Mvua yakwamisha mahudhurio ya wananchi sherehe za Muungano

Mwonekano wa Uwanja wa Uhuru leo Ijumaa Aprili 26, 2024. Picha na Sunday George

Muktasari:

Leo Ijumaa  Aprili 26, 2024, Tanzania inasherekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar  katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam

Dar es Salaam. Hali ya mvua inayoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam, imesababisha idadi ndogo ya wananchi kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Sherehe hizo zinazoendelea kufanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, hadi saa 4:50 asubuhi ya leo imeshuhudiwa idadi ndogo ya wananchi katika majukwaa ya uwanja huo.

Hali hiyo ni tofauti na miaka yote ambayo sherehe hizo hufanyika, aghalabu idadi kubwa ya wananchi hushuhudiwa katika majukwaa ya uwanja huo.

Lakini, kilichoshuhudiwa ni  makundi machache ya wananchi waliojigawa kwa mafungu wakikaa katika baadhi ya majukwaa ya uwanja wa Uhuru.

Ukiachana na eneo la jukwaa kuu, karibu robo tatu ya majukwaa ya uwanja huo, yalikuwa wazi.

Idadi ndogo ya wahudhuriaji katika maadhimisho hayo, imesababisha na mvua zinazoendelea kunyesha katika uwanja huo na maeneo mengine.

Mvua hizo zimesababisha wananchi wachache waliohudhuria katika sherehe hizo wakimbilie majukwaa ambayo hayafikiwi na maji iwapo mvua itanyesha.

Sherehe hizo zilizopangwa kuanza saa tatu, zilichelewa kidogo na kuanza saa 4 asubuhi kwa vikosi vya ulinzi na usalama kujipanga kwa ajili ya kuanza Gwaride.

Wageni mbalimbali wameendelea kuwasilia uwanjani hapo ambao miongoni ni Marais Azali Assoumani (Comoro), Evarist Ndayishimiye (Burundi), Dk William Ruto (Kenya), Nangolo Mbumba (Namibia), Hassan Sheikh Mohamud (Somalia), Hakainde Hichilema (Zambia), Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima na  Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo Felix Tshisekedi (DRC).

Kwa upande wa Tanzania waliokuwa wamefika ni Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa. Pia, wapo Rais mstaafu Jakaya Kikwete na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Miamvuli ndiyo iliyopamba shughuli hizo, kwani idadi kubwa ya wananchi waliokuwepo katika sherehe hizo walikuwa na miamvuli kujikinga na mvua.


Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi