NCCR-Mageuzi wafanya mkutano mkuu Dodoma

Muktasari:

  • Chama cha NCCR- Mageuzi upande wa unaomuunga mkono, katibu mkuu, Martha Chiomba leo Jumamosi Septemba 24, 2022 unafanya mkutano wa dharura lengo likiwa ni kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mtazamo wa chama hicho kuwa na makundi mawili

Dodoma. Chama cha NCCR- Mageuzi upande wa unaomuunga mkono, katibu mkuu, Martha Chiomba leo Jumamosi Septemba 24, 2022 unafanya mkutano wa dharura lengo likiwa ni kujadili masuala mbalimbali ikiwemo mtazamo wa chama hicho kuwa na makundi mawili.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la chama hicho, Joseph Selasini amesema katiba ya chama hicho inasema kutakuwa na mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano.

Hata hivyo, amesema panapotokea dharura katiba hiyo inaruhusu kufanyika kwa mkutano mkuu wa dharura.

“Pamoja na mambo mengine, mkutano mkuu utakuja kujadili na kuamua kuhusu kauli kuwa chama kina makundi mawili,” amesema.

Mkutano huo unaofanyikia ukumbi wa St. Gasper umetanguliwa na vikao vya kamati kuu na halmashauri kuu ya chama hicho uliofanyika kuanzia juzi Alhamisi jijini Dodoma.

Awali, mkutano huo unafanyika huku upande wa unaomuunga mkono, mwenyekiti wa chama hicho James Mbatia ukilalamikia ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kubariki kufanyika kwa mkutano huo.

Msajili wa vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliwashauri kwenda mahakamani kwani ratiba ya mkutano huo ilimfikia kabla ya kufunguliwa kwa kesi hiyo.

Hata hivyo, NCCR-Mageuzi, upande wa Mbatia imekwisha kufungua kesi mahakamani pamoja na mambo mengine, uliomba kusimamishwa kwa mkutano huo.

Licha ya ajenda kutokujulikana, lakini miongoni ni kujadili mienendo ya viongozi akiwemo Mbatia.

Endelea kufuatilia mitandao yetu kwa habari zaidi