Mvua yaleta maafa Nachingwea

Wakazi wakiangalia mabaki ya nyumba zilizobomolewa kwa mvua

Muktasari:

Mkuu wa wilaya hiyo ameelezea athari hizo huku wananchi wakiiomba Serikali kuwasaidia.





Nachingwea. Mvua zinazoendelea kunyesha Wilaya ya Nachingwea, Mkoa wa Lindi zimesababisha maafa ya uharibifu wa mali na makazi ya watu katika maeneo mbalimbali wilayani humo, huku wakimwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamedi Moyo akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Machi 30, 2024,  amesema kaya takribani 1,660 makazi yao yameharibiwa na mvua hizo huku nyumba 699  zikibomoka kabisa.

"Mvua zilizonyesha na zinazoendelea kunyesha zimeleta athari kwa wananchi wetu, kuna kaya kama 1,660 nyumba zao zimebomoka, zingine kuta zimekatika na zingine zimetitia.

Moyo amesema nyumba nyingi walizozipitia wamebaini msingi wa nyumba hizo hauna ubora na umejengwa kwa tope na sio kwa saruji na msingi ni mfupi.

Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Nagaga kata ya Naipanga wameiyomba Serikali iwasaidie kupata makazi pamoja na chakula kutokana na mvua kuharibu nyumba zao na vyakula.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nagaga, Kata ya Naipanga, Thobiasi Hokororo amesema kijiji chao kimepata maafa makubwa kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kijijini kwao na kaya 330 zimepata madhara na nyumba 100 zimeanguka kabisa.

Amesema asilimia kubwa watu waliobomokewa na nyumba zao wanakaa kwenye nyumba za kuomba na nyumba hizo pia ni mbovu siku yoyote zinaweza kuanguka.

"Nimekutwa na majanga makubwa sana baada ya kunyesha mvua, nyumba yangu imebomoka jamii ndiyo imenisaidia kupata hiki kibanda ili niweze kujihifadhi, kwa umri wangu afya yangu siwezi tena kujenga naomba Mama Samia atusaidie," amesema Rose Hokororo

Suzana Damiani amesema nyumba yake yote imebomoka, vitu vyake vyote vimeharibika na kwa sasa hajui atawezaje kuishi kwani mme wake ni mlemavu na ana mtoto anayetakiwa kwenda chuo haelewi afanye nini.

Kwa upande wake, Diwani wa Naipanga, Geofray Kambona ameiomba Serikali iwasaidie wananchi wa kijiji cha Nagaga waliopatwa na majanga ya kubomokewa na nyumba zao.