Msigwa ataka mdahalo na Sugu uenyekiti Kanda ya Nyasa

Msafara wa wanachama wa Chdema wakimsindikiza Mchungaji Peter Msigwa kurudisha fomu ya kugombea uenyekiti wa Kanda ya Nyasa jijini Mbeya

Muktasari:

  • Mchungaji Peter Msigwa anatetea nafasi hiyo na leo Aprili 21, 2024 amerudisha fomu kuwania muhula wa pili katika nafasi ya mwenyekiti wa Chadema, Kanda ya Nyasa akishindana Joseph Mbilinyi “Sugu” aliyerudisha fomu jana Aprili 20, 2024.

Mbeya. Mgombea uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa amesema mkakati wa chama hicho ni kupambana na kushinda katika uchaguzi ujao.

Amesema iwapo atafanikiwa kutetea kiti hicho, atapambana kuhakikisha anapunguza udumavu uliopo katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini licha ya kuzalisha chakula cha kutosha.

Msigwa amemtumia salamu mgombea mwenzake, Joseph Mbilinyi “Sugu” kwenye nafasi hiyo, akiomba kuwekwa naye kwenye mdahalo mmoja kuulizwa maswali ya msingi akieleza kuwa licha ya urafiki wake na mpinzani huyo, lakini katika kinyang'anyiro hicho hajamwelewa.

Shughuli katika Mtaa wa Kabwe jijini Mbeya zimesimama kwa muda kufuatia mapokezi ya Mchungaji Msigwa aliyerudisha fomu kuwania nafasi hiyo.

Akizungumza baada ya kurudisha fomu hiyo, Msigwa amesema katika uongozi wake amefanya mambo mengi, lakini kwa sasa ameamua kurejea tena kupambana na udumavu na kushinda viti vyote katika uchaguzi ujao.

“Katika mikoa 12, mitano inatoka katika Kanda yetu kwa kuwa na udumavu, licha ya chakula cha kutosha kilichopo, lakini nahitaji kuona Chadema tunashinda kila kiti kwenye ngazi zote hadi uchaguzi mkuu 2025 tukichukua Urais.

“Lakini namuomba Katibu Mkuu, John Mnyika atupe mdahalo mmoja na Sugu ili tushindanishe sera zetu, tuone nani mwenye uwezo. Chama hiki kinahitaji watu wenye uwezo kukitangaza kama ambavyo tumeisimamisha Mbeya kwa muda,” amesema.

Ameongeza kuwa: “Niwashukuru na kuwapongeza kwa mapokezi haya makubwa na huu ndio ushindi rasmi umeanza, hadi sasa naona kura zangu ni 82 kati ya 103 za wajumbe wote, ambapo uhalisia nimeshashinda hao wengine watafute kazi nyingine.”

Msigwa alikuwa akishangiliwa wakati wote na wafuasi waliojitokeza kumsindikiza kurudisha fomu hiyo, kila alipokuwa akizungumza.

Mbunge wa zamani wa Tunduma, Frank Mwakajoka amesema ameamua kuungana na Msigwa kutokana na uwezo na weledi wake akieleza kuwa iwapo yeye atapewa kura za makamu mwenyekiti wa Kanda, watakuwa na mafanikio makubwa.

Amesema wanaombeza Msigwa kwamba hajafanya mambo makubwa, hawawezi kupoteza muda kwani kila kitu kipo kitakwimu, akieleza uwezo na uzoefu wao katika kazi za siasa hazina dosari.

“Mimi naomba mnipe ridhaa ya makamu mwenyekiti nikiwa chini ya Msigwa na kwa timu yetu tutakijenga chama na kanda yetu na tunawaahidi makubwa, chama chetu kimekua na kinahitaji viongozi makini,” amesema Mwakajoka.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee Chadema (Bawacha) mkoa wa Mbeya, John Mwambigija naye amesema wanayo imani na matumaini na Msigwa kutokana na uongozi wake aliouonyesha kwa kipindi kilichopita.

Amesema uwezo binafsi, uzoefu katika chama na uweledi alionao, ndiye anaweza kupambana na vyama vingine wakati wakielekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Ndio maana hata Serikali huweka masharti katika kuomba nafasi za kazi wakihitaji uzoefu, lakini tumeona hata mabadiliko yao CCM kwenye nafasi kubwa za utendaji, wakiwapa watu wenye uzoefu. Walimtoa Paul Makonda na kumpa Amos Makalla, hivyo hivyo kwa Balozi Dk Emmanuel Nchimbi.

“Hata sisi tunayo sababu ya kumpa nafasi tena Msigwa kuendelea kuongoza Kanda ya Nyasa kwani Sugu bado ni mwanafunzi kwenye siasa, asubiri tukimuhitaji huko mbeleni tutampa nafasi,” amesema.

Amesisitiza kwamba mtu anayeweza kupambana na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge ni Msigwa pekee na hivyo wanaamini watashinda kwa kishindo uchaguzi ujao.

Ameongeza kuwa suala la kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Chadema Kanda, tayari eneo lipo na kwenye akaunti zipo Sh2.6 milioni na wanasubiri uchaguzi uishe mchakato uanze rasmi.

“Sugu anatutisha na kiwanja chake kilichopo kwenye dampo la uchafu, kwani sisi tunataka magonjwa? Sasa niseme hivi kiwanja kipo na kimepimwa na Serikali na iwapo kitapata changamoto tutalipwa,” amesema kada huyo.

Naye wakili wa kujitegemea, Philip Mwakilima ambaye ni mweka hazina wa chama hicho, amesema Msigwa ndiye mtu sahihi na kuwa kiwanja cha ofisi kilisajiliwa kwa majina ya Chadema na siyo mtu binafsi.

Amesema Msigwa anacho kipawa na karama ya uongozi, anayeeleweka kwa yeyote na amewalea vijana wengi ambao kwa sasa ni viongozi katika nafasi mbalimbali akiwamo Fakhi Rulandala.

“Msigwa ni kiongozi mwenye maono, hata kwenye wasifu wake ameweka picha ya Rais Samia na wala si mtoto wake, anao udugu na familia ya Hayati Rais John Magufuli lakini hata siku moja hajawahi kukisaliti chama, huyu ndiye wa kwenda naye tena,” amesema Mwakilima.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Sumbawanga, Adolf Mkono amesema kwa kipindi hiki mtu sahihi kwa mustakabali wa chama katika kanda hiyo ni Msigwa kutokana na uimara aliouweka hadi sasa.

Amesema licha ya uwezo alionao Sugu, lakini kwa muda huu yupo mtu sahihi anayeweza kupambana kuifikisha Chadema katika mafanikio, akiahidi kuwa mkoa wa Rukwa uko pamoja na Msigwa.

“Sisi Rukwa kwa ujumla tunajua uwezo alionao Msigwa na nia yake ya dhati kuiongoza tena Chadema, tunataka mafanikio na yule Sugu asubiri muda wake, tukimtaka tutampa kwa muda wake,” amesema Mkono.

Mwenyekiti wa Chadema wilaya ya Rungwe, Gideon Mwakila amesema pamoja na Sugu kuchukua fomu, lakini lazima kila mmoja abaki kwenye nafasi yake, akisema Msigwa ni kiongozi bora aliyeonyesha mafanikio makubwa.

“Sugu abaki kwenye muziki wake, amuache Msigwa katika utawala, huyu ni kiongozi mwenye usikivu, anashaurika na kuunganisha chama bila kubagua, hivyo lazima tumkumbatie,” amesema Mwakila.

Ayoub Sikagonamo ambaye ni mwenyekiti wilaya ya Momba mkoani Songwe, amesema wanamuunga mkono Msigwa kwa kuridhishwa na msimamo wa chama kutokana na uimara wake na mafanikio aliyofanya.

"Hata hao wanaosema wamenunua kiwanja kwa ajili ya ofisi ni kutokana na kuona juhudi na kazi aliyoifanya Msigwa, wote hao wanakubaliana na ubora wake na sisi tunaungana naye kumpa mitano tena," amesema Sikagonamo.