Mpina aibua hoja tata bungeni

Mbunge wa Kisesa (CCM) Luhaga Mpina akizungumza wakati akichangia maoni yake kwenye makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma leo.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Mpina licha ya CCM wilayani Meatu kumuhoji, bado ameendelea kuwa moto, hapoi  leo amemshangaa Waziri Mkuu kutojiuzulu kwa maagizo yake kupuuzwa, amemshangaa Simbachawene kutozungumza kuhusu kauli ya Mkuu wa Majeshi kuhusu raia wa kigeni kuteuliwa na ametaka mawaziri, makatibu wakuu, ma-RC na ma-DC waombe kazi badala ya kuteuliwa.

Dodoma. 'Hajawahi kupoa.' Hilo ni neno unaloweza kulitumia pale unapomtaja Mbunge wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina ambaye ameendelea kuuwasha moto bungeni akitaka mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa wilaya na mikoa waombe kazi na kufanyiwa usaili badala ya kuteuliwa.

Mpina ambaye aliingia bungeni kwa mara ya kwanza mwaka 2005 na amekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa takriban miaka mitatu (2017-2020), licha ya Januari 25, 2024 kuhojiwa na Kamati ya Usalama na Maadili ya CCM, Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu, leo Ijumaa, Aprili 19, 2024, ameendelea ‘kukinukisha’ bungeni kwa kutaka utaratibu wa uteuzi usiwepo na watu waombe kazi na kufanyiwa usaili.

Mpina amesema hayo wakati akichangia kwenye mjadala wa taarifa ya utekelezaji wa mpango na Bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka 2023/24, ambayo imewasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene.

Wizara hiyo ndiyo inasimamia taasisi kadhaa zikiwamo za maadili ya viongozi wa umma na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Huku akimshangaa Waziri Simbachawene kwa kutosema lolote au kuonekana ameifanyia kazi kauli iliyotolewa Januari 2024 na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, kwamba kuna baadhi ya waomba hifadhi na wakimbizi wameajiriwa na kuteuliwa katika nafasi za kufanya maamuzi serikalini.

Jenerali Mkunda alitoa kauli hiyo kwa Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu wakati akifungua Mkutano wa Saba wa CDF na Makamanda.

“Tunao mfumo wa utumishi unaruhusu mpaka watumishi ambao sio raia wa Tanzania, mpaka viongozi ambao siyo raia wa Tanzania, lakini na taarifa hii imeshatolewa na vyombo vyetu vya dola, imeshatolewa na CDF, Jenerali Jacob Mkunda ambaye ni mkuu wa majeshi, ameshatoa taarifa hii.”

“Lakini, Waziri wa Utumishi na Utawala Bora yeye kwake hajaona kama ni changamoto wala hajazungumza suluhisho  la tatizo hili ni nini? Hawa waliotajwa kuteuliwa na kuajiriwa siyo raia wa Tanzania ni kina nani?”

Mpina hakuishia hapo amehoji utaratibu wa kufanya uchunguzi ‘vetting’ kwa wanaofikiriwa kuteuliwa na mamlaka ya Rais, kwamba hauwezi kuwafikia wananchi wote nchini kwa kuwa Tanzania ina watu 61 milioni.

“Lakini, pia teuzi na baadhi ya ajira kutolewa bila kufanyika kwa ushindani, kunafanya kupatikana viongozi dhaifu, watendaji dhaifu ambao wanashindwa kutekeleza majukumu yao.”

“Lakini, kumpa kazi kubwa mheshimiwa Rais kila wakati kutengua na kuteua, kazi kubwa kusoma ma-CV (wasifu) ya watu, wakati kazi hizi zingeweza kutangazwa tu, Watanzania wenye uwezo wakapata.

“Kwa nini waziri leo ateuliwe, kwa nini asishindane tu kwenye interview (usaili), kwa nini makatibu wakuu, kwa nini wakurugenzi, kwa nini wakuu wa wilaya, kwa nini wakuu wa mikoa, mwisho wa siku tungeweza kupata, lakini hata huu mfumo wa ‘vetting’ huu hauna garantii kuwapata Watanzania wote milioni 60, huwezi ‘guarantee vetting’. unampata wapi, unapendekeza huyu awe DC, unapendekeza huyu awe mkuu wa wilaya umempata wapi.

“Nani ameanzisha, maombi yamepatikanaje kwa mheshimiwa Rais maombi hayo, kwa hiyo tunajenga Taifa ambalo hatuwezi kupata viongozi wazuri.

“Lakini, pia mpaka sasa hivi watu wamepewa nafasi, anapewa nafasi ya ukurugenzi baadaye anakuja kutenguliwa, utawala unabaki uleule, haya mambo yanatupa tabu sana,” amesema.

Hata hivyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo ameomba kumpa taarifa Mpina kwamba anayoyazungumza yanagusa mamlaka ya Rais Kikatiba.

“Mtoa hoja amegusia kwamba mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa wilaya wanateuliwa teuliwa tu. lakini nataka nimpe taarifa kwamba mamlaka ya uteuzi kwa nafasi ambazo anataja ambaye na yeye amewahi kuteuliwa ni ya kikatiba.

“Kwa hivyo, kuna tofauti kati ya kuhoji Katiba na kuhoji matendo, anachokihoji ni Katiba, lakini nimtaarifu kwamba mamlaka hayo ambayo anayazungumzia kwa mheshimiwa Rais ni mamlaka ya kikatiba,” amesema Profesa Mkumbo.

Hata hivyo, Mpina amekataa taarifa hiyo na kuendelea kuchangia akitoa hoja nyingine ya kupuuzwa kwa maagizo ya viongozi.

“Viongozi wetu sasa wanapuuzwa, viongozi walioko juu wanaweza kuagiza na wakampuuza maagizo yake.

“Mfano mzuri, mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwahi kuagiza hapa maelekezo 12 katika Bunge hili kwa watendaji wa Serikali, hasa wale wa uhifadhi, lakini mpaka nikaja hapa bungeni na vielelezo na vithibitisho kwamba maelekezo ya Waziri Mkuu yamepuuzwa.

“Lakini yale niliyoyakataa na yale ambayo hata Ofisi ya Spika ilithibitisha Ofisi ya Waziri Mkuu inapuuzwa yanaendelea mpaka sasa hivi, na nilitegemea kwamba baada ya kupuuzwa kwa maelekezo haya ya Waziri Mkuu, moja waliyoyapuuza wangekuwa wamefukuzwa au Waziri Mkuu mwenyewe angekuwa ameshajiuzulu kwa sababu huwezi ukawa Waziri Mkuu halafu maelekezo yako yanapuuzwa,” amesema Mpina.

Mpina pia amepongeza mchango wa wabunge Esther Matiko na Mbunge wa Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangay: “Ukweli mliongea kwa hisia kubwa sana na mchango wenu ulinibubujisha machozi hapa bungeni.”

Kutowiana kwa taarifa

Pia, Mpina amesema kuna tatizo la kutowiana kwa taarifa ya uchunguzi na taarifa ya ukaguzi.

“Kumekuwa na shida kubwa Takukuru, Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP) wana taarifa zao, wakaguzi wana taarifa zao. wakaguzi wanakagua na kubaini kila aina ya wizi, kila dalili ya wizi katika maeneo husika, unaenda kwenye taarifa ya Takukuru hakuna hizo taarifa za wizi, hazijafanyiwa kazi mahala popote, hawasemi kama ni wizi au nini kilitokea.

“Mwaka jana hapa tuliona maeneo mengi ambayo yalikuwa na ishara kubwa sana za ufisadi na rushwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere na hata Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL zaidi ya trilioni 1.4 (Sh1.4 trilioni), lakini tuliona kwenye mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) zaidi ya trilioni 3.4 (Sh3.4 trilioni). Tuliona kwenye deni la Taifa mikopo inachukuliwa bila kufuata sheria zaidi ya trilioni 2.5 (Sh2.5 trilioni).

“Tuliona kwenye mikataba mingine ambayo fedha za umma zimetumika na mamilioni ya fedha yamepotea na wahusika wote wanajulikana, ukienda kusoma taarifa ya Takukuru hakuna taarifa hiyo.

“Ukisoma malalamiko yanayowasilishwa na taarifa ambayo PCCB (Takukuru) wanaifanyia kazi ni kama asilimia sita tu ya malalamiko yaliyowasilishwa, sasa hapo utazungumzia utawala bora, hapo utazungumzia ushughulikiaji wa rushwa, kama kwa mwaka unapokea malalamiko halafu unashughulikia kati ya asilimia 6.7 mpaka asilimia 23, utazungumzia utawala bora pale.

“Lakini kesi tunazoshindwa mahakamani ni wastani wa asilimia 43, yaani kesi ambayo imechunguzwa ina ushahidi PCCB wakajiridhisha, DPP akaidhinisha kwamba ni kweli tuna madai ya halali, mnaendaje kushindwa kesi mahakamani, mpaka asilimia 43 ya kesi mnapoteza mahakamani.

“Lakini, kumeendelea kuwa na mikataba ya siri, inafungwa hapa nchini, tuliambiwa kuna mikataba 43 ambayo ilifungwa hapa, lakini Watanzania hatujaelezwa,” amesema.