Mvua yakwamisha shughuli kwa muda Dar

Hali ilivyokuwa eneo la Tabata Mwananchi Relini Dar es Salaam baada ya mvua kunyesha kwa saa tatu.

Muktasari:

 Barabara, mitaro yajaa maji, TMA yatabiri hali mbaya kwa baadhi ya maeneo

Dar es Salaam. Mvua kubwa iliyonyesha kwa takriban saa tatu katika Mkoa wa Dar es Salaam, imesababisha maji kujaa kwenye makazi ya watu, kusitisha shughuli za usafiri na biashara kwa muda katika baadhi ya maeneo.

Baadhi ya maeneo yaliyoathiriwa na mvua ni Kinondoni, Tabata, Sinza, Temeke, Mbweni, Tegeta, Boko, Bunju, Mwenge, Kunduchi na Bahari Beach, ambako maji yalijaa barabarani na kusababisha usumbufu kwa wasafiri.

Maeneo ya mito na mifereji ilijaa maji.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) juzi ilitoa taarifa ya hali mbaya ya hewa kwa siku tano.

Hayo yakitokea Serikali kupitia Msemaji wake, Mobhare Matinyi aliweka wazi athari zilizotokana na mvua za masika zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na hatua zilizochukuliwa.

Utabiri wa hali mbaya ya hewa uliotolewa na TMA juzi ulionyesha jana mvua ilinyesha maeneo mengi ya nchi.

Mikoa iliyotajwa katika taarifa hiyo ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara, Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Dodoma, Singida, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Njombe, Iringa na Songwe. Pia visiwa vya Unguja na Pemba.

Kwa leo, TMA imetoa angalizo la mvua kubwa kwa maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia) na visiwa vya Unguja na Pemba.

“Angalizo la upepo mkali unaofikia kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa kufikia mita mbili, limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa pwani ya Bahari ya Hindi (mikoo ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi na Mtwara pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba),” ilieleza taarifa hiyo.

Kiwango cha athari ambayo ilielezwa na TMA kutokana na mvua hizo ni wastani.

Kwa Aprili 24, TMA imetoa angalizo la mvua kubwa katika maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia) na visiwa vya Unguja na Pemba.

Pia, angalizo la upepo mkali wa kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayofikia mita mbili limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya ukanda wote wa Pwani ya Bahari ya Hindi (mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia), Lindi na Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.

Kiwango cha athari ambayo imeelezwa na TMA kutokana na mvua hizo ni wastani

TMA katika taarifa hiyo, imetoa angalizo kwa Aprili 25, la mvua kubwa katika Mkoa wa Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba.

Kiwango cha athari ambayo imeelezwa na TMA kutokana na mvua hizo ni wastani.

Athari za mvua

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Aprili 20, Matinyi alisema tayari vifo kutokana na mafuriko katika Halmashauri ya Mlimba mkoa wa Morogoro vimefikia 49.

Pia, alisema nyumba 1,276 zimebomolewa huku 7,731 zikizingirwa na maji eneo la Mlimba.

“Ekari 97,545.9 za mazao mbalimbali ya chakula zimeathirika. Kwa Mkoa wa Pwani ekari 105,296.24 za mashamba ya mazao ya chakula ziliathirika,” alisema.

Kwa Mkoa wa Mbeya, Matinyi alisema nyumba 20 zimeathiriwa na maporomoko ya tope kutoka Mlima Kawetere, Kata ya Itesi na kusababisha kaya 27 zenye watu 96 kukosa makazi.

Alisema watu wote walioathiriwa na mafuriko wapo katika makambi wakihudumiwa na Serikali kwa kupewa chakula, makazi, tiba, maji na usalama.

Matinyi alisema tathimini ya mafuriko ya mvua inaendelea kufanywa na watatoa taarifa ikiwamo idadi kamili ya vifo vilivyotokana na mafuriko.