Mke wa Sumaye aibuka kidedea kortini

Muktasari:

  •  Katika kesi hiyo, Esther Sumaye alikuwa ameiomba Mahakama itamke Jimmy Mushi ni mvamizi wa shamba namba 25 lililopo Madale eneo la Wazo

Kilimanjaro.

Esther Frederick Sumaye

ambaye ni mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameibuka kidedea katika kesi ardhi ya kugombea shamba namba 25 lililopo Madale eneo la Wazo Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Jaji Elinaza Luvanda wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi aliyesikiliza kesi hiyo namba 99 ya 2023 kati ya Esther na Jimmy Mushi, alimnyima Esther fidia maalumu ya Sh500 milioni baada ya kushindwa kuwasilisha ushahidi.

Hukumu hiyo imetolewa jana Aprili 25, 2024 baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili za mgogoro huo na kumtamka Esther aliyefungua kesi hiyo ya madai, kuwa ndiye mmiliki halali wa shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 1.90 likiwa na hati namba 53085.


Katika kesi hiyo, Esther Sumaye aliiiomba Mahakama itamke Jimmy Mushi kama mvamizi wa shamba hilo, amri ya kumtaka kuondoka eneo hilo na kumlipa fidia ya Sh500 milioni baada ya Esther kushindwa kulitumia kipindi chote alicholihodhi.

Mbali na kuomba amri hizo, lakini Esther Sumaye aliiomba Mahakama itoe amri ya kudumu ya kuwazuia mdaiwa (Mushi), mawakala wake na mtu yeyote mwingine atakayemtuma, kuingia kwa jinai katika shamba hilo na kulipa gharama za kesi hiyo.


Walivyochuana mahakamani

Katika ushahidi wake, Esther alieleza kuwa yeye ndio mmiliki halali alilipata shamba hilo kama zawadi kutoka kwa mjomba wake aitwaye Pantaleo Tumbo Kyisima aliyekuwa pia shahidi wa kwanza ambaye naye aligawiwa eneo hilo na Tegeta.

Esther alilipata shamba hilo kutoka kwa mjomba wake huyo Agosti 6,1997 huku mjomba wake akiwa ndiye alikuwa mmiliki wa mwanzo akilipata Juni 27,1991 kutoka Halmashauri ya Kijiji cha Tegeta na katika kuthibitisha hilo, aliwasilisha stakabadhi.

Hata hivyo, mdaiwa yeye katika ushahidi wake wa utetezi ameeleza kuwa alilipata eneo lenye ukubwa futi 60 kwa 40 kama zawadi kutoka kwa baba yake aliyemtaja kwa jina la Peter Mushi ambaye alipewa eneo hilo na Serikali ya Kijiji cha Tegeta Februari 15,2005.

Kulingana na mdaiwa, baba yake aligawiwa kwa barua hekari tatu za ardhi na Serikali ya kijiji hicho cha Tegeta Machi 20, 1991 na tangu kipindi hicho hadi hukumu inatoka ikiwa ni miaka 33 imepita, amekuwa akimiliki ardhi hiyo pasipo usumbufu wa aina yoyote.

Lakini mdai katika shauri hilo (Esther) naye alieleza Mahakama kuwa alikuwa akifurahia umiliki huo wa shamba lote hilo bila bughudha yoyote hadi mwaka 2015 ambapo mdaiwa alipoingia na kuvamia eneo lake.


Hukumu ya Jaji ilivyokuwa

Baada ya mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja zao, Jaji Luvanda alisema kuhusu kama mdai ndiye mmiliki halali, kwa mtazamo wake, Esther Sumaye ambaye ana hati ya umiliki aliyoipata 2002 anaonekana kuwa na hati nzuri.

“Hii ni kwa sababu hati yake  ilithibitishwa kuwa ilipatikana kama zawadi ya kupewa na mjomba wake na pia shahidi wa kwanza (mjomba) amethibitisha kuwa aligawiwa eneo hilo na serikali ya kijiji cha Tegeta mwaka 1991 kulingana na vielelezo,” amesema Jaji.

Jaji amesema, ushahidi kuwa baada ya kukabidhi futi 40 kwa 60, mdaiwa alibaki na jukumu la kuwa mwangalizi wa shamba lililobaki la baba yake, lakini hilo halikuelezwa popote kwa majibu ya kesi hiyo wala katika ushahidi wake wa msingi,” amesema Jaji Luvanda.

Kwa mujibu wa Jaji, madai kuwa baba wa mdaiwa alipewa ardhi na Serikali ya Kijiji cha Tegeta Machi 20, 1991 haikusemwa popote katika majibu yake ya maandishi ya utetezi.

Jaji ameeleza kuwa, mdaiwa alishindwa hata kueleza ukubwa wa kipande cha shamba la baba yake kilichobaki baada ya kumpa ardhi yenye ukubwa wa futi 40 kwa 60 na hata hoja kuwa baba yake ni mzee na anaumwa haikusemwa kwenye majibu ya utetezi.

Mbali na hoja hiyo, Jaji amesema mdaiwa pia alishindwa kueleza ni lini hasa baba yake aliamua kwenda Kijiji cha Uru Moshi na alishindwa kueleza kwa nini Februari 14,2005 alipompa mdaiwa sehemu ya ardhi, mdaiwa akabaki kuwa mwangalizi.

Jaji amesema hiyo inapingana na shahidi wake wa pili, Gration Mbelwa ambaye amesema Peter Mushi na familia yake walikuwa wakiishi Tegeta kipindi chote na hata shahidi wake wa 44, Waumoja Puga hakueleza chochote kuwa baba wa mdaiwa alihamia Moshi.

Kwa mujibu wa Jaji, yapo mashaka yaliyoonyeshwa na Wakili Elly Mkwawa aliyekuwa anamwakilisha Esher Sumaye kuhusu uhalisia wa kielelezo cha utetezi D3 na  alisema kwa kukitizama, wino uliotumika unaonekana ni mpya na mwandiko unaonyesha ni wa siku za karibuni.

Wakili Mkwawa amesema ukilinganisha wino huo na nyaraka iliyoandikwa miaka 19 iliyopita ni vitu viwili havifanani.

“Yote kwa yote, kielelezo hicho kilitaja eneo mahsusi la kipande cha ardhi cha futi 40 kwa 60, lakini hakikuonyesha ukubwa wa shamba lote lenye ukubwa wa hekari tatu linalodaiwa baba wa mdaiwa aligawiwa Machi 20,1991,” amesema Jaji.

Katika hitimisho lake, Jaji Luvanda amesema kwa kuwa tayari Mahakama imeamua kuwa shamba hilo ni mali ya Esther Sumaye, hoja ya kutolewa uamuzi na Mahakama ni kama mdai anastahili kulipwa fidia ya Sh500 milioni alizoziomba katika hati ya madai.

Jaji amesema katika madai hayo, mbali na kuomba kulipwa Sh500 milioni, aliomba kulipwa riba ya malipo hayo, hasara yoyote aliyoipata kwa mdaiwa kuhodhi shamba lake baada ya kulivamia na pia Mahakama imuamuru kulipa gharama za kesi.

Wakati akihojiwa maswali ya dodoso na Wakili Sarah Matembo aliyekuwa anamtetea mdaiwa, Jaji amesema mdai alieleza kuwa, hakuwa amewasilisha ushahidi wa hasara inayohitaji fidia ya Sh500 milioni lakini shahidi wake wa tatu akasema ungeelezewa baadaye.

Hata hivyo, Jaji amesema baada ya ushahidi huo, wakili wa mdai alifunga kesi yao.

Jaji Luvanda amesema Esther Sumaye mmiliki halali wa shamba hilo namba 25 lenye hati miliki namba 53085 na mdaiwa atawajibika kulipa gharama za kesi hiyo.