Mwanafunzi darasa la saba adaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya chandarua

Muktasari:

  • Kirugu amesema kuwa kwa zaidi ya miezi mitatu amekuwa akiishi na watoto wake saba bila ya uwepo wa mama yao na kuhakikisha wanapata mahitaji yote muhimu kama chakula na vifaa vya shule.

Morogoro. Mwanafunzi wa darasa la saba shule ya msingi Lukobe, Stephen Robert (13) amekutwa amejinyonga nyumbani kwao,  kwa kutumia kamba ya chandarua.

Akisimulia tukio baba mzazi wa mtoto huyo, Robert Kirugu ambaye ni dereva wa bodaboda, amesema wakati tukio hilo linatokea yeye alikwenda kwenye shughuli za utafutaji rizki na mama wa mtoto huyo alikwenda jijini Dar es Salaam kutafuta maisha, na kwamba mtoto huyo alikuwa akiishi na watoto wake wengine hapo nyumbani.

"Kabla sijatoka nyumbani kwenda kwenye utafutaji Stephen alinipa taarifa ya kuwepo kwa kikao shuleni kwao hivyo nilimwambia dada yake aende akasikilize kitakachoongelewa kwenye kikao hicho. Ilipofika mchana ndio nikapigiwa simu na kuambiwa Stephen amejinyonga na ameshafariki," ameeleza Kirugu.

Mwanafunzi darasa la saba adaiwa kujinyonga kwa kutumia kamba ya chandarua

Amesema kuwa hadi sasa bado hawajafahamu sababu zilichangia  mtoto huyo kujinyonga, na alipokagua begi lake la shule pamoja na madaftari hawajakuta ujumbe wala kitu kitu chochote.

Kirugu amesema kuwa kwa zaidi ya miezi mitatu amekuwa akiishi na watoto wake saba bila ya uwepo wa mama yao na kuhakikisha wanapata mahitaji yote muhimu kama chakula na vifaa vya shule.

"Mimi ni bodaboda lakini pia ni mfanyabiashara, mara zote kabla sijatoka asubuhi nahakikisha nimeacha pesa kwa ajili ya chakula na pia nimekuwa nikifuatilia kwa karibu tabia na mienendo ya watoto wangu pamoja na maendeleo yao ya shule," amesema Kirugu.

Amesema kwa sasa ameliachilia Jeshi la Polisi liendelee na uchunguzi zaidi, hata hivyo taratibu za mazishi zinaendelea na wamepanga kuzika kesho Ijumaa Februari 23 katika makaburi ya Kihonda Youth mission.

Naye mama wa mtoto huyo, Joyce Malanda amesema mpaka tukio hilo linatokea yeye alikuwa jijini Dar es Salaam ambalo alikwenda kutafuta vibarua Ili aweze kupata pesa za kurejesha madeni ya mikopo aliyochukua kutoka kwenye vikoba na taasisi nyingine za fedha.

"Muda wote niliokaa huko nilikuwa nikiongea na watoto wangu kwa simu akiwemo Stephen na nilikuwa nikimsisitiza asome kwa bidii Ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa mwanajeshi au mcheza mpira wa timu kubwa za kimataifa," amesema Joyce.

Ameongeza; "Mara ya mwisho kuongea na mtoto wangu ilikuwa ni wiki iliyopita aliniuliza mama utarudi lini nikamjibu nitarudi mwezi ujao na nitamletea zawadi nzuri, hivyo ajitahidi kufanya vizuri kwenye masomo yake na aendelee kuwa na tabia njema."


Amesema taarifa za kifo cha mtoto wake alizipata baada ya kufika Morogoro ambapo taarifa za awali alizopewa akiwa Dar es Salaam zilidai kuwa baba yake anaumwa sana hivyo allipofika Morogoro ndipo alipoelezwa ukweli kuwa mtoto wake amejinyonga na amefariki.

"Nilikuwa na madeni mengi lakini nimepambana kwa sasa yamepungua hivyo nilipanga kurudi Ili niendelee na biashara zangu ndogondogo na nitakachokipata niendelee kupunguza madeni yaliyobaki. Hiyo ndio sababu hasa iliyonifanya niondoke Morogoro na nikimbulie Dar es Salaam," amesema Joyce.

Amesema mtoto wake huyo ni wa tano kati ya watoto wake saba na pamoja na tabia njema aliyoninayo nyumbani, lakini hata shuleni alikuwa mtoto msikivu na aliyependa kusoma.

Kwa upande wake dada wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Esther Robert amesema kuwa yeye amepanga jirani na nyumbani kwao hata hivyo muda mwingi amekuwa akishinda nyumbani hapo kwa ajili ya kuwahudumia wadogo zake ikiwa ni pamoja na kuwapikia na kufuatia mienendo yao ya shule.

Amesema siku ya tukio alifika nyumbani hapo mapema kwa lengo la kuwaandaa wadogo zake waende shule. Hata hivyo,  Stephen (marehemu) alidai kuwa anaumwa kichwa na pia alimuelekeza kuwa shuleni kwao kuna kikao cha wazazi wa wanafunzi wa darasa la saba.

"Aliponiambia anaumwa kichwa nilimpa panadol nikamwambia akalale, nikampikia chai na nikamwachia hela ya kununua vitafunwa kisha nikaenda shule kwenye kikao na baada ya kutoka kwenye kikao nikaenda kazini ambako ndiko nilikopatia taarifa za tukio hili," amesema Esther.

Amesema kuwa mtu wa kwanza kugundua tukio hili ni mdogo wao wa mwisho anayesoma darasa la nne (jina limehifadhiwa) ambaye allirudi nyumbani akitokea shule na kukuta mlango wa mbele wa nyumba ukiwa umefungwa kwa ndani, hivyo alliamua kutumia mlango wa nyuma na alipoingia ndani alikuta vitafunwa aina ya kachori vikiwa mezani na alipoingia chumbani alikuta mwili wa Stephen ukiwa unaning'inia kwenye kenchi.

"Huyu mdogo wetu anaanza kumuita Stephen Kwa sauti kubwa na kuomba msaada kwa majirani ndipo watu walipokimbilia na kumpigia baba simu na baadaye na mimi nikapigiwa simu nikiwa kazini," amesema Esther.

Baadhi ya majirani wameeleza namna wanavyomfahamu mtoto huyo katika mazingira ya mtaani ambapo wamesema kutokana na tabia yake njema,  hawakutegemea kama angeweza kuchukua maamuzi magumu kama hayo.

Mmoja wa majirani hao Flora Katungutu amesema kuwa mbali ya kuwa mnyenyekevu lakini Stephen katika uhai wake alikuwa mtoto aliyempenda Mungu na Kwa kuthibitisha hilo alikuwa ni mmoja wa wanakwaya katika kabisa alilokuwa akiabudu.

Hilo ni tukio la pili kutokea eneo hilo ndani ya kipindi cha mwaka mmoja na kwa mujibu wa Mwenyekiti wa mtaa huo,  Omary Hassan amesema polisi wanaendelea kuchunguza kujua chanzo hasa cha matukio hayo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro,  Kamishna msaidizi mwandamizi wa Polisi,  Alex Mkama amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema kuwa uchunguzi bado unaendelea.