wa Rais Samia katika kuongoza nchi.

“Amekaa na viongozi wenzake na kujadili na kuona haja ya kuondoa zuio hilo. CCM imelipokea na hatuogopi kwa sababu mikutano ya hadhara imekuwa kwa muda mrefu na chama tawala imeshindwa kuanzia urais hadi ubunge.

“Katika bara la Afrika CCM inaendelea kufurahia sapoti ya wananchi na hakijawahi kuogopa mikutano ya hadhara,” amesema Profesa Kitila ambaye ni mtaalamu wa masuala ya elimu.

Jana, Januari 3, 2023, Rais Samia akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu Ikulu Dar es Salaam, aliruhusu mikutano ya hadhara iiliyokuwa ikililiwa kwa muda mrefu na vyama vya upinzani kutaka ruhusiwe.

"Uwepo wangu leo (jana) hapa mahali nimekuja kufanya ruhusa ya mikutano hii, nimekuja kutangaza kuondoa zuio la kuzuia mikutano ya hadhara na ninasema kwamba, sasa linaondoka,” alisema Rais Samia.