Neema ya watalii yarejea Tanzania

Ofisa Uhifadhi mkuu, kitengo cha Sayansi ya Uhifadhi katika Hifadhi ya Tarangire, Gladis Ng’umbi.

Muktasari:

  • Uboreshwaji wa uwanja ndege wa Kuro uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, uliofanywa kwa fedha za Uviko-19 umechangia kuongeza watalii katika Hifadhi hiyo kutoka 78,946 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 288,444 mwaka 2022/2023.

Tarangire. Ni kama anga la Tanzania linazidi kufunguka katika sekta ya utalii na sasa uwanja wa ndege wa Kuro uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire unapokea ndege kati ya 13 hadi 18 kwa siku katika msimu wa utalii.

 Hii ni kutokana na kuboreshwa kwa uwanja huo na miundominu ya barabara iliyofanywa kwa fedha za Uviko-19 ambapo watalii wameongezeka katika Hifadhi hiyo kutoka 78,946 mwaka 2020/2021 hadi kufikia 288,444 mwaka 2022/2023.

Idadi hiyo inaweza kuongezeka zaidi kwa kuwa takwimu za watalii 288,444 ni za kipindi cha kuanzia Julai 2022 hadi Machi 2023 na idadi ya watalii imezidi kuongezeka kuelekea kuanza kwa msimu wa utalii (high season) mwezi Juni.

Septemba 2021, Tanzania ilipokea mkopo wenye masharti nafuu wa Dola 567.25 milioni sawa na Shilingi za Tanzania 1.291 trilioni kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo zilielekezwa sekta afya, elimu, maji na utalii na mazingira.

Akizungumza na wanahabari Alhamisi ya Aprili 27, 2023 kwa niaba ya mkuu wa Hifadhi hiyo, Mathew Mombo, Askari mkuu daraja la pili, Zakaria Natei, alisema ukarabati huo wa uwanja wa ndege umeondoa changamoto ya utuaji katika uwanja huo.

“Ukarabati umetusaidia sana ukilinganisha na siku za nyuma. Siku za nyuma ndege zilikuwa chache kuanzia ndege tano hadi 13 kwa siku. Tangu uwanja uboreshwe ndege zimeongezeka kuanzia ndege 13 hadi 18 msimu wa utalii,” alisema, Natei.

“Hii kwetu sisi ni faraja kubwa sana kwa sababu watalii wameongezeka na jambo ambalo tunajivunia. Tunaishukuru sana serikali kutupatia fedha za uviko. Ndege hizi zinazotua zingine ni za abiria 12 hadi 14 na zingine zinabeba watu 24”.

Kwa upande wake, Charles Nyaongo, ambaye ni Askari mwandamizi anayeshughulikia kitengo cha miundombinu, alisema Tarangire ina miundombinu ya barabara karibu kilometa 758 wanazozihudumia.

“Katika hizi fedha za Uviko-19 tuliboresha barabara zenye urefu wa kilometa 238 Kiukweli kabla ya kupokea fedha hizi na mitambi, hali ya miundombinu ilikuwa mbaya. Tunamshukuru sana Rais Samia (Suluhu) na Serikali,” alisema Nyaongo.

“Ndege sasa hivi zinatua. Uwanja wetu ulikuwa ni mbovu sana na kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa marubani na Tour Operators (Mawakala) kwa hiyo mradi wa Uviko umeboresha ule uwanja sasa hivi ni kicheko,” alieleza Afisa huyo.

“Tulitengeneza barabara za kimkakati na tulienda kwenye maeneo ya vivutio ambavyo watalii walikuwa wanashindwa kufika. Tulikwenda kwenye moja nzuri sana linaitwa Gurusi lina wanyama wengi lakini walikuwa hawawezi kufika,” alisema

Ofisa Uhifadhi mkuu, kitengo cha Sayansi ya Uhifadhi katika Hifadhi hiyo, Gladis Ng’umbi alisema mbali na mitambo ambayo hifadhi ilipokea, lakini walipokea Sh2.7 bilioni zilizotumika kuboresha uwanja na miundombinu ya barabara.

“Hii hifadhi inasifika sana kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya Tembo na inaitwa Paradiso ya Tembo lakini baadhi ya maeneo yalikuwa hayafikiki kiurahisi. Huu uwanja tumeweka moram urefu wa kilometa 1,200”alisema Ng’umbi.

Mhifadhi huyo alipongeza hatua ya Serikali kupitia kwa Rais Samia kuwapatia sehemu ya fedha hizo za mkopo kutoka IMF ambazo zimesaidia kuboresha hifadhi na kusema filamu ya Royal Tour imesaidia kuitangaza Tanzania kimataifa.

Ukiacha hifadhi hiyo ya Tarangire, lakini idadi ya watalii pia imeongezeka katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa) kutoka watalii 12,000 mwaka 2020/2021 hadi kufikia watalii 47,000 katika mwaka unaomalizikia Juni wa 2022/2023.