Polisi waimarisha ulinzi maandamano Chadema Dar

Muktasari:

  • Maandamano ya amani ya Chadema yamelenga kuishinikiza Serikali kuondoa miswada ya sheria za uchaguzi na vyama vya siasa bungeni

Dar es Salaam. Zaidi ya polisi 20 wameonekana maeneo ya Buguruni yanakoanzia maandamano ya Chama cha Demokrasia na  Maendeleo (Chadema) kupitia Karume- Kariakoo - Barabara ya Morogoro kuelekea Barabara ya Sam Nujoma eneo la Ubungo katika Jengo la PSSSF zilipo ofisi za Umoja wa Mataifa (UN).

Mbali na Buguruni, maandamano mengine yanaanzia Mbezi Mwisho kwenda Ofisi za Umoja wa Mataifa.

Lengo la maandamano hayo yaliyotangazwa Januari 13, 2024 ni kupinga miswada mitatu ya sheria za uchaguzi iliyowasilishwa bungeni Novemba 10, 2023 kwa kile Chadema wanachodai haijazingatia maoni ya wadau wengi wa demokrasia.

Pia, maandamano hayo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe yanalengo la kuitaka Serikali kushughulikia ugumu wa maisha unaowakabili wananchi.

Wakati maandamano hayo yakianza eneo la Buguruni, polisi waliovaa sare za Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wameonekana wakiwa kwenye magari na wengine wakitembea karibu na umati wa wafuasi wa Chadema.

Wafuasi hao wa Chadema wamevalia sare huku wakiwa na mabango ya ujumbe tofauti wameambatana na viongozi wa chama kuanzia ngazi za chini.

Baadhi ya viongozi walioambatana na wanachama hao ni Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema Hashim Juma Issa, Katibu wa Chadema Kanda ya Victoria, Zacharia Obadia, Naibu Katibu Mkuu Chadema Bara Benson Kigaila.

Wanachama hao wameonekana wakiwa na usafiri wa bodaboda, magari huku wengi wao wakiwa ni wale wanaojiandaa kutembea kwa miguu.

Akizungumza na waandishi wa habari latika eneo hilo leo, Jumatano Januari 24, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema, Hashim Jumma Issa amesema maandalizi yamekamilika na punde wataanza maandamano hayo.

“Mpaka sasa hakuna tukio lolote la uvunjifu amani lililotokea eneo la Buguruni na wanachama wanaendelea na kuimba nyimbo na kucheza ngoma,” amesema

Baadhi ya mabango yaliyoshikwa na waandamanaji yamesomeka; ‘Ugumu wa maisha sio mpango wa Mungu’ na jingine limesomeka, ‘Tunataka Katiba mpya itakayozaa Tume huru ya uchaguzi.'

Wakati huo huo, ulinzi umeimarishwa na Jeshi la Polisi maeneo ya Kariakoo, huku msafara wa maandamano ya Chadema unaoanzia Buguruni ukisubiriwa.

Mwananchi Digital imeshuhudia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) wamesimama katika vikundi wakiimarisha ulinzi.

Kwa upande wao wanachama na viongozi wa Chadema wameonekana wakiajiandaa na maandamano hayo maeneo ya Buguruni.

Maandamano hayo yaliyotangazwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe yana lengo la kuitaka Serikali kushughulikia ugumu wa maisha.