Ngorongoro yatengeneza barabara, vivuko kwa Sh1 bilioni

Ngorongoro yatengeneza barabara, vivuko kwa Sh1 bilioni

Muktasari:

  • Serikali imetaja namna ilivyokabiliana na uharibifu wa barabara zilizoharibika na mvua Wilaya ya Ngorongoro.

Dodoma. Serikali imesema ili kukabiliana na uharibifu wa barabara katika  Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro,  katika mwaka wa fedha 2019/20 imefanya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita  94.4, vivuko 15 na daraja moja kwa gharama ya Sh1.08 bilioni.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, David Silinde amesema hadi Aprili 2021, Serikali imeipatia Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Sh917.64 milioni kati ya Sh1.05 bilioni zilizotengwa katika mwaka wa fedha 2020/21 kwa ajili ya matengenezo ya barabara.

Alikuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM), Catherine Magige aliyetaka kujua iwapo Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kuongeza bajeti ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (Tarura) wilayani Ngorongoro, ili kukabiliana na uharibifu wa barabara uliotokana na mvua zilizonyesha msimu wa mwaka 2019 na 2020.

Naibu Waziri amesema katika kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa miundombinu ya barabara iliyotokana na mvua,  msimu wa mwaka 2019 na 2020, Tarura wameanza kukarabati barabara katika halmashauri hiyo na maeneo mengine nchini hata kwa kutenga fedha za dharura.

Silinde amesema katika mwaka wa fedha 2019/20 sambamba na matengenezo ya kawaida, Serikali iliipatia Tarura katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro Sh 276.68 milioni kwa ajili matengenezo ya dharura katika barabara zilizoharibiwa na mvua.

Amezitaja barabara zilizotengenezwa ni kipande chenye urefu wa kilomita 1.2 na makalavati 4 katika barabara ya Oldonyowas - Ormania – Piyaya, ujenzi wa makalvati 4 na madrifti 5 katika barabara ya Mdito – Digodigo Oldonyosambu na matengenezo ya kipande chenye urefu wa kilomita 1.5 na drifti 1 katika barabara ya Ormania – Oldonyorock.